TIMU za Kiluvya ya Dar es Salaam na African Sports ya Tanga zimefanikiwa kutinga fainali ya mashindano ya First League Nane Bora baada ya kushinda michezo yao ya nusu fainali.
Kiluvya iliyocheza dhidi ya Malimao ya Dar es Salaam imeshinda kwa mikwaju ya penati 4-2 baada ya kutoka suluhu katika dakika 120.
African Sports ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Mwadui ya Shinyanga kwenye mchezo ulioshuhudia Mwadui wakionyeshwa kadi mbili nyekundu huku moja ikionyeshwa baada ya vurugu zilizotokea uwanjani dakika chache kabla ya mchezo kumalizika.
Matokeo hayo yanazifanya timu za Kiluvya na African Sports kufuzu moja kwa moja kucheza Ligi ya Championship ya NBC msimu wa 2024/25 huku fainali ya mashindano hayo ikitarajiwa kupigwa Mei 11, kwenye uwanja wa Mkwakwani ili kupata bingwa wa First League msimu wa 2023/24.
Timu za Mwadui na Malimao zitacheza mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu Mei 11 huku pia zikiwa na nafasi ya kupanda daraja msimu ujao ikiwa zitashinda michezo ya mtoano dhidi ya timu za Ligi ya Championship zitakazofungwa michezo ya mtoano.