Author: Honest Mwanitega

TAARIFA KUTOKA BODI YA LIGI KUU TANZANIA

KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Novemba 4, 2022 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;

 

Ligi Kuu ya NBC (NBCPL)

Mechi Namba 64: Young Africans SC 1-1 Simba SC

Timu ya Young Africans imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la kuingia chumba cha kuvalia kupitia mlango usio rasmi kuelekea mchezo tajwa hapo juu uliofanyika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Oktoba 23, 2022.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 17:(21 & 60) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

Mchezaji wa timu ya Young Africans, Stephan Aziz Ki na Clatous Chama wa klabu ya Simba wamefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kukwepa kusalimiana na wachezaji wa timu pinzani kabla ya kuanza kwa mchezo tajwa hapo.

Wachezaji hao kwa nyakati na mazingira tofauti walionekana kufanya hila kwa kusubiri nje ya kiwanja ili kusubiri zoezi la kusalimiana likamilike ndipo waingie kiwanjani.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni 41:5(5.4) ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti kwa Wachezaji.

 

Mashabiki na Wanachama wa klabu ya Yanga, Israel Suma, Kais Mwasongwe, Soud ‘Tall’ na Mohamed Mposo wamefungiwa miezi mitatu (3) kwa kosa la kuwavamia waamuzi wa mchezo tajwa hapo juu wakiwa wanaelekea chumbani wakati wa mapumziko, kabla walinzi wa uwanjani (Stewards) hawajaingilia kati na kuwaondoa.

Mashabiki na wanachama hao ambao wanatumiwa na klabu ya Young Africans kama maafisa wasaidizi wa usalama, walionekana kupitia picha jongeo (video) zilizonaswa na kamera za uwanja wa Benjamin Mkapa, wakifanya kitendo hicho wakiwa katika njia ya kuelekea vyumba vya kuvalia.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 47:2 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

 

Mechi Namba 74: Geita Gold FC 0-1 Young Africans SC

Mwamuzi wa kati, Florentina Zabron amepelekwa Kamati ya Waamuzi ya TFF kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria 17 za mpira wa miguu katika mchezo tajwa hapo juu.

Kamati ya Waamuzi ya TFF italitazama kitaalamu tukio la pigo la penati ya klabu ya Young Africans dhidi ya Geita Gold katika dakika ya 18 ya mchezo kabla ya kuishauri Kamati kwa kuzingatia kanuni ya 42:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti Waamuzi.

 

Ligi ya Championship

Mechi Namba 46: Pamba FC 1-0 Pan African FC

Timu ya Pan African imepewa onyo kwa kosa la kuchelewa kuwasili kwenye mkutano wa maandalizi ya mchezo (MCM) kwa dakika tano (5) huku pia ikichelewa kwenye chumba chao cha kuvalia wakati wa mapumziko jambo lililosababisha kipindi cha pili cha mchezo tajwa hapo juu kichelewe kuanza kwa dakika tano (5).

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 17:2(2.2) na 17:(33 & 60) ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

Mechi Namba 55: Fountain Gate FC 1-0 Ndanda FC

Klabu ya Fountain Gate imetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la mashabiki wake kwenda kusimama nyuma ya goli la klabu ya Ndanda na kuanza kumtolea lugha za matusi golikipa wa timu hiyo wakimshutumu kuwa ameweka kitu golini ambacho kinazuia Fountain Gate kupata ushindi.

Mashabiki hao walimshinikiza mtoto muokota mipira (ball kid) kwenda golini na kuchukua chupa ya maji ya golikipa huyo kisha kuitupa nje.

Adhabu hiyo ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

 

First League

Mechi Namba 6B: Mbao FC 1-1 Mwadui FC

Klabu za Mbao na Mwadui zimepewa onyo kwa kosa la kuwakilishwa na maafisa pungufu kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM).

Mbao waliwakilishwa na maafisa wanne (4) huku Mwadui wakiwakilishwa na maafisa wawili (2) badala ya watano (5) walioainishwa kikanuni.

Katika kikao hicho, Mwadui walikuwa na seti moja ya jezi za wachezaji wa ndani bila jezi za magolikipa wala soksi.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 18:2(2.2) na 18:60 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

Kamati imemfungia michezo mitatu (3) mtunza vifaa wa klabu ya Mbao, Bw. Chriss Shimbe baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi wa mchezo tajwa hapo juu kwa kosa la kurudia mara kadhaa kupinga maamuzi ya waamuzi wa mchezo huo.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 47:21 ya First League kuhusu Udhibiti kwa Viongozi.

 

Mechi Namba 6B: Cosmopolitan FC vs Majimaji FC

Klabu ya Cosmopolitan imepewa ushindi wa alama tatu (3) na mabao matatu (3) huku klabu ya Majimaji ikitozwa faini ya Sh. 2,000,000 (milioni mbili) na kupokwa alama 15 katika msimamo wa Ligi kwa kosa la kushindwa kufika kwenye kikao cha maandaalizi ya mchezo na baadae uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo tajwa hapo juu.

Maafisa wa mchezo huo walisubiri kwa dakika 30 kama ilivyoainishwa kwenye kanuni kabla ya kuahirisha mchezo huo baada ya klabu ya Majimaji kutoonekana uwanjani.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 31:1(1.6) ya First League kuhusu Kutofika Uwanjani.

 

Mechi Namba 10A: African Lyon FC vs Njombe Mji FC

Klabu ya African Lyon imepewa ushindi wa alama tatu (3) na mabao matatu (3) huku klabu ya Njombe Mji ikitozwa faini ya Sh. 2,000,000 (milioni mbili) na kupokwa alama 15 katika msimamo wa Ligi kwa kosa la kushindwa kufika kwenye kikao cha maandaalizi ya mchezo na baadae uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo tajwa hapo juu.

Maafisa wa mchezo huo walisubiri kwa dakika 30 kama ilivyoainishwa kwenye kanuni kabla ya kuahirisha mchezo huo baada ya klabu ya Njombe Mji kutoonekana uwanjani.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 31:1(1.6) ya First League kuhusu Kutofika Uwanjani.

Mechi Namba 10B: Stand United FC 2-1 Rhino Rangers FC

Klabu za Stand United na Rhino Rangers zimepewa onyo kwa kosa la kuwakilishwa na maafisa pungufu kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM).

Mbao na Rhino ziliwakilishwa na maafisa wanne (4) kila moja badala ya watano (5) walioainishwa kikanuni.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 18:2(2.2) na 18:60 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

Mechi Namba 11B: TMA FC 2-0 Alliance FC

Klabu ya Alliance imepewa onyo kwa kosa la kutoingia kwenye chumba cha kuvalia katika mchezo tajwa hapo juu kwa kile walichoeleza kuwa walisahau ufunguo wa mlango wa chumba hicho ambao walikabidhiwa kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM).

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 18:20 na 18:60 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

 

RUVU SHOOTING, PRISONS HAKUNA MBABE

TIMU ya Ruvu Shooting imeshindwa kupata ushindi katika mchezo wa sita mfululizo baada ya kulazimishwa sare ya bao moja na Tanzania Prisons katika mchezo uliochezwa uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Tanzania Prisons ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Samson Mbangula dakika tano baada ya kipindi cha pili kuanza lililodumu kwa dakika nane pekee kabla ya Ruvu kusawazisha kwa mkwaju wa penati dakika ya 58 kupitia kwa Abalkassim Suleiman.

Ruvu Shooting watajilaumu kwa kushindwa kutumia nafasi walizopata ikiwemo mkwaju wa penati aliokosa Abalkassim Suleiman dakika chache kabla ya mpira kumalizika.

Akizungumza baada ya mchezo kocha wa Ruvu Shooting Charles Mkwasa amesema kuwa timu yake ilistahili kupata alama tatu katika mchezo wa leo hivyo matokeo ya sare kwao ni sawa na kupoteza.

Naye kocha wa Tanzania Prisons, Patrick Odhiambo ameonesha kufurahishwa na matokeo waliyopata na kukiri kwamba Ligi Kuu ya NBC msimu huu ni ngumu hivyo kupata alama moja ugenini si jambo dogo kwao.

“Ni faraja kwetu kupata alama moja ugenini kwani ligi ya msimu huu ni ngumu sana hivyo tutafanya maandalizi mazuri kuhakikisha tunapata ushindi katika michezo yote ya nyumbani,” alisema Odhiambo.

Ligi Kuu NBC itaendelea tena Novemba 9 kwa michezo miwili, Azam FC watakuwa wenyeji wa Dodoma Jiji katika uwanja wa Azam Complex huku Singida Big Stars ikiwakaribisha Simba SC katika uwanja wa CCM Liti mjini Singida.

 

RUVU SHOOTING TAYARI KWA ‘VITA’ YA MAJESHI UHURU

 

BAADA ya kupoteza michezo mitatu mfululizo ya Ligi Kuu NBC, timu ya Ruvu Shooting itashuka kwenye uwanja wa Uhuru Novemba 6, kuwakaribisha Tanzania Prisons katika mchezo utakaokutanisha timu mbili zinazomilikiwa na majeshi ya Tanzania.

Akizungumza katika mkutano na  wanahabari mapema leo kocha msaidizi wa Ruvu Shooting, Rajab Mohamed amesema mchezo wa kesho utakuwa mgumu na muhimu sana kwao na wamejiandaa kikamilifu kuhakikisha wanapata ushindi

“Mechi yetu dhidi ya Prisons haijawahi kuwa rahisi, wachezaji wetu wanatambua hilo na tumefanyia masahihisho makosa yetu ya michezo iliyopita hivyo tunaenda kupambana kupata alama tatu muhimu,” alisema Rajab.

Kwa upande wake kocha wa Tanzania Prisons, Shaban Mtupa amesema wapo tayari kwa mechi ya kesho na wanafahamu ubora wa timu ya Ruvu, wanaamini watapata matokeo mazuri kutokana na maandalizi waliyofanya.

“Tumefanya maandalizi mazuri ukizingatia msimu uliopita tulipoteza michezo yote miwili dhidi ya Ruvu Shooting, tupo tayari kwa mchezo wa kesho kuhakikisha tunapata alama tatu,” alisema Shaban.

Ligi Kuu ya NBC inaendelea tena leo kwa mchezo kati ya Polisi Tanzania inayoikaribisha Singida Big Stars majira ya saa 10:00 alasiri katika mchezo wa pili wa raundi ya 11 utakaochezwa kwenye uwanja wa Black Rhino Academy, Arusha.

MBEYA CITY YAFUTA ‘UTEJA’ KWA NAMUNGO

Timu ya Mbeya City imemaliza uteja wake wa kupoteza mechi dhidi ya Namungo kwa kuifunga mabao 2-1 na kupanda nafasi nne za juu katika msimamo wa Ligi Kuu NBC

Mchezo huo wa tano kwa Mbeya city wakicheza katika uwanja wa nyumbani ulishuhudia mabao ya timu hiyo yakifungwa na Sixtus Sabilo na Hassan Muhamud huku bao pekee la Namungo likifungwa na Reliants Lusajo akifikisha mabao sita na kuwa kinara wa wafungaji katika Ligi ya NBC

Matokeo hayo yanaifanya Mbeya City kufikisha alama 15 baada ya mechi tisa huku Namungo wakisalia na alama 15 baada ya kucheza mechi 10

Mchezo huo ulishuhudiwa ukimalizika Dakika zote 90 bila mchezaji yeyote kuonyeshwa kadi ya njano wala nyekundu

Ligi hiyo itaendelea tena Novemba 6 kwa mchezo kati ya Polisi Tanzania dhidi ya Singida Big Stars katika uwanja wa Black Rhino Academy uliopo Karatu mkoani Arusha .

NAMUNGO KUENDELEZA UBABE KWA MBEYA CITY LEO?

Timu ya Mbeya City leo inaikaribisha timu ya Namungo kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya katika muendelezo wa michezo ya Ligi Kuu ya NBC kuanzia saa 10:00 alasiri.

Mbeya City inashuka uwanjani ikiwa na rekodi mbaya dhidi ya Namungo ikifanikiwa kushinda mechi moja kati ya sita zilizopita, ikipata sare moja na kupoteza mechi nne.

Namungo inaingia katika uwanja huo wa Sokoine ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kulazimishwa sare katika dakika za nyongeza kwenye mchezo uliopita dhidi ya Tanzania Prisons baada ya mchezaji wake Frank Magingi kushindwa kuokoa mpira na kujifunga.

Mchezo huu wa leo ni wa ufunguzi wa raundi ya 11 itakayoshudia michezo mingine sita ikipigwa katika viwanja tofauti huku mchezo mmoja, Coastal Union dhidi ya Dodoma Jiji ukitarajiwa kupangiwa tarehe nyingine.