Author: Honest Mwanitega

WARATIBU WA MICHEZO WAPIGWA MSASA

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kwa kushirikiana na TFF jana Septemba 22, 2022 iliandaa semina ya waratibu wa michezo iliyofanyika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es saalam.
Semina hiyo ilikuwa na lengo la kuwaongezea ufanisi waratibu hao katika kusimamia michezo mbalimbali ya kimashindano iliyochini ya TFF na TPLB.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Steven Mnguto, aliwataka waratibu kuzingatia mafunzo watakayopewa na wakufunzi kwani mafunzo hayo yanafaida kubwa kwenye ufanisi wa Ligi.
“Sisi Bodi ya Ligi peke yetu hatuwezi nyinyi mmekua msaada mkubwa sana kwetu, zingatieni mafunzo mnayopewa kwani mmepata bahati ya kufundishwa na watu waliokatika mpira kwa muda mrefu na wabobezi.” Alisema Steven Mnguto.
Semina ilihusisha mafunzo ya nadharia na vitendo ambapo waratibu wa michezo walipata nafasi ya kufanya yale waliyofundishwa darasani.
Wakati wa kufunga semina hiyo Mkurugenzi wa mashindano wa TFF Salum Madadi aliwapongeza waratibu kwa kazi nzuri wanayoifanya.
“Sponsors (wadhamini) wanajenga Imani kubwa na shirikisho kutokana na kazi kubwa mnayoifanya, mwisho kabisa niwatakie utekelezaji mwema wa msimu wa 2022/2023.” Alisema Salum Madadi.
Semina hiyo ilihudhuriwa na waratibu kutoka mikoa zaidi ya 22 Tanzania Bara na wengine kutoka Zanzibar Pamoja na watumishi wa Bodi ya Ligi na TFF.

SIMBA, PRISONS NI REKODI NA HISTORIA LEO MBEYA,YANGA YAPANDA KILELENI

Kivumbi cha raundi ya nne ya Ligi Kuu ya NBC kinaendelea leo kwa mchezo mmoja kati ya Tanzania Prisons na Simba utakaochezwa saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mchezo wa mwisho kwa timu hizi kukutana ilikuwa ni Juni 26, 2022 kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya na Tanzania Prisons kuibuka na ushindi wa bao moja lililofungwa na Benjamin Asukile.

Mara ya mwisho kwa Simba kupata matokeo katika uwanja ugenini dhidi ya Tanzania Prisons ilikuwa ni Mei 5, 2019 waliposhinda kwa bao moja.

Jana michezo miwili ya raundi ya nne ilichezwa, Mbeya City wakiwaalika Azam FC ulitamatika kwa Azam kushinda kwa bao moja, Saa 1:00 usiku Yanga SC waliwakabili Mtibwa Sugar na kumalizika kwa Yanga kushinda kwa mabao matatu, ushindi huo unawapandisha Yanga hadi nafasi ya kwanza ya msimamo.

RAUNDI YA NNE KUANZA LEO MBEYA ,YANGA MTIBWA VITANI

Ligi kuu ya NBC inaendelea hii leo kwa michezo miwili ya raundi ya nne, saa 10:00 alasiri Mbeya City watawaalika Azam FC kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Kwenye michezo mitano ya mwisho ya Ligi Kuu kwa timu hizi kukutana, Azam wameshinda mara tatu, Mbeya City wakishinda mchezo mmoja huku wakitoka sare mchezo mmoja.

Saa 1:00 usiku kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Yanga SC watawakabili Mtibwa Sugar.

Kwenye msimamo wa Ligi ya NBC Mtibwa Sugar wapo nafasi ya pili wakiwa na alama saba sawa na Yanga wenye alama saba, timu yoyote itakayopata ushindi kwenye mchezo wa leo itapanda moja kwa moja kwenye nafasi ya kwanza ya msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

PRISONS MBEYA CITY KUISIMAMISHA MBEYA LEO

Wakazi wa jiji la Mbeya na viunga vyake leo  Septemba 9, 2022 wanakwenda kushuhudia ‘derby’ ya pili ndani ya msimu huu wa 2022/2023 na ya kwanza jijini hapo, ‘Mbeya Derby’ inayozikutanisha Tanzania Prisons na Mbeya City.

Timu hizi zimekutana mara 14 kwenye michezo ya Ligi Kuu ambapo Tanzania Prisons wameshinda mara nne, Mbeya City wakishinda mara tatu huku wakienda sare michezo saba.

Mara ya kwanza kwa timu hizi kukutana ilikuwa ni msimu wa 2015/2016 ambapo mchezo huu ulimalizika kwa Tanzania Prisons kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Katika michezo mitano ya mwisho ya Ligi Kuu timu hizi zilipokutana, Mbeya City wameonekana kuwa wababe kwa Tanzania Prisons, baada ya kuibuka na ushindi mara mbili na kwenda sare mara tatu.

Kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu wa 2022/2023 Mbeya City wapo nafasi ya saba wakiwa na alama tatu huku Tanzania Prisons wakiwa nafasi ya tisa na alama zao tatu utofauti ukiwa katika mabao ya kufunga na kufungwa.

KMC WAVUNJA MWIKO KWA SIMBA

Baada ya kusubiri kwa takribani misimu minne ya Ligi kuu bila kupata alama yoyote mbele ya Simba, KMC wamevunja mwiko huo baada ya kupata sare ya mabao mawili jana Septemba 7, 2022 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kabla ya mchezo wa jana, KMC tangu walipopanda daraja msimu wa 2018/2019 walicheza jumla ya michezo nane ya Ligi Kuu na Simba bila kupata alama yoyote.

Mchezo wa kwanza kuzikutanisha timu hizi ulikua ni Desemba 19, 2018 ambapo mchezo huo ulimalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, tangu hapo Simba iliweza kupata matokeo ya ushindi katika michezo saba mfululizo, mechi ya mwisho kwa timu hizi kukutana ilikua ni Juni 19, 2022 katika uwanja wa Benjamin Mkapa na Simba kuifunga KMC kwa Mabao 3-1.

Kwa matokeo hayo KMC wamepanda kwa nafasi mbili kutoka nafasi ya 13 kwenye msimamo hadi nafasi ya 11.

Mchezo unaofuata KMC watakuwa wenyeji wa Ihefu kwenye uwanja wa Uhuru Septemba 17, 2022 saa 10:00 Alasiri