Author: Cynthia Michael

SIKU NYINGINE YA KUSAKA ALAMA TATU ZA LIGI KUU YA NBC.

 

Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/27 inaendelea leo, Agosti 18, kwa michezo miwili inayotarajiwa kutoa ushindani mkubwa katika mzunguko wa pili wa ligi.

Huko Arusha, Fountain Gate itakuwa mwenyeji wa Mashujaa katika mchezo utakaopigwa saa 10:00 alasiri kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa wa ushindani kutokana na timu zote kutafuta matokeo muhimu mapema katika msimu.

Fountain Gate itakuwa na jukumu la kutumia vizuri faida ya kucheza nyumbani, huku Mashujaa ikilenga kuondoka na matokeo mazuri katika safari yake jijini Arusha.

Kwa mujibu wa ratiba rasmi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, mchezo huo ni sehemu ya michezo ya wiki ya pili ya Ligi Kuu ya NBC

Wakati huo huo, huko Lindi, Namungo itakuwa mwenyeji wa Geita Gold katika mchezo utakaopigwa saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Majaliwa.

Namungo itaingia uwanjani ikitafuta kutumia vyema uwanja wake wa nyumbani, wakati Geita Gold, ambayo ilianza msimu kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Mbeya City itajaribu kuendeleza mwanzo wake mzuri wa msimu.

Mchezo wa Lindi unatarajiwa kuwa na mvuto kutokana na umuhimu wa kila timu kupata alama katika hatua hii ya mwanzo ya msimu.

Kwa Namungo, ushindi mbele ya mashabiki wake unaweza kuwa kichocheo muhimu, huku Geita Gold ikitafuta matokeo yatakayoiweka katika mwendelezo mzuri.

Kwa ujumla, michezo yote miwili ya leo ina umuhimu mkubwa katika kujenga mwelekeo wa timu hizo katika msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC, huku kila upande ukisaka alama tatu muhimu

TPLB YAKUTANISHA MAAFISA HABARI KUELEKEA MSIMU WA 2026/27.

 

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) leo imefanya semina ya kuwajengea uwezo maafisa habari wa klabu za Ligi Kuu ya NBC na Championship katika Ukumbi wa NSSF Mafao House, Ilala jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano nchini.

Akifungua semina hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Cornel Barnabas, aliwashukuru maafisa habari kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya soka nchini, akisisitiza kuwa wao ni kiungo muhimu kati ya klabu, mashabiki na wadau mbalimbali wa mchezo huo.

Barnabas alisema maafisa habari wana jukumu la kuhakikisha taarifa za Ligi Kuu ya NBC na Ligi ya Championship ya NBC zinawafikia wadau kwa usahihi na kwa wakati, hatua inayochangia kujenga uelewa wa pamoja, kuimarisha taswira ya ligi na kukuza mchezo wa mpira wa miguu nchini.

“Semina hii ni fursa ya kujengana kitaaluma, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano ili tuendelee kuzifanya ligi zetu kuwa bora zaidi. Ni muhimu kuzingatia misingi na maadili ya uandishi wa habari pamoja na kuhakikisha taarifa zinazotolewa ni sahihi na zenye kuwajengea imani wadau wetu,”

Katika semina hiyo, Afisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, aliwasilisha mada kuhusu nafasi na majukumu ya vyombo vya habari akieleza umuhimu wa mawasiliano ya kitaalamu katika kukuza soka na kujenga uhusiano mzuri kati ya klabu, wadau na mashabiki.

Naye Meneja wa Chapa, Matukio na Udhamini wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Janeth Mbelwa aliwasilisha mada kuhusu usimamizi wa chapa, matukio na udhamini katika michezo.

Aliwataka maafisa habari kutambua nafasi yao katika kuongeza thamani ya ligi na wadhamini kupitia utoaji wa taarifa sahihi, maudhui yenye ubora na ushirikiano unaoimarisha taswira ya mashindano na washirika wa kibiashara.

Afisa habari wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Prudence Constantine, aliwasilisha mada kuhusu maadili ya taaluma ya uandishi wa habari, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia weledi, uwajibikaji na viwango vya taaluma katika utoaji wa habari.

Aidha, wataalamu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) waliwasilisha mada kuhusu mapambano dhidi ya rushwa katika michezo, wakieleza athari za vitendo vya rushwa kwa maendeleo ya soka na umuhimu wa kila mdau kushiriki katika kulinda misingi ya haki, uwazi na uadilifu katika mashindano.

Semina hiyo ililenga kuwajengea uwezo maafisa habari, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano kuelekea msimu mpya wa mashindano, huku TPLB ikiendelea kusisitiza utoaji wa taarifa sahihi, zenye weledi na zinazochangia maendeleo ya soka nchini.

BODI YA LIGI KUU TANZANIA YAJENGEA UWEZO WAANDISHI KUELEKEA MSIMU WA 2026/27.

 

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeendesha semina ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari za michezo katika Ukumbi wa NSSF Mafao House, Ilala, Agosti 3, 2026, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC 2026/27.

Akifungua semina hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, Nassor Idrissa, aliwataka waandishi kuendelea kuutumikia mpira wa Tanzania kwa uandishi wa kitaalamu, ukosoaji wenye kujenga na utoaji wa taarifa sahihi zitakazochangia maendeleo ya soka nchini.

Nassor alisema maendeleo ya mpira wa miguu nchini yanahitaji ushirikiano wa wadau wote, akibainisha kuwa waandishi wa habari wamekuwa na mchango mkubwa katika kuufikisha mchezo huo kwenye kiwango cha sasa. Alisisitiza kuwa kadri ushindani wa ligi unavyozidi kuongezeka, ndivyo mafanikio na changamoto zinavyoongezeka, hivyo jukumu la waandishi ni kuhabarisha, kuibua changamoto na kukosoa kwa lengo la kujenga, badala ya kubomoa juhudi zinazofanywa kuendeleza soka.

“Mpira wetu ni wa Watanzania wote, si wa mtu mmoja. Ninyi mna nafasi kubwa ya kuutangaza, kuuelimisha umma na kuusaidia kukua kupitia taarifa sahihi na zenye kujenga. Tupiganie pamoja kuufikisha mpira wetu katika viwango vya juu zaidi.” alisema Nassor.

Washiriki walipata mafunzo kutoka kwa Mkurugenzi wa Sheria na Habari na Masoko wa TFF Boniface Wambura, aliyewasilisha mada kuhusu Uandishi wa Habari za Mpira wa Miguu (Football Reporting), akisisitiza maadili ya taaluma, usahihi wa taarifa na wajibu wa waandishi katika kukuza mchezo wa soka kupitia uandishi wa kitaalamu.

Aidha, Afisa kutoka TAKUKURU aliwasilisha mada kuhusu uadilifu katika michezo na umuhimu wa kupambana na vitendo vya rushwa, huku wataalamu kutoka JAB wakielezea taratibu za ithibati (accreditation), matumizi sahihi ya vitambulisho vya waandishi wa habari na wajibu wa wanahabari wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Akifunga mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, Cornel Barnabas, aliwasisitiza waandishi kuhakikisha wanazihakiki taarifa kabla ya kuzichapisha na kuendelea kushirikiana na Bodi ya Ligi katika kuifikisha kwa umma taarifa sahihi na zenye kujenga.

“Ninyi ni sehemu muhimu ya maendeleo ya mpira wetu. Kadiri mnavyotoa taarifa sahihi na zenye kujenga, ndivyo mnavyochangia kukuza soka la Tanzania na kulifikisha katika kiwango cha kimataifa,” alisema Barnabas.

Semina hiyo ililenga kuongeza uwezo wa waandishi wa habari ili waendelee kuripoti kwa weledi, kuzingatia maadili ya taaluma na kuchangia maendeleo ya soka la Tanzania.

YOUNG AFRICANS ‘MBABE’ WA LIGI KUU YA NBC MSIMU WA 2025/26.

 

TIMU ya Young Africans wamehitimisha kwa mafanikio makubwa msimu wa Ligi Kuu ya NBC 2025/26 kwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Tanzania katika moja ya mchezo wa mwisho wa msimu uliochezwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na kukabidhiwa rasmi taji la ubingwa.

Prince Dube, Max Nzengeli na Laurindo Dilson ‘Depu’ walifunga mabao yaliyoipa Yanga ushindi huo na kuhitimisha msimu kwa kiwango cha juu mbele ya mashabiki wao.

Baada ya kutwaa ubingwa wa msimu wa 2025/26 timu ya Young Africans imeandika rekodi ya kutwaa taji la Ligi Kuu ya NBC kwa mara ya tano mfululizo na kuendeleza ubabe wao katika soka la Tanzania Bara.

Katika michezo mingine ya mwisho timu ya Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC kupitia kwa Inno Loemba huku Azam ikiifunga Dodoma Jiji mabao 2-0 yaliyofungwa na Jean Ngita na Nathaniel Chilambo.

Coastal Union iliishinda Pamba Jiji kwa mabao 2-1, Namungo ikaichapa Mtibwa Sugar mabao 2-1 na kuishusha timu hiyo daraja hivyo ‘wakata miwa’ hao watakuwa sehemu ya NBC Championship msimu ujao.

Tanzania Prisons ikaibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa, Mbeya City na TRA United zikitoka suluhu.

Mchezo uliokuwa na mabao mengi zaidi uliwakutanisha Fountain Gate na Singida Black Stars ambapo Fountain Gate iliibuka na ushindi wa mabao 4-3.

Ndumumwe Mossi aling’ara kwa kufunga mabao matatu (hat-trick) akifanya hivyo kwa mara ya pili msimu huu, Obina Awara akiongeza bao moja kwa Singida Black Stars huku Chukwunonye Macdonald akifunga bao moja na Hashim Kindemile akifunga mawili.

Kumalizika kwa michezo hiyo kumeshusha pazia rasmi la msimu wa Ligi Kuu ya NBC 2025/26, ulioshuhudia ushindani mkubwa kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Sherehe za kukabidhiwa taji kwa Young Africans zimekuwa hitimisho la msimu mwingine wenye mafanikio makubwa huku mabingwa hao wakithibitisha ubora wao kwa kutwaa ubingwa wa ligi kwa mara ya tano mfululizo.

PAZIA LA LIGI KUU YA NBC 2025/26 KUFUNGWA LEO.

Baada ya miezi kadhaa ya ushindani wa hali ya juu leo Juni 30, 2026, msimu wa Ligi Kuu ya NBC 2025/26 unafikia tamati rasmi kwa kuchezwa kwa michezo yote ya mwisho ya ligi.

 

Mechi zote zitapigwa kwa wakati mmoja kuanzia saa 10:00 alasiri, hatua inayotarajiwa kuleta msisimko mkubwa kwa mashabiki wa soka nchini.

 

Katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam timu ya JKT Tanzania watawakaribisha mabingwa wa msimu uliopita Young Africans.

 

Wakati huo huo uwanja wa KMC Complex kutakuwa na mchezo kati ya Simba na KMC ,huku Azam Complex ikipeperusha bendera ya mchezo kati ya Azam na Dodoma Jiji.

 

Mkoani Tanga, Uwanja wa Mkwakwani utashuhudia Coastal Union wakivaana na Pamba Jiji, huku Sheikh Amri Abeid Stadium mjini Arusha ukiwa mwenyeji wa pambano la Fountain Gate dhidi ya Singida Black Stars.

 

Katika Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya, Mbeya City watachuana na TRA United, wakati uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma utakuwa uwanja wa Mashujaa dhidi ya Tanzania Prisons.

 

Nako mkoani Lindi,uwanja wa Majaliwa utahitimisha msimu kwa mchezo kati ya Namungo na Mtibwa Sugar.

 

Michezo ya leo si ya kukamilisha ratiba pekee, bali ni ya kufunga rasmi pazia la msimu ulioshuhudia ushindani mkubwa, rekodi mbalimbali na burudani ya kipekee.

 

Mara baada ya filimbi za mwisho, sherehe za kukabidhi taji la ubingwa wa NBC 2025/26 zitafanyika, zikihitimisha safari ya msimu mmoja uliobeba hisia, mapambano na historia.

 

Leo ndiyo mwisho wa safari ya Ligi Kuu ya NBC 2025/26, lakini pia ni siku ambayo historia mpya itaandikwa kwa mabingwa wa Tanzania kupatikana.