Author: Cynthia Michael

CHAMPIONSHIP 2026/27 KUANZA RASMI LEO.

Ligi ya Championship ya NBC msimu 2026/27 inaanza rasmi leo kwa michezo mitatu itakayochezwa katika viwanja tofauti huku timu zikianza safari ya kuwania nafasi za kupanda Ligi Kuu ya NBC.

Mchezo kwanza utapigwa katika uwanja wa Ali hassan Mwinyi mkoani Tabora timu ya Rhino Rangers itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons kwenye mchezo utakaorushwa mubashara kupitia chaneli ya FIFA+.

Dar es salaam, KMC itawakaribisha Mbuni katika uwanja wa KMC katika mchezo utakaoonyeshwa kupitia Ligi Kuu TV kupitia mtandao wa youtube.

Katika mchezo mwingine katika mkoa wa Dar es salaam kigamboni united itakuwa mwenyeji wa TMA katika uwanja wa uhuru , na michezo yote itapigwa saa 10:00 alasiri.

Ufunguzi huo unatarajiwa kuleta ushindani mkubwa kutokana na kila timu kuanza msimu zikiwa na malengo mapya huku mashabiki wakisubiri kuona kiwango cha timu zao baada ya maandalizi ya msimu mpya.

GEITA ‘YAUA’ BUKOMBE, SIMBA IKIENDELEZA UBABE LIGI KUU YA NBC.

Ligi Kuu ya NBC imeendelea kwa michezo miwili iliyotoa burudani kubwa kwa mashabiki, Singida Black Stars waliwakaribisha simba na kupoteza 1-2 kwenye uwanja wa Airtel mkoani Singida huku Geita Gold ikianza vyema kwenye uwanja wake mpya kwa ushindi mnono wa mabao 6-2 dhidi ya Kagera Sugar.

Clatous Chama aliifungia Simba bao la kwanza dakika ya 12, Sheikhah Ibrahim wa singida akaweka mzani sawa dakika ya 22 na kuwainua mashabiki wa Singida.

Hata hivyo, Simba ilirejea ikiwa na nguvu zaidi kipindi cha pili na kufanikiwa kuongoza mchezo kupitia Rushine De Reuck, aliyefunga dakika ya 62.

Mchezo huo pia ulishuhudia Simba ikicheza ikiwa pungufu baada ya Anthony Mligo kuonyeshwa kadi nyekundu na kuwa mchezo wa tatu mfululizo Simba kupata kadi nyekundu tangu ligi ianze.

Katika mchezo mwingine uliochezwa Uwanja wa kisasa wa Bukombe, mkoani Geita, ambapo Geita Gold ilianza kwa kishindo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 6-2 dhidi ya Kagera Sugar.

Mchezo huo ulikuwa wa kipekee kwa timu hizo mbili ambazo zimepanda kutoka Championship na kushiriki Ligi Kuu, huku ikiwa pia ni mara ya kwanza kwao kucheza katika uwanja huo mpya uliopo Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita, ambao Geita Gold inautumia kama uwanja wake wa nyumbani.

Geita Gold ilianza kuandika historia hiyo dakika ya 10 kupitia Richard N’gondya, kabla ya kuongeza bao la pili dakika ya 23 kupitia Obrey Chirwa kwa mkwaju wa penalti.

Yussufu Mhilu aliendelea kuipa Geita Gold nguvu kwa kufunga dakika ya 34 na 46, huku Richard N’gondya akifunga bao lake la pili katika mchezo huo dakika ya 63.

Chirwa alikamilisha siku yake nzuri kwa kufunga bao la pili dakika ya 69 na kuifanya Geita Gold kufikisha mabao sita.

Kagera Sugar ilipata mabao mawili ya kufutia machozi, yakifungwa na Hassan Mwatelema dakika ya 40 na Robert Mkandya dakika ya 90+1.

Ushindi huo unaifanya Geita Gold kuanza safari yake ya Ligi Kuu kwa kiwango cha kuvutia, huku mchezo huo ukitoa burudani kubwa kwa mashabiki waliojitokeza kushuhudia historia ya timu hizo kwenye uwanja mpya.

POLISI, YANGA, AZAM ZAVUNA ALAMA LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kwa michezo mitatu iliyochezwa katika viwanja vya Arusha na Dar es Salaam, huku Polisi Tanzania, Young Africans na Azam zikivuna ushindi.

 

Mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha uliwakutanisha Polisi Tanzania na JKT Tanzania, ambapo Polisi Tanzania iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

 

Polisi Tanzania ilianza kupata bao katika dakika ya 45+2 kupitia Kenny Ally, kabla ya Habib Kyombo kuongeza bao la pili dakika ya 65 na kuipa timu yake ushindi wa nyumbani.

 

Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam, Young Africans iliendelea na matokeo mazuri baada ya kuichapa Coastal Union mabao 4-1.

 

Albert Kangandwa aliifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 37, huku Maxi Nzengeli akiongeza la pili dakika ya 45+4.

 

Yanga iliendelea kutawala mchezo na kuongeza mabao mawili kupitia Mudathir Yahya dakika ya 49 na Mohamed Hussein dakika ya 90+5.

 

Coastal Union ilipata bao lake pekee dakika ya 77 kupitia Gradi Lassa.

 

Coastal Union ilimaliza mchezo ikiwa na wachezaji 10 baada ya Geoffrey Manyasi kuonyeshwa kadi nyekundu.

 

 

Katika mchezo wa usiku uliochezwa saa 3:00 katika Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam, Azam iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya TRA United.

 

Azam ilianza kwa kasi na kupata bao la kwanza dakika ya 8 kupitia Iddi Selemani, kabla ya Abdul Suleiman kuongeza bao la pili dakika ya 33.

 

TRA United ilipunguza pengo dakika ya 45 kupitia Ousmane Kamisoko na kufanya mchezo kuendelea kuwa na ushindani.

 

Azam ilimaliza mchezo ikiwa na changamoto baada ya mlinda mlango wake, Aishi Manula, kuonyeshwa kadi nyekundu kufuatia kufanya rafu.

 

Pamoja na kucheza pungufu, Azam iliweza kulinda uongozi wake hadi dakika ya mwisho na kuondoka na alama tatu muhimu.

MBEYA CITY, SIMBA ZAGAWA ‘DOZI’, KAGERA YABANWA NYUMBANI.

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kwa michezo mitatu iliyochezwa mkoani Mbeya, Mwanza na mkoani Kagera.

Mchezo wa kwanza uliwakutanisha mbeya city na Dodoma jiji na ‘wababe’ wa Mbeya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji kwenye uwanja wa Sokoine.

Wenyeji hao walihitaji dakika 9 pekee kuandika bao la kwanza kupitia kwa Mwani Thobias, kabla ya Yahya Mbegu kuifungia Mbeya City bao la pili dakika ya 72 na kuifanya Dodoma Jiji kuondoka Mbeya mikono mitupu.

Mchezo mwingine uliovuta hisia ulipigwa saa 10:15 jioni katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, ambapo Simba ilikuwa ugenini dhidi ya Pamba Jiji na kupata ushindi wa mabao 2-1.

Simba ilianza mchezo kwa kasi na kupata bao la kuongoza dakika ya 19 kupitia Clatous Chama, kabla ya Anicet Oura kuongeza bao la pili dakika ya 31.

Hata hivyo, mambo yalibadilika kwa Simba dakika ya 39 baada ya Ibraheem Jabaar kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kucheza vibaya na hivyo Simba kulazimika kuendelea na mchezo ikiwa na wachezaji pungufu.

Pamba Jiji ilitumia nafasi hiyo kuongeza presha na hatimaye kupata bao la kufutia machozi dakika ya 72 kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Diomande Idris.

Licha ya Pamba Jiji kusukuma mashambulizi katika kipindi cha mwisho, Simba iliweza kusimama imara na kulinda ushindi wake hadi filimbi ya mwisho

Mkoani Kagera, katika Uwanja wa Kaitaba, mchezo mwingine wa kusisimua uliwakutanisha Kagera Sugar na Singida Black Stars uliomalizika kwa sare ya 1-1.

Kagera Sugar ilianza vyema na kupata bao dakika ya 13 kupitia Kassim Feka, hali iliyowapa wenyeji matumaini ya kuondoka na alama zote.

Hata hivyo, Singida Black Stars haikukubali kushindwa na ilirejea kipindi cha pili kwa nguvu zaidi.

Juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 50 baada ya Jonathan Sowa kuisawazishia timu yake.

Bao hilo liliifanya mechi kuwa ya ushindani zaidi, huku pande zote zikisaka bao la ushindi, lakini juhudi zao hazikuzaa matunda hadi dakika za mwisho.

Kwa ujumla, michezo hiyo imeendelea kuonyesha ushindani mkubwa , huku Mbeya City ikifurahia ushindi wa nyumbani, Simba ikivuna alama ugenini licha ya kucheza pungufu, na Kagera Sugar pamoja na Singida Black Stars zikigawana alama katika Uwanja wa Kaitaba.

NAMUNGO, FOUNTAIN ZATAMBA NYUMBANI LIGI KUU YA NBC.

 

Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/27 imeendelea jana kwa mzunguko wa pili kwa kuzikutanisha timu za Fountain gate na Mashujaa mchezo wa mapema saa 10:00 alasiri mkoani Arusha,huku mchezo mwingine ukichezwa saa 1:00 usiku mkoani Lindi ukiwakutanisha Namungo na Geita Gold.

Katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Fountain Gate ilikusanya alama tatu muhimu kwa bao la Kassim Shaban dakika ya 10.

Bao hilo lilitosha kuipa Fountain Gate alama muhimu mbele ya mashabiki wake, huku Mashujaa ikishindwa kupata bao la kusawazisha hadi filimbi ya mwisho na kuondoka ugenini mikono mitupu.

Mchezo mwingine uliopigwa Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi uliwakutanisha Namungo na Geita Gold, ambapo wenyeji Namungo walitumia vyema faida ya uwanja wa nyumbani na kupata ushindi wa bao 1-0.

Hashimu Manyanya ndiye aliyekuwa shujaa wa Namungo baada ya kuifungia timu yake bao la ushindi dakika ya 25, bao lililodumu hadi mwisho wa mchezo.

Geita Gold, licha ya jitihada za kutafuta bao la kusawazisha, haikuweza kupata matokeo na hivyo kulazimika kuondoka Lindi bila alama.

Matokeo hayo yamezifanya Fountain Gate na Namungo kuanza safari kwa ushindi wa nyumbani huku Mashujaa na Geita Gold zikipoteza alama ugenini.