Author: Honest Mwanitega

DABI YA DAR ES SALAAM.

IMESALIA Siku moja pekee kwa miamba ya soka nchini Tanzania Simba na Yanga kukutana katika mchezo wa duru la pili katika Ligi Kuu ya NBC utakaopigwa majira ya 11:00 jioni kwenye uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam jumapili Aprili 16 .

Fiston Mayele wa Yanga ndiye kinara wa kufunga mabao katika michezo ya Ligi Kuu akifunga 16 huku akifuatiwa na Moses Phiri wa Simba mwenye mabao 10.

Said Ntibazonkiza ndiye mchezaji aliehusika katika mabao mengi kwenye Ligi Kuu ya NBC (19) akifunga mabao 10 na kutoa pasi za mabao tisa huku akifuatiwa na Fiston Mayele wa Yanga aliehusika katika mabao 18 akifunga 16 na kutoa pasi mbili za mabao.

Timu hizo zinakutana Simba ikiwa kinara wa kufunga mabao katika Ligi Kuu NBC ikifunga mabao 60 huku Yanga ikishika nafasi ya pili na mabao 50.

YANGA KUENDELEZA REKODI LEO?

TIMU ya Yanga leo inaingia uwanjani ikiwa ugenini dhidi ya KMC kutafuta rekodi mpya ya kushinda katika michezo kumi mfululizo ya Ligi Kuu ya NBC kwenye uwanja wa Mkapa mkoani Dar es Salaam.

Mechi hiyo itakayochezwa saa 10:00 alasiri inakutanisha KMC ambayo haijapata matokeo katika mechi tano mfululizo dhidi ya Yanga iliyofanikiwa kushinda mechi tisa mfululizo za Ligi Kuu ya NBC.

KMC imeshinda mechi moja pekee dhidi ya Yanga kati ya tisa zilizopita, sare mechi mbili na kupoteza michezo sita huku ikiwa imeruhusu mabao 12 katika mechi hizo.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kocha msaidizi wa timu ya KMC Ahmad Ally amesema kuwa wanatambua uwezo wa Yanga na wamejipanga kushindana kupata ushindi.

“Tunakwenda kucheza dhidi ya timu bora inayoshiriki mashindano ya kimataifa, kinara wa Ligi na yenye muendelezo wa matokeo mazuri hivyo tumejiandaa vizuri kuchukua tahadhari na tupo tayari kupambana ili kupata alama tatu muhimu”  alisema Ahmad.

Timu ya Yanga inaingia katika mchezo huo siku tatu baada ya kupata ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe na endapo itapata ushindi leo itaongoza kwa tofauti ya alama nane dhidi ya timu ya Simba inayoshika nafasi ya pili.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari kocha msaidizi wa Yanga Cedric Kaze amesema sherehe za ushindi dhidi ya Mazembe zimekwisha hivyo nguvu zimeelekezwa katika mchezo wa Ligi Kuu leo ili kutetea ubingwa msimu huu.

“Hakuna siku tumewahi kucheza na KMC mechi ikawa rahisi hivyo tunaelewa ugumu wa mechi ya leo na kama tukiwa vizuri katika kila idara kwenye timu yetu tutafanikiwa kushinda na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa msimu huu” alisema Kaze.

 

 

MBOMBO, KANGWA KUIKOSA MZIZIMA DERBY LEO

TIMU ya Simba leo inaingia katika uwanja wa Mkapa mkoani Dar es Salaam kuikabili Azam FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaoanza saa 1:00 usiku.

Wekundu hao wa Msimbazi watajaribu kurudisha furaha kwa mashabiki wake baada ya kushindwa kupata walau alama moja katika michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya AC ya Guinea na Raja Casablanca ya Morocco.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana Oktoba 27 katika uwanja wa Mkapa, Dar mchezo ambao wenyeji Azam walifanikiwa kuondoka na alama zote tatu kwa bao 1-0 lililofungwa na Prince Dube.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kocha wa timu ya Simba Roberto Oliveira amesema kupoteza michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa sio sababu ya wachezaji wake kuwa na morali ya chini hivyo anatarajia kupata matokeo mazuri leo.

“Tumecheza vizuri sana mechi ya Ligi Kuu iliyopita dhidi ya Singida ingawa hatujafanya vema katika mechi za kimataifa haiwezi kuwa sababu ya kushindwa kupata alama tatu dhidi ya Azam hivyo tunaingia uwanjani akili zetu zikiwaza ushindi ili tuendelee kusalia katika nafasi nzuri ya kuwa bingwa wa Ligi Kuu NBC msimu huu” alisema Roberto

Naye kocha msaidizi wa timu ya Azam John Matambala amesema kuwa wamefanya marekebisho katika baadhi ya maeneo katika kiwanja cha mazoezi kwa takribani wiki mbili hivyo wako tayari kupambana kwaajili ya kupata alama tatu.

“Kiuhalisia timu yetu imekuwa na muendelezo wa matokeo yasiyoridhisha tangu kuanza kwa duru la pili hivyo lazima tujiandae kurekebisha makosa yetu ya nyuma na tuingie kwa tahadhari kubwa dhidi ya Simba kwani tukidharau tunaweza kupoteza mchezo huu” alisema Matambala.

Azam itaingia uwanjani bila huduma ya kinara wao wa mabao Idris Mbombo mwenye mabao saba na nahodha Bruce Kangwa wenye kadi tatu za njano.

SIMBA, YANGA KUPEPERUSHA BENDERA KIMATAIFA

Timu za Simba na Yanga zinazoshiriki mashindano ya kimataifa wikiendi hii zinaingia uwanjani kuanza safari ya kutafuta ubingwa wa kombe la klabu Bingwa Afrika na kombe la Shirikisho katika michezo ya makundi mzunguko wa kwanza.

Simba wawakilishi katika klabu Bingwa Afrika leo watakuwa ugenini katika nchi ya Guinea dhidi ya timu ya Horoya AC mechi itakayoanza majira ya 01:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki kwenye uwanja wa General Lansana Conte.

Huu ni mchezo wa pili katika kundi la Simba baada ya hapo jana timu ya Raja Casablanca ya Morocco ikiwa uwanja wa nyumbani kuanza kwa kuifunga Vipers ya Uganda mabao 5-0.

Timu ya Yanga itaanza ushiriki wake katika kombe la Shirikisho nchini Tunisia kesho katika mchezo dhidi ya timu ya US Monastir majira ya 01:00 usiku kwenye uwanja wa Olympic Rades jijini Tunis.

Timu ya Yanga iliyo katika kundi moja na TP Mazembe, Monastir na Real Bamako imefanikiwa kuingia hatua ya makundi mwaka huu katika mashindano ya kimataifa ikiwa ni baada ya miaka mitano.

Baada ya michezo hiyo ya kimataifa timu hizo zitarejea kuendelea na michezo ya Ligi Kuu ya NBC, Simba itacheza dhidi ya Azam katika uwanja wa Mkapa, Dar ikiwa ni ‘Mzizima derby’ Februari 21 na Yanga itakua ugenini dhidi ya KMC Februari 22 katika uwanja wa Mkapa, Dar.

LIGI KUU YA NBC NAMBA TANO UBORA AFRIKA

Ligi Kuu ya NBC imefanikiwa kushika nafasi ya tano katika viwango vya Ligi bora barani Afrika kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za mpira wa miguu (IFFHS).

Kwa mujibu wa Shirikisho hilo Ligi Kuu ya NBC imepanda kwa nafasi 23 kutoka nafasi ya 62 mpaka nafasi ya 39 kwa takwimu za dunia nzima.

Mwaka 2021 Ligi hii ilishika nafasi ya 10 katika bara la Afrika hivyo kupanda mpaka  nafasi ya tano kwa mujibu wa takwimu hizo mpya zilizotolewa na shirikisho hilo.

Ligi Kuu ya NBC imezidiwa na ligi za Misri inayoshika namba moja kwa bara la Afrika, Algeria (mbili), Morocco (tatu) na Sudan (nne) huku ikiwa juu ya ligi za Afrika Kusini (sita), Angola(saba), Tunisia(nane), Nigeria(tisa) na Zambia(10).

Kupanda kwa ubora wa Ligi hiyo kumetokana na mambo kadhaa ikiwemo kiwango bora cha usimamizi wa michezo, ubora wa viwanja, ubora wa klabu zinazoshiriki Ligi, vyombo vya habari vya ndani na nje vinavyoitangaza zaidi Afrika na duniani, mvuto wake wa hali ya juu unaosababisha iwe gumzo zaidi ukilinganisha na Ligi nyinginezo na mambo mengine mengi.

Ligi hiyo itaendelea tena februari 3, kwa michezo miwili timu ya Simba ikiikaribisha Singida Big Stars uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam saa 1:00 usiku huku Tanzania Prisons ikiwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar uwanja wa Sokoine, Mbeya saa 10:00 alasiri.