TIMU ya Yanga leo inaingia uwanjani ikiwa ugenini dhidi ya KMC kutafuta rekodi mpya ya kushinda katika michezo kumi mfululizo ya Ligi Kuu ya NBC kwenye uwanja wa Mkapa mkoani Dar es Salaam.
Mechi hiyo itakayochezwa saa 10:00 alasiri inakutanisha KMC ambayo haijapata matokeo katika mechi tano mfululizo dhidi ya Yanga iliyofanikiwa kushinda mechi tisa mfululizo za Ligi Kuu ya NBC.
KMC imeshinda mechi moja pekee dhidi ya Yanga kati ya tisa zilizopita, sare mechi mbili na kupoteza michezo sita huku ikiwa imeruhusu mabao 12 katika mechi hizo.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kocha msaidizi wa timu ya KMC Ahmad Ally amesema kuwa wanatambua uwezo wa Yanga na wamejipanga kushindana kupata ushindi.
“Tunakwenda kucheza dhidi ya timu bora inayoshiriki mashindano ya kimataifa, kinara wa Ligi na yenye muendelezo wa matokeo mazuri hivyo tumejiandaa vizuri kuchukua tahadhari na tupo tayari kupambana ili kupata alama tatu muhimu” alisema Ahmad.
Timu ya Yanga inaingia katika mchezo huo siku tatu baada ya kupata ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe na endapo itapata ushindi leo itaongoza kwa tofauti ya alama nane dhidi ya timu ya Simba inayoshika nafasi ya pili.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari kocha msaidizi wa Yanga Cedric Kaze amesema sherehe za ushindi dhidi ya Mazembe zimekwisha hivyo nguvu zimeelekezwa katika mchezo wa Ligi Kuu leo ili kutetea ubingwa msimu huu.
“Hakuna siku tumewahi kucheza na KMC mechi ikawa rahisi hivyo tunaelewa ugumu wa mechi ya leo na kama tukiwa vizuri katika kila idara kwenye timu yetu tutafanikiwa kushinda na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa msimu huu” alisema Kaze.