Author: Cynthia Michael

DODOMA YAPANDA NAFASI YA SITA LIGI KUU YA NBC.

 

DODOMA Jiji imeendelea kuonyesha makali yake kwenye Ligi Kuu ya NBC baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2–1 dhidi ya KMC katika mchezo uliochezwa Jijini Dodoma kwenye uwanja wa Jamhuri.

Bao la kwanza la Dodoma Jiji lilifungwa dakika ya 43 na Faraji Kayanda na Kipindi cha kwanza kumalizika Dodoma ikiwa mbele kwa bao moja.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku KMC ikijaribu kusawazisha na jitihada zao zilifanikiwa dakika ya 76 baada ya Rashid Chambo kufunga bao la kusawazisha na kuirejesha timu yake mchezoni.

Hata hivyo iliwachukua dakika moja pekee Dodoma kurejea kwenye uongozi kwa bao la Iddi Kipangwile na kufanya mabao kuwa 2–1 hadi mchezo unamalizika.

Katika mchezo huo, Khleffin Hamdoun alionyesha kiwango cha juu na hatimaye kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi akichangia kwa kiasi kikubwa ushindi wa Dodoma Jiji.

Ushindi huo unaifanya Dodoma Jiji kufikisha alama 17 na kuendelea kushika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi huku KMC ikisalia nafasi ya mwisho (16) ikiwa na alama 8 hali inayozidi kuwaweka kwenye presha ya kusaka matokeo chanya katika michezo ijayo ili kusalia Ligi Kuu ya NBC.

MTIBWA HAIKAMATIKI,JKT YAREJEA KILELENI LIGI KUU YA NBC.

 

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kwa michezo miwili iliyochezwa mkoani Dodoma kwenye uwanja wa Jamhuri na jiji Dar es saalam katika uwanja wa Mej. Jen Isamuhyo.

Mchezo wa Kwanza uliopigwa saa kumi alasiri kati ya Mtibwa Sugar na Tanzania Prisons na kushuhudia Mtibwa sugar ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons.

Tanzania Prisons walitangulia kupata bao la mapema dakika ya nane kupitia kwa George Mpole akitumia mkwaju wa penati na Mtibwa sugar ilijibu mapigo kwa kusawazisha dakika ya 38 kupitia Magata Fredrick naye kwa mkwaju wa penati na dakika ya 87 Ismail Mhesa aliipatia Mtibwa bao la ushindi na kuwahakikishia alama tatu muhimu nyumbani.

Katika mchezo mwingine uliochezwa saa moja jioni maafande wa JKT Tanzania waliibuka na ushindi mnono wa Mabao 3-0 dhidi ya Pamba jiji ya Mwanza.

JKT walifungua ukurasa wa mabao dakika ya 34 kupitia kwa Valentino Mashaka bao lililowapa morali na kuwadhibiti Pamba jiji waliojaribu kujibu mashambulizi lakini walishindwa kusawazisha hadi kipindi cha kwanza kinatamatika.

Kipindi cha pili Salehe Karabaka aliendelea kuzamisha jahazi la Pamba jiji baada ya kufunga bao la pili dakika ya 55 na dakika ya 70 Valentino Mashaka aliyewapatia bao la tatu na kuihakikishia ushindi JKT.

Matokeo ya michezo hii yanaendelea kuongeza moto wa ushindani kwenye Ligi Kuu ya NBC huku JKT Tanzania wakiwa kileleni kwa alama 24 na Mtibwa Sugar ikishika nafasi ya tatu baada ya kukusanya alama 20.

COASTAL, TRA HAKUNA MBABE MKWAKWANI.

 

TIMU ya Coastal union imeshindwa kupata ushindi nyumbani kwenye mchezo wa pili mfululizo baada ya kulazimishwa sare ya bao moja na TRA kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC katika uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Coastal union ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 35 kupitia kwa Shiza Kichuya aliyesajiliwa kwenye dirisha dogo la usajili na kuipeleka Coastal mapumziko ikiwa kifua mbele.

Kipindi cha pili kilianza kwa TRA United kuonyesha nia ya kusawazisha mapema na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 48 kupitia kwa Denis Nkane alipofunga bao la kusawazisha.

Licha ya timu zote kutengeneza nafasi kadhaa katika dakika za mwisho hakuna aliyeweza kuongeza bao jingine na hivyo mchezo kumalizika kwa timu hizo kugawana alama.

Matokeo haya yameifanya kila timu kuongeza alama kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC, TRA ikiwa nafasi ya 8 na alama 13 na Coastal Union nafasi ya 11 na alama 11 kwenye msimamo wa ligi hiyo.

AZAM HAIJAPOTEZA MCHEZO KWENYE LIGI KUU YA NBC.

LIGI kuu ya NBC imeendelea kwa timu ya Azam kuwakaribisha TRA United katika dimba la Azam Complex kwenye pambano lililokuwa na ushindani mkubwa na Azam ikiibuka mbabe kwa kushinda mabao 2-0.

Azam wakicheza nyumbani walianza mchezo kwa kasi wakitawala umiliki wa mpira na kutengeneza nafasi zilizozaa matunda baada ya Jean Ngite kufunga bao la kuongoza dakika ya 28.

Kipindi cha pili dakika ya 70 Iddi Nado aliongeza bao la pili na kuwaamsha mashabiki wa Azam waliofurahia timu yao kuongeza bao na kumaliza na ushindi hivyo kusogea hadi nafasi ya tano ikifikisha alama 16.

Kwa matokeo hayo timu ya TRA United inashika nafasi ya 9 ikiwa na alama 12 katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC huku mchezo unaofuata itakuwa mgeni wa timu ya Coastal Union iliyopata sare katika mchezo uliopita nyumbani dhidi ya KMC inayoshika mkia kwenye msimamo.

MTIBWA YAENDELEZA MOTO LIGI KUU YA NBC

TIMU ya Mtibwa Sugar imefanikiwa kuondoka na alama tatu muhimu baada ya kuifunga Pamba Jiji bao moja katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliochewa katika dimba la Jamhuri mkoani Dodoma.

Mchezo huo uliokuwa mkali tangu mwanzo ulishuhudia timu zote zikicheza kwa tahadhari kubwa huku kila moja ikilenga kutumia vizuri nafasi zilizojitokeza ingawa wababe hao walienda mapumziko bila bao kupatikana.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kutengeneza nafasi na dakika ya 90+3 Twalib Hassan aliibuka shujaa wa Mtibwa Sugar baada ya kufunga bao la ushindi akitumia vyema nafasi ya mwisho na kuamsha shangwe kubwa kwa benchi la ufundi na mashabiki wa timu hiyo.

Bao hilo lilitosha kukusanya alama tatu kwa ‘wakata miwa’ huku Pamba Jiji ikilazimika kuondoka mikono mitupu licha ya kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo.

James Mwashinga wa Pamba aliibuka mchezaji bora wa mchezo huo licha ya timu yake kupoteza dakika za mwisho.

Mchezo wa mapema ulishuhudia ‘maafande’ wa Tanzania Prisons na JKT Tanzania wakigawana alama baada kutoka suluhu kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.