Author: Cynthia Michael

NADO, FEISAL VINARA WA KUTUMIA ‘GUU’ LA KULIA.

 

WACHEZAJI wa timu ya Azam, Iddi Selemani na Feisal Salum, wanashikilia usukani kwenye orodha ya wachezaji waliofunga mabao mengi kwa kutumia mguu wa kulia katika Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026 hadi sasa baada ya kila mmoja kufunga mabao nane.

Nyota hao wa Azam wamekuwa na mchango mkubwa katika safu ya ushambuliaji ya timu yao, wakionyesha umakini mkubwa mbele ya lango na uwezo wa kutumia mguu wao wa kulia kuipa timu yao alama muhimu katika mechi mbalimbali za ligi.

Nyuma yao kuna Ndumumwe Mossi wa Singida Black Stars pamoja na wachezaji wa Young Africans, Mudathir Yahya na Pacome Zouzoua ambao wote wamefunga mabao saba kwa mguu wa kulia.

Orodha hiyo pia inamjumuisha mshambuliaji wa Coastal union, Maabad Maabad ambaye ameweka kambani mabao saba kwa kutumia mguu wa kulia huku akithibitisha kuwa ni mmoja wa washambuliaji hatari wa kuchungwa katika ligi msimu huu.

Takwimu hizi zinaonyesha ushindani mkubwa uliopo miongoni mwa wafungaji wa Ligi Kuu ya NBC, huku vita ya kuwania tuzo mbalimbali za ufungaji ikiendelea kushika kasi kadri msimu unavyoelekea ukingoni.

‘FEITOTO’ KINARA WA MABAO YA ‘UTOSI’ LIGI KUU YA NBC.

LICHA ya kujulikana zaidi kwa uwezo wao wa kucheza mpira wa chini na kutengeneza nafasi za kufunga, baadhi ya nyota wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026 wameonyesha ubora mkubwa wa kufunga mabao kwa kichwa.

Kiungo mshambuliaji wa Azam na raia wa Tanzania Feisal Salum (Feitoto), ndiye kinara wa orodha hiyo akiwa amefunga mabao manne 4 ya kichwa hadi sasa.

Feisal ameendelea kuwa silaha muhimu kwa Azam , akitumia vizuri mipira ya krosi na mipira ya adhabu kuisaidia timu yake kupata matokeo muhimu.

Nafasi ya pili inashikiliwa na mshambuliaji wa TRA United United, Mapaka Beatus aliyefunga mabao matatu 3 kwa kichwa.

Uwezo wake wa kuruka na kutumia nguvu za mwili umemfanya kuwa tishio kubwa kwa mabeki wa timu pinzani na kuisaidia TRA kupata matokeo mazuri hivi karibuni.

Mshambuliaji wa Tanzania Prisons Oscar Mwaijanga, anashika nafasi ya tatu akiendelea kuonyesha uwezo mkubwa wa kumalizia mashambulizi ndani ya eneo la hatari hasa kupitia mipira ya juu.

Nafasi ya nne inashikiliwa na Paul Peter wa JKT ambaye pia amefunga mabao matatu 3 ya kichwa.

Mchango wake umekuwa muhimu kwa JKT katika harakati za kutafuta matokeo mazuri msimu huu.

Hii inaonyesha kuwa mabao ya kichwa yameendelea kuwa sehemu muhimu ya ushambuliaji katika Ligi Kuu ya NBC msimu huu huku ‘Fei’ akiongoza orodha ya wachezaji waliotumia vyema mipira ya juu kuwatesa walinzi na makipa wa timu pinzani.

‘WAZEE’ WA ‘MAKOMBORA’ YA LIGI KUU YA NBC.

Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026 imeendelea kushuhudia mabao ya kuvutia kutoka nje ya eneo la hatari, huku baadhi ya nyota wakionyesha uwezo mkubwa wa kupiga mashuti sahihi yanayowapa mashabiki burudani ya kipekee.

Kinara wa orodha hiyo ni mshambuliaji wa Azam Idd Seleman ambaye hadi sasa ameweka kambani mabao matano akifunga kutoka nje ya eneo la 18 ambapo wezo wake wa kupiga mashuti ya kushtukiza umekuwa silaha muhimu kwa Azam katika harakati za kutafuta mafanikio msimu huu.

Nafasi ya pili inashikiliwa na kiungo mshambuliaji wa Simba Clatous Chama aliyefunga mabao manne kutoka nje ya eneo la 18.

Chama ameendelea kuthibitisha ubora wake wa muda mrefu kwa kutengeneza nafasi na kufunga mabao muhimu katika nyakati ngumu za mchezo zinazowafanya Simba kuendelea kusalia kwenye mbio za ubingwa.

Katika nafasi ya tatu ni nyota wa Mtibwa Sugar Ismail Mhesa, mwenye mabao matatu ya nje ya boksi likiwemo lile alilofunga kwa mpira wa kona ulioingia moja kwa moja dhidi ya Young Africans.

Beki wa Singida Black Stars, Ibrahim Imoro ambaye licha ya kucheza nafasi ya ulinzi amekuwa tishio kubwa kupitia mashuti yake ya mbali na mipira ya adhabu nae amefunga matatu sawa na Mhesa.

Kadri msimu unavyoelekea ukingoni mashabiki wataendelea kutarajia kuona mabao mengi zaidi ya kuvutia kutoka kwa nyota hawa wenye uwezo wa kubadili matokeo ya mchezo kwa shuti moja tu lililo sahihi.

OKELLO KINARA WA MABAO YA MGUU WA KUSHOTO LIGI KUU YA NBC.

 

MSHAMBULIAJI wa Young Africans raia wa Uganda Allan Okello ameendelea kuonyesha ubora wake katika Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26 baada ya kuongoza kwenye orodha ya wachezaji waliofunga mabao mengi kwa kutumia mguu wa kushoto.

Nyota huyo anaongoza kwa mabao 10 ya mguu wa kushoto akithibitisha uwezo wake mkubwa wa kumalizia mashambulizi na kuwa silaha muhimu kwa Young Africans katika harakati za kutetea ubingwa wao.

Nyuma yake wapo nyota wawili waliolingana kwa mabao sita kila mmoja ambao ni Libasse Guèye wa Simba na Salehe Karabaka wa JKT waliotoa mchango mkubwa katika safu za ushambuliaji za timu zao.

Katika nafasi ya nne ni Fredrick Magata wa Mtibwa Sugar mwenye mabao matano ya mguu wa kushoto huku Methew Tegisi wa Pamba Jiji akifuatia kwa mabao manne.

Wachezaji wengine waliopo kwenye orodha hiyo ni Selemani Mwalimu, Clatous Chama wa Simba na Prince Dube wa Young africans waliofunga mabao manne kwa kutumia mguu wao wa kushoto kila mmoja.

Hii inaonyesha umuhimu wa wachezaji wenye uwezo wa kutumia mguu wa kushoto kwa ufanisi huku Allan Okello akiendelea kuwa kinara na mmoja wa wachezaji wenye mchango mkubwa zaidi kwa ‘wananchi’ katika mashindano ya Ligi Kuu ya NBC.

‘WALINDA LANGO’ LA AZAM NI MOTO WA KUOTEA MBALI LIGI KUU YA NBC.

Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026 imeendelea kushuhudia ushindani mkubwa si tu katika ufungaji wa mabao, bali pia katika uimara wa safu za ulinzi huku takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa Azam ndiyo timu iliyocheza michezo mingi zaidi bila kuruhusu bao, ikifanikiwa kutofungwa katika michezo 20 hadi sasa.

Azam imeonyesha nidhamu kubwa langoni chini ya magolikipa wao Aishi Manula aliyecheza michezo 11 bila kuruhusu bao, Zuberi Foba aliyecheza michezo nane bila kuruhusu na Issa Fofana aliyefanya hivyo kwenye mchezo mmoja.

Mabingwa watetezi Young Africans wanafuatia kwa kutofungwa bao katika michezo 19 wakionyesha uimara mkubwa wa walinda mlango wao chini ya Djigui Diarra, Hussein Masalanga na Abutwalib Mshery.

Simba wanashika nafasi ya tatu kwa michezo 17 ya kutofungwa bao, huku Mashujaa wakishika nafasi ya nne kwa michezo 12, Dodoma Jiji wakikusanya michezo 11 ya kutofungwa bao na kujikita miongoni mwa timu zenye safu bora za golikipa msimu huu.

JKT Tanzania, TRA na Pamba Jiji zote zimefanikiwa kutofungwa bao katika michezo 10 kila moja, zikithibitisha uimara wao wa kujilinda dhidi ya mashambulizi ya wapinzani.

Orodha hii inaonyesha wazi kuwa mafanikio ya timu nyingi msimu huu hayajatokana na ushambuliaji pekee, bali pia uimara wa walinda mlango na mabeki ambao wamekuwa nguzo muhimu katika kupambania matokeo chanya ndani ya Ligi Kuu ya NBC.