TIMU ya Kagera Sugar imeendeleza rekodi mbaya ya mwanzo wa msimu wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kufungwa bao 1-0 na Ihefu ya Mbeya.
Kagera Sugar tayari imepoteza michezo miwili msimu huu dhidi ya Mashujaa na Ihefu idadi sawa na michezo miwili ya mwanzo msimu uliopita ilipofungwa na timu za Azam na Simba.
Bao la Ihefu limefungwa na Moubarack Amza na kuifanya Ihefu kupata ushindi wa kwanza msimu huu baada ya kufungwa na Geita Gold mchezo wa mzunguko wa kwanza.
Timu ya Namungo imeendelea kusota uwanja wa nyumbani baada ya kushindwa kupata ushindi na kuambulia sare ya bao moja dhidi ya KMC ya Dar.
Namungo iliyopoteza mchezo wa ufunguzi dhidi ya JKT iliyopanda daraja kwa bao moja imeambulia alama moja pekee ikiwapeleka nafasi ya tisa katika msimamo wa Ligi Kuu NBC.
Ligi hiyo itaendelea kesho Agosti 20 kwa michezo miwili kati ya Mtibwa na Coastal Union uwanja wa Manungu, Morogoro saa 8:00 mchana na Simba itakakua mwenyeji wa Dodoma Jiji kwenye uwanja wa Uhuru, Dar saa 10:00 alasiri.