LIGI ya NBC Championship inafika tamati leo kwa michezo nane ya mwisho kupigwa kuhitimisha jumla ya michezo 240 ya Ligi hiyo huku Michezo yote ikipigwa kuanzia saa 10:00 alasiri.
Vita ya Ubingwa leo itamtambulisha rasmi bingwa wa NBC Championship msimu 2023/2024 huku Ken Gold ikiwa tayari imekata tiketi ya kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025 itahitaji alama moja pekee ili kutangazwa bingwa.
Timu ya Pamba itahitaji kushinda dhidi ya Mbuni na endapo Ken Gold itapoteza mchezo wa leo timu ya Pamba itafanikiwa kuwa bingwa wa NBC Championship msimu huu.
Vita ya kupanda daraja moja kwa moja kwenda Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025 itamalizika leo ambapo ni Pamba au Mbeya Kwanza wenye nafasi hiyo, Pamba inahitaji kushinda ili kujihakikishia alama 65 ambazo haziwezi kufikiwa na Mbeya Kwanza huku Mbeya Kwanza inahitaji kushinda na kuiombea Pamba ipoteze ili ipate nafasi hiyo.
Upande wa ufungaji wa mabao bado safari haijafika mwisho ambapo Edger William wa Ken Gold anashika usukani akiwa na mabao 20 huku Boban Bogere wa Biashara United akifuatia kwa karibu akiwa na mabao 19, Oscar Mwajanga wa Mbeya Kwanza na Maulid Shaban wa Mbeya City wanafuatia kila mmoja akiwa na mabao 17, je ni nani kuwa kinara wa Mabao msimu huu ?