TIMU ya Coastal union imeshindwa kupata ushindi nyumbani kwenye mchezo wa pili mfululizo baada ya kulazimishwa sare ya bao moja na TRA kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC katika uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Coastal union ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 35 kupitia kwa Shiza Kichuya aliyesajiliwa kwenye dirisha dogo la usajili na kuipeleka Coastal mapumziko ikiwa kifua mbele.
Kipindi cha pili kilianza kwa TRA United kuonyesha nia ya kusawazisha mapema na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 48 kupitia kwa Denis Nkane alipofunga bao la kusawazisha.
Licha ya timu zote kutengeneza nafasi kadhaa katika dakika za mwisho hakuna aliyeweza kuongeza bao jingine na hivyo mchezo kumalizika kwa timu hizo kugawana alama.
Matokeo haya yameifanya kila timu kuongeza alama kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC, TRA ikiwa nafasi ya 8 na alama 13 na Coastal Union nafasi ya 11 na alama 11 kwenye msimamo wa ligi hiyo.