Author: Cynthia Michael

MTIBWA SUGAR ‘WABABE’ WA NYUMBANI NBC CHAMPIONSHIP

LIGI ya Championship ya NBC imeendelea kwa mzunguko wa 28 ambapo Mtibwa Sugar inaongoza kwa kushinda mechi iliyocheza nyumbani katika uwanja wa Manungu Complex ikishinda mechi zote 14, huku ikifanikiwa kupanda daraja kwenda Ligi Kuu ya NBC ikiwa  na alama 67 hadi sasa.

Geita Gold imeshinda michezo 13 iliyocheza uwanja wa nyumbani wa Nyankumbu huku timu hiyo ikishika nafasi ya nne baada ya kukusanya alama 54.

Nafasi ya tatu inashikwa na Stand United iliyoshinda michezo 12 katika uwanja wa Kambarage  uliopo mkoani Shinyanga ikishika nafasi ya tatu pamoja na kukusanya alama 59.

Mbeya City imefanikiwa kushinda michezo 10 katika uwanja wa  Sokoine mkoani Mbeya  huku ikiwa katika nafasi ya pili  kwenye msimamo wa Ligi ya NBC Championship ikikusanya alama 62 sawa na TMA iliyoshinda michezo 10 katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha.

Kwa upande wa  timu ya Bigman  iliyopo nafasi ya saba kwenye msimamo ikiwa na alama 46 ikiwa imeshinda michezo tisa katika uwanja wa Ilulu uliopo mkoani Lindi.

Mbeya Kwanza na Songea United zimefanikiwa kushinda michezo nane kila timu katika  viwanja vyao vya nyumbani ambavyo ni Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara kwa upande wa Mbeya Kwanza na Majimaji mkoani Songea kwa upande wa Songea United.

FEISAL TISHIO LIGI KUU YA NBC

KIUNGO wa Azam Feisal Salum ameendelea kuwa kinara wa kutoa Pasi za mabao katika Ligi Kuu ya NBC  akiwa na Pasi 13  katika mechi  11 alizocheza msimu huu hadi sasa.

Pacome Zouzoa wa Yanga anashika nafasi ya pili akiwa na Pasi 9 huku akifuatiwa na wachezaji  wenzake Maxi Nzengeli wa Yanga na Prince Dube wenye pasi 8 za mabao sawa na kiungo wa Singida Black Stars.

Kiungo Jean Ahoua wa Simba na Stephane Azizi Ki wa Yanga wanafuata wakiwa na Pasi 7 kila mmoja ikisalia mizunguko mitatu msimu kutamatika huku baadhi ya timu zikiwa na michezo ya ‘kiporo’.

 

SIMCHIMBA KINARA WA MABAO LIGI YA NBC CHAMPIONSHIP

Ikiwa imesalia michezo mitatu ya Ligi ya Championship ya NBC vita ya ufungaji wa mabao ikiendelea kushika kasi baada ya  mchezaji  wa Geita Gold kutoka mkoani Geita,  Andrew  Simchimba, kuongoza  akiwa ameshatupia mabao  18 katika mechi 20 ambazo amecheza akiwa na timu yake hiyo.

Nafasi ya pili ikishikiliwa na mchezaji Raizin Hafidhi wa Mtibwa Sugar  ya mkoani Morogoro akiwa amefanikiwa kufunga mabao 16, sambamba na mchezaji, Abdulaziz Shahame, wa timu ya TMA ya mkoani Arusha  akiwa na mabao 16

Nafasi ya nne ikichukuliwa na mchezaji  Ambokile Eliud wa Mbeya City  ya mkoani Mbeya akiwa na mabao 9 huku Mwani Ally wa timu hiyo pia akiwa na mabao 9 yanayomfanya kuwa nafasi ya tano.

Mzunguko wa 28  wa Ligi ya NBC Championship utaendelea kesho ambapo mechi zote nane za mzunguko huo zitachezwa majira ya saa kumi jioni.

COASTAL UNION YATAMBA MKWAKWANI.

Ligi Kuu ya NBC ilitimua vumbi tena kwenye uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga majira saa moja jioni ambapo ulizikutanisha timu ya Coastal union na Kengold na Coastal kushinda 2-1.

Timu zote zilikuwa na shauku ya kupata alama tatu muhimu na hasa Kengold ambayo ipo nafasi ya mwisho katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC na ushindi pekee ungeweka  matumaini yao ya kusalia ligi kuu.

Dakika ya 20 Bakari Msimu wa Coastal Union aliipatia bao la kwanza timu yake na kuamsha mashabiki kwa shangwe na dakika ya 37 mchezaji Amara Bagayoko alipigilia msumari wa pili na kuzima matumaini ya KenGold kusalia ligi kuu.

Dakika ya 39 zikiwa zimesalia dakika 6 kipindi cha kwanza kutamatika Kengold  ilipata bao pekee lililofungwa na Sadalah Lipangile hivyo mchezo kumalizika 2-1.

Ushindi huo umeiweka Coastal union nafasi ya 8 na alama 31 huku Kengold ikiwa nafasi ya 16 ambayo ni ya mwisho ikiwa na alama 16 na kushuka daraja rasmi.

NAMUNGO,JKT TANZANIA HAKUNA MBABE

LIGI Kuu ya NBC imeendelea ambapo JKT Tanzania waliikaribisha Namungo uwanja wa Isamuhyo mchezo uliochezwa saa nane mchana na kumalizika kwa sare ya 2-2.

Mchezo ulianza kwa kasi ambapo  Namungo walishambulia lango la JKT na dakika ya 18 Saleh Karabaka aliipatia timu yake bao la kwanza kabla ya dakika ya 49 Fabrice Ngoy kuongeza bao la pili.

Kipindi cha pili JKT Tanzania walirudi kwa kasi baada ya kutambua makosa yao na dakika ya 63  Maka Edward akaipatia JKT bao la kwanza na dakika ya 69 wakaongeza bao la pili lililofungwa na  Shiza Kichuya.

Katika mchezo huo mchezaji bora alikuwa  Shiza Kichuya wa JKT Tanzania aliyetengeneza bao la kwanza kwa mpira wa kona huku akifunga bao la kusawazisha kwa timu yake.

Kwa matokeo hayo JKT inafikisha alama 32 na kushika nafasi ya saba huku Namungo ikishika nafasi ya 11 baada ya kukusanya jumla ya alama 28.