TIMU ya Simba leo inaingia katika uwanja wa Mkapa mkoani Dar es Salaam kuikabili Azam FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaoanza saa 1:00 usiku.
Wekundu hao wa Msimbazi watajaribu kurudisha furaha kwa mashabiki wake baada ya kushindwa kupata walau alama moja katika michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya AC ya Guinea na Raja Casablanca ya Morocco.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana Oktoba 27 katika uwanja wa Mkapa, Dar mchezo ambao wenyeji Azam walifanikiwa kuondoka na alama zote tatu kwa bao 1-0 lililofungwa na Prince Dube.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kocha wa timu ya Simba Roberto Oliveira amesema kupoteza michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa sio sababu ya wachezaji wake kuwa na morali ya chini hivyo anatarajia kupata matokeo mazuri leo.
“Tumecheza vizuri sana mechi ya Ligi Kuu iliyopita dhidi ya Singida ingawa hatujafanya vema katika mechi za kimataifa haiwezi kuwa sababu ya kushindwa kupata alama tatu dhidi ya Azam hivyo tunaingia uwanjani akili zetu zikiwaza ushindi ili tuendelee kusalia katika nafasi nzuri ya kuwa bingwa wa Ligi Kuu NBC msimu huu” alisema Roberto
Naye kocha msaidizi wa timu ya Azam John Matambala amesema kuwa wamefanya marekebisho katika baadhi ya maeneo katika kiwanja cha mazoezi kwa takribani wiki mbili hivyo wako tayari kupambana kwaajili ya kupata alama tatu.
“Kiuhalisia timu yetu imekuwa na muendelezo wa matokeo yasiyoridhisha tangu kuanza kwa duru la pili hivyo lazima tujiandae kurekebisha makosa yetu ya nyuma na tuingie kwa tahadhari kubwa dhidi ya Simba kwani tukidharau tunaweza kupoteza mchezo huu” alisema Matambala.
Azam itaingia uwanjani bila huduma ya kinara wao wa mabao Idris Mbombo mwenye mabao saba na nahodha Bruce Kangwa wenye kadi tatu za njano.