Author: Cynthia Michael

PAMBA JIJI YABANWA NYUMBANI LIGI KUU YA NBC.

Ligi Kuu ya NBC imeendelea kwa mchezo mmoja uliozikutanisha Pamba jiji na Fountain Gate kwenye uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza majira ya saa kumi Alasiri.

Kipindi cha kwanza kilianza kwa kasi na dakika ya 22 Mathew Momanyi wa Pamba Jiji alipatia timu yake bao la kwanza kwa mkwaju wa Penati


Dakika ya 61 kipindi cha pili Fountain Gate walifanikiwa kujipatia bao la kusawazisha lililofungwa na Elie Makono na kufanya matokeo kuwa 1-1 na dakika za nyongeza Pamba ilipata mkwaju wa penati na kukoswa na Mathew Momanyi aliyepiga na mpira kugonga mwamba hivyo kufanya mchezo kumalizika kwa matokeo ya 1-1.

Matokeo hayo yanaifanya Pamba jiji kushika nafasi ya 10 na alama 27 huku Fountain Gate ikiwa nafasi ya  8 na alama 29 kibindoni.

FOUNTAIN GATE YASHINDWA ‘KUFURUKUTA’ KWA SINGIDA LIGI KUU YA NBC.

Ligi Kuu ya NBC mzunguko 24 imeendelea huku mchezo uliochezwa mkoani Manyara kati ya Fountain Gate na Singida Black Star ukishuhudia Fountain ikishindwa kutamba na kufungwa mabao 3-0.

Dakika ya 29 zilitosha kuipa uongozi Singida Black Star  kwa bao la kwanza kupitia mchezaji wake Jonathan Sowah aliyefunga bao lake la 7 tangu kujiunga na miamba hiyo ya Singida.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo Singida Black Star waliendelea kushambulia lango la Fountain Gate na mchezaji Frank Kwabena kuongeza bao la pili dakika ya 56 na dakika ya 71 mchezaji Emmanuel Kwame aliongeza bao la tatu kwa timu yake hivyo Singida Black Star kuongoza kwa mabao matatu na Fountain kumaliza bila bao mpaka mwisho wa mchezo.

Katika mchezo huo mchezaji kiungo wa Singida Black Star Keyeheh Emmanuel alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo huku Singida ikiwa nyuma ya Azam inayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo.

 

NBC CHAMPIONSHIP YAZIDI KUNOGA

Ligi ya Championship ya NBC mzunguko wa 24 umemalizika kwa Mtibwa Sugar kuwa kinara ikiwa na alama 57 na kushika nafasi ya kwanza huku ikifunga mabao 47 na kufungwa mabao 34.

Nafasi ya pili inashikwa na Mbeya City yenye alama 52 mabao 48 huku ikifuatiwa na Stand United inayoshika nafasi ya tatu na alama 52 ikifunga mabao 40.

Geita Gold inashika nafasi ya nne ikikusanya jumla ya alama 48 baada ya kufunga mabao 41 na kufungwa 22.

Timu hizi nne zipo kwenye ushindani mkubwa wa kugombea nafasi ya kucheza Ligi Kuu ya NBC msimu ujao zikipishana kwa tofauti ya alama chache kwenye msimamo.

HAWA HAPA WABABE WA MABAO NBC CHAMPIONSHIP

LIGI ya championship ya NBC inazidi kushika kasi ikielekea ukingoni huku Mbeya City ikiwa kinara wa ‘kupachika’ mabao baada ya kufunga mabao 45 hadi sasa ikiwa ni idadi kubwa kwa timu ya Ligi hiyo hadi sasa.

Mbeya city ipo nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na alama 49 huku Mtibwa sugar ikiwa kinara kwenye msimamo na alama 54 na ikishika nafasi ya pili kwa mabao baada ya kufunga 44 na kuruhusu mabao 11 hadi sasa.

Geita gold inashika nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na alama 48 huku ikiwa timu ya tatu kwa idadi kubwa ya mabao baada ya kufunga 41 huku ikifungwa mabao 17.

Stand united ni timu ya nne kwa kupachika mabao ikiwa nayo 37 na kufungwa 19 huku ikishika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi na alama 49.