Author: Cynthia Michael

AZAM HAIJAPOTEZA MCHEZO KWENYE LIGI KUU YA NBC.

LIGI kuu ya NBC imeendelea kwa timu ya Azam kuwakaribisha TRA United katika dimba la Azam Complex kwenye pambano lililokuwa na ushindani mkubwa na Azam ikiibuka mbabe kwa kushinda mabao 2-0.

Azam wakicheza nyumbani walianza mchezo kwa kasi wakitawala umiliki wa mpira na kutengeneza nafasi zilizozaa matunda baada ya Jean Ngite kufunga bao la kuongoza dakika ya 28.

Kipindi cha pili dakika ya 70 Iddi Nado aliongeza bao la pili na kuwaamsha mashabiki wa Azam waliofurahia timu yao kuongeza bao na kumaliza na ushindi hivyo kusogea hadi nafasi ya tano ikifikisha alama 16.

Kwa matokeo hayo timu ya TRA United inashika nafasi ya 9 ikiwa na alama 12 katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC huku mchezo unaofuata itakuwa mgeni wa timu ya Coastal Union iliyopata sare katika mchezo uliopita nyumbani dhidi ya KMC inayoshika mkia kwenye msimamo.

MTIBWA YAENDELEZA MOTO LIGI KUU YA NBC

TIMU ya Mtibwa Sugar imefanikiwa kuondoka na alama tatu muhimu baada ya kuifunga Pamba Jiji bao moja katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliochewa katika dimba la Jamhuri mkoani Dodoma.

Mchezo huo uliokuwa mkali tangu mwanzo ulishuhudia timu zote zikicheza kwa tahadhari kubwa huku kila moja ikilenga kutumia vizuri nafasi zilizojitokeza ingawa wababe hao walienda mapumziko bila bao kupatikana.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kutengeneza nafasi na dakika ya 90+3 Twalib Hassan aliibuka shujaa wa Mtibwa Sugar baada ya kufunga bao la ushindi akitumia vyema nafasi ya mwisho na kuamsha shangwe kubwa kwa benchi la ufundi na mashabiki wa timu hiyo.

Bao hilo lilitosha kukusanya alama tatu kwa ‘wakata miwa’ huku Pamba Jiji ikilazimika kuondoka mikono mitupu licha ya kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo.

James Mwashinga wa Pamba aliibuka mchezaji bora wa mchezo huo licha ya timu yake kupoteza dakika za mwisho.

Mchezo wa mapema ulishuhudia ‘maafande’ wa Tanzania Prisons na JKT Tanzania wakigawana alama baada kutoka suluhu kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.

MTIBWA SUGAR YASOGEA NAFASI YA NNE LIGI KUU YA NBC

 

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kwa mchezo mmoja uliochezwa katika uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma na kushuhudia Mtibwa sugar ikifanikiwa kuondoka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City.

Mtibwa Sugar ilianza mchezo kwa kasi na dhamira ya kutafuta ushindi mapema na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 27 baada ya George Chota kufunga bao la kwanza kwa shuti lililomshinda kipa wa Mbeya City Beno Kakolanya na kuwapa wenyeji uongozi wa 1-0.

Mbeya City haikukata tamaa na dakika ya 45+2 Eliud Ambokile aliisawazishia Mbeya City bao baada ya kutumia vyema krosi ya beki wa kulia Maranyingi na kufanya matokeo kuwa 1-1 hadi mapumziko.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa kutoka Mtibwa Sugar wakitafuta bao la ushindi na dakika ya 63 Said Mkopi aliibuka shujaa baada ya kufunga bao la pili kwa ustadi mkubwa lililowarejesha Mtibwa Sugar mbele na matokeo kuwa 2-1.

Mbeya City ilijaribu kurejea mchezoni kwa kuongeza kasi ya mashambulizi lakini safu ya ulinzi ya Mtibwa Sugar ilisimama imara hadi filimbi ya mwisho na kuhakikisha wanachukua alama tatu muhimu huku timu hiyo ikipanda hadi nafasi ya 4 kwenye msimamo wa Ligi Kuu wakifikisha na alama 14.

 

YOUNG AFRICANS ‘YAICHAPA’ MASHUJAA LIGI KUU YA NBC.

Young Africans imeendelea kuonyesha ubora wao katika Ligi Kuu ya NBC ilipokutana na Mashujaa katika wa uwanja KMC Complex baada ya kuichapa Mashujaa mabao 6-0.

Kikosi cha Young Africans kilitawala mchezo kuanzia dakika ya kwanza hadi mwisho huku wachezaji sita wakiandika majina yao kwenye orodha ya wafungaji.

Bao la kwanza lilifungwa mapema dakika ya 8 na Mohamed Damaro na dakika ya 28 Duke Abuya aliongeza bao la pili baada ya kumalizia pasi safi kutoka kwa Maxi Nzengeli.

Dakika saba baadae Pacome Zouzoua aliweka bao la tatu kwenye dakika ya 35 na Young Africans kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao matatu.

Kipindi cha pili Young Africans waliendelea kushambulia bila kuchoka na alikuwa Prince dube alifunga bao la nne dakika ya 79 kabla ya Mudathir Yahya kuongeza bao la tano dakika moja baadae na msumari wa sita wa ‘Wananchi’ ulipigiliwa na mshambuliaji wao mpya Laurindo Dilson ‘Depu’.

Ushindi huu unaipeleka Young Africans ‘kileleni’ mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Katika mchezo huu Mudathir Yahya alikuwa mchezaji bora wa mchezo huu

HAWA HAPA WAKALI WA ‘GUU’ LA KULIA KWENYE LIGI KUU YA NBC.

WAKALI wa kutumia mguu wa kulia katika kufunga mabao ndani ya Ligi Kuu ya NBC wanazidi kuongezeka kadri Ligi inavyozidi kuendelea ikiwa ni mzunguko wa sita wa Ligi .

Maxi Nzengeli mchezaji anaecheza eneo la kiungo katika timu ya Young Africans amefanikiwa kuifungia mabao mawili timu yake akitumia ufundi wa mguu wake wa kulia na kuwa tishio kwa mabeki wa timu pinzani.

Peter Lwasa kiungo mshambuliaji anaekipiga kwenye timu ya Pamba Jiji nae amekuwa hodari na mguu wake wa kulia kwa kuifungia mabao mawili timu yake ndani ya msimu huu.

Mshambuliaji wa timu Mashujaa Mundhir Vuai aliyeanza msimu kwa kiwango bora ameingia pia kwenye orodha hiyo akiwa ameshatupia mabao mawili kwa ufundi wa mguu wake wa kulia.

Coastal Union nao wanatamba na mshambuliaji wao Athuman Makambo ambaye aliwika akiwa mfungaji bora wa Ligi ya Vijana akiwa na Mtibwa Sugar amefanikiwa kufunga mabao mawili kwa ‘guu’ lake wa kulia.

‘Kino Boys’ timu ya KMC inawakilishwa na Darueshi Saliboko ambaye amefunga mabao mawili kwa mguu wake wa kulia huku moja ya bao hilo likiwa bao la kwanza la msimu wa 2025/2026.

Mkongwe Vitalis Mayanga wa timu ya Mbeya City anazidi kuwafundisha vijana kuwa mguu wake wa kulia bado upo vizuri akifanikiwa kufunga mabao mawili ndani ya msimu huu.

Andy Boyeli ambaye jina lake halikuimbwa sana wakati wa usajili wake ni mshambuliaji wa timu ya Young Africans ambaye hadi sasa amefanikiwa kutikisa nyavu za wapinzani mara mbili kwa mguu wake wa kulia akifunga yote kwenye mchezo dhidi ya KMC.