Author: Cynthia Michael

LIGI KUU YA NBC KUPAMBA MOTO LEO.

 

LIGI Kuu ya NBC itaendelea leo kwa michezo minne muhimu itakayochezwa ikiwa ni muendelezo wa mzunguko wa 23 katika viwanja tofauti huku kila timu ikisaka alama muhimu kuelekea mwisho wa msimu.

Timu za juu zinapigania ubingwa huku zile za chini zikihangaika kujinasua kwenye hatari ya kushuka daraja na kucheza Ligi ya Championship ya NBC.

Mchezo wa kwanza utawakutanisha Mtibwa Sugar dhidi ya KMC katika uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro Majira ya saa nane mchana ambapo Mtibwa Sugar wanaingia wakiwa nafasi ya 11 kwenye msimamo huku KMC wakiwa nafasi ya mwisho.

Katika mchezo mwingine Tanzania Prisons watawakaribisha Fountai Gate kwenye uwanja wa Sokoine Mkoani Mbeya majira ya saa nane mchana katika pambano litakalokuwa na ushindani mkubwa.

Tanzania Prisons wanashika nafasi ya 15 huku Fountain Gate wakiwa nafasi ya 10 na alama 25 wakisaka kuendelea kubaki kwenye nafasi za juu za msimamo ili kuepuka kushuka daraja.

Mashujaa watakuwa na kazi ngumu dhidi ya timu ya Simba inayosaka taji la Ligi Kuu ya NBC baada ya misimu minne huku Mashujaa ikiwa nafasi ya tisa kwenye msimamo ikipambana kujihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu ujao.

Mchezo huo utachezwa Uwanja wa Lake Tanganyika Mkoani Kigoma majira ya saa 10 :15 jioni na unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na ubora wa timu zote mbili msimu huu.

Katika mchezo mwingine wa kusisimua Azam FC watachuana na Pamba Jiji Katika uwanja wa Azam complex jijini Dar es salaam majira ya saa 12:30 jioni.

Azam wanaingia wakiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo huku Pamba Jiji wakiwa nafasi ya saba, kila mmoja akihitaji ushindi ili kutimiza malengo yake msimu huu.

SINGIDA, FOUNTAIN, AZAM ZATAMBA LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kwa michezo iliyochezwa katika mikoa ya Arusha,Singida na Dar es salaam.

Katika dimba la Singida, timu ya Singida Black Stars waliwakaribisha Pamba Jiji katika mchezo uliokuwa na kasi na ushindani mkubwa ulioshuhudia wenyeji wakionyesha ubora wao kwa kupata ushindi wa 3-1.

Mabao mawili yaliwekwa kambani na Ndumumwe Mossi aliyefunga dakika ya 21 na kuongeza lingine dakika ya 53 huku Horso Malanga akijiunga kwenye orodha ya wafungaji kwa bao la dakika ya 70 na kuhakikisha Singida wanakusanya alama zote tatu.
Bao pekee la Pamba Jiji lilifungwa na Henry Lutonja dakika ya 90 ingawa haikutosha kuzuia ushindi wa Singida.

Wakati huo huo, katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Fountain Gate walikuwa na kibarua kigumu dhidi ya Coastal Union walioanza mchezo kwa kasi wakiandika bao la mapema dakika ya 2 kupitia kwa Shiza Kichuya.

Hata hivyo, Fountain Gate walirudi na kusawazisha kupitia Chukwunonye Obasi dakika ya 14 kabla ya kuongeza la pili dakika ya 33 huku Henry David akifunga bao la tatu dakika ya 70 na kufanya matumaini ya ushindi kuwa makubwa kwa wenyeji.

Coastal Union hawakukata tamaa, wakipata bao la pili dakika za nyongeza (90+3) kupitia Meshack Mwamita, lakini juhudi zao hazikutosha kubadili ubao wa matokeo.

Katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Azam FC walikuwa wenyeji wa Namungo katika mchezo uliokuwa wa ushindani mkubwa huku timu zote zikionesha nidhamu ya hali ya juu.

Azam walifanikiwa kupata bao pekee la mchezo dakika ya 41 kwa njia ya penalti iliyofungwa kwa utulivu na Feisal Salum aliandika bao lake la kumi msimu huu lililodumu hadi mwisho na kuwapatia ushindi muhimu.

Kwa ujumla, michezo hiyo imeendelea kuonyesha ushindani mkubwa ndani ya ligi, huku timu zikionyesha nia ya kupambana hadi dakika ya mwisho kusaka alama tatu muhimu.

HAKUNA MBABE WA KARIAKOO MSIMU WA 2025/26.

 

LIGI Kuu ya NBC iliendelea jana kwa mchezo wa ‘Derby’ ya Kariakoo kati ya Simba na Yanga iliyochezwa Mej. Jenerali isamuhyo na kumalizika kwa sare ya kusisimua ya mabao 2-2, katika pambano lililovuta hisia za mashabiki wengi.

Simba walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Libasse Gueye dakika ya tatu kwa pasi safi ya Clatous Chama ambaye dakika saba baadae aliiandikia Simba ‘chuma’ ya pili baada ya kupokea pasi kutoka kwa Elie Mpanzu.

Dakika ya 17 Prince Dube alirudisha matumaini kwa Yanga na kufanya mchezo huo kwenda mapumziko Simba ikiongoza 2-1.

Dakika tano baada ya kipindi cha pili kuanza nahodha wa Yanga Bakari Mwamnyeto alisawazisha na kurejesha matumaini ya wananchi.

Mchezo huo uliendelea kwa kasi kubwa huku kila timu ikitafuta bao la ushindi, lakini uimara wa safu za ulinzi na makipa ulihakikisha matokeo yanabaki kuwa sare ya 2-2.

hii imeendelea kuthibitisha ushindani mkubwa uliopo kwenye Kariakoo Derby huku kila upande ukionyesha ubora na mapambano makali hadi dakika ya mwisho.

Mchezaji wa Simba Claotus Chama alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kufunga bao moja na kutoa pasi moja ya bao.

CHIRWA KINARA WA MABAO NBC CHAMPIONSHIP. 

 

 

LIGI ya Championship ya NBC msimu wa 2025/26 inaendelea kushika kasi huku vita ya ufungaji ikizidi kupamba moto huku wachezaji mbalimbali wakionyesha uwezo wao wa kutikisa nyavu.

Kinara wa orodha hiyo anaekipiga katika kikosi cha Kagera sugar Obrey Chirwa tayari ameweka kambani mabao 14 na kuwa kileleni mwa wafungaji.

 

Akifuatiwa na Adam Uledi wa Transit Camp ambaye amehamia KMC inayoshiriki Ligi Kuu ya NBC mwenye mabao 11 sawa na Ramadhani Hashimu kutoka timu ya B19 inayopambana vikali kusalia Ligi ya Championship ya NBC.

 

Nafasi ya tatu inashikwa na Boniface Brown wa Mbeya Kwanza mwenye mabao 10 sambamba na Abdereheman Mussa wa Transit Camp na Maulid Shaban kutoka Geita Gold wote wakiwa na idadi hiyo ya mabao.

 

Ushindani huu unaonyesha wazi kuwa msimu huu ni wa ushindani mkubwa ambapo kila mchezaji anapambana kuisaidia timu yake pamoja kuwania kiatu cha ufungaji bora.

SIMBA YAICHAPA NAMUNGO LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kwa mchezo mmoja ambapo Namungo walikuwa wenyeji wakiikaribisha Simba katika mchezo uliochezwa majira ya saa kumi jioni katika uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.

Mchezo huo ulimalizika kwa Simba kupata ushidi wa mabao 3-1 huku wakionyesha ubora wao hasa katika kipindi cha kwanza walipofanikiwa kupata bao la mapema kupitia kwa Libasse Gueye dakika ya 12 kabla ya kuongeza bao la pili kupitia kwa Anicet Oura dakika ya 25.

Namungo walijaribu kurejea mchezoni na kufanikiwa kupata bao lao dakika ya 33 kupitia Haritier Makambo aliyefunga kwa mkwaju wa penati lakini juhudi zao hazikutosha kuizuia timu ya Simba.

Kipindi cha pili Simba waliendelea kuwa hodari kwenye mchezo huo mbele ya mashabiki wao wa mkoa wa Lindi na kuongeza bao la tatu dakika ya 74 kupitia Elie Mpanzu aliyehitimisha ushindi huo Muhimu kwa ‘Mnyama’.

Ushindi huo unaifanya Simba kuwa na alama 42 ikishika nafasi ya pili huku Namungo wakiwa nafasi ya 10 na alama 22.

Katika mchezo huo winga wa Simba Anicet Oura alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.