Author: Loveness Bernard

KARIA AFUNGUA SEMINA YA FIFA KUHUSU WELEDI KATIKA UENDESHAJI KLABU NCHINI.

Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wallace Karia amefungua semina ya siku mbili iliyoandaliwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) jijini Dar es salaam kuhusu weledi katika uendeshaji wa klabu nchini kwa wenyeviti na watendaji wakuu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo Karia amewashukuru timu ya FIFA chini ya Mkuu wa Maendeleo ya Programu wa FIFA, Solomon Mudege kwa kuweka semina hii kwa wenyeviti na watendaji wakuu wa klabu za Ligi Kuu ya NBC.

Karia amesema kuwa uanzishwaji wa program hii kwa klabu hususani namna klabu zitakavyofanya biashara ya mpira kiueledi zaidi na pia wakati wa program hii wataelewa namna ya kushughulikia mipango mikakati ya klabu zao.

Aidha Karia amesema kuwa kama unataka klabu yako kuwa sahihi ndani nje ya uwanja unapaswa kuwa na mpango mkakati maalumu.

Programu hii itazisaidia klabu kubadilisha mtazamo katika kila Nyanja ili kwenda na wakati.

“Naamini baada ya programu hii klabu zetu zitabadili mtazamo kwa upande wa uongozi na mtafanya mambo yote kwa ufanisi mkuu nami sina budi kumshukuru Rais wa FIFA, Gianni Infantino kwa programu hii inayokidhi mazingira yetu ya kiafrika na tunatamani ziwepo nyingi zaidi” amesema Karia.

Karia amemaliza kwa kutoa nukuu maarufu isemayo kuwa malengo bila mpango ni sawa na matamanio hivyo amewaomba washiriki wa program hii kuweza kuwafundisha wenzao katika klabu ili hata kama ikitokea wameondoka wawepo watu kuendeleza mipango mikakati iliyowekwa na klabu.

AZAM YATAMBA UGENINI ,SINGIDA, COASTAL HAKUNA MBABE

Ligi Kuu ya NBC jana iliendelea kwa michezo miwili iliyochezwa jijini Dar es Salaam katika Uwanja wa Azam Complex na Uwanja wa Amaan Complex visiwani Zanzibar.

Timu ya Yanga ilikuwa mwenyeji wa Azam katika mchezo maarufu kama ‘dabi ya Dar es Salaam’ na kupoteza kwa bao moja huku beki wa Yanga Ibrahim Bacca akishindwa kumaliza mchezo baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumfanyia rafu mshambuliaji wa Azam Nassoro Saadun.

Gibril Sillah ndiye aliyefunga bao pekee dakika ya 34 ya mchezo huo uliokuwa na upinzani mkali kwani timu zote zilikuwa zikishambuliana muda wote.

Mchezo wa pili uliochezwa saa mbili na nusu usiku mjini Zanzibar Singida Black Star walishindwa kutamba mbele ya timu ya Coastal Union baada ya kulazimishwa suluhu.

Ligi Kuu ya NBC leo itaendelea jijini Mbeya ambapo Tanzania Prisons watawakaribisha KenGold katika Uwanja wa Sokoine saa 10 alasiri.

COASTAL YATAMBA, KENGOLD, DODOMA HAKUNA MBABE

 

LIGI Kuu ya NBC jana iliendelea katika viwanja vya Sokoine jijini Mbeya katika mchezo uliozikutanisha KenGold na Dodoma Jiji na kwenye uwanja Sheikh Amri Abeid Arusha Coastal Union wakiwakaribisha Kagera Sugar michezo iliyopigwa saa 10:00 alasiri.

Katika michezo hiyo KenGold iligawana alama na timu ya Dodoma Jiji baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 yalifungwa na Mishamo Daud kwa upande wa KenGold huku Dissan Galiwango na Zidane Sereri wakifunga mabao ya Dodoma Jiji.

Kwa upande wa Coastal Union Kiungo Mshambuliaji Charles Semfuko alifanikiwa kufunga bao dakika ya 85 ya mchezo huo ambao uliisha kwa Coastal kuibuka washindi na kukusanya alama zote tatu za mchezo huo.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo Visiwani Zanzibar timu ya Singida Black Star watawakaribisha Yanga katika Uwanja wa Amaan mjini Unguja saa 2:30 usiku.

VITA YA KITAMBI NA GAMONDI NANI KUKAA KILELENI?

Ligi Kuu ya NBC kesho itaendelea Zanzibar kwa mchezo namba 40 utakaozikutanisha timu za Singida Black Star na Yanga utakaochezwa saa 2:30 usiku katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Katika mchezo huo timu mbili zinazoongoza msimamo wa Ligi Kuu ya NBC zitakutana, Singida Black Star iliyocheza michezo nane ikiongoza msimamo kwa kuwa na alama 22, ikifunga mabao matatu na kuruhusu nyavu zao ‘kutikiswa’ mara tatu huku ikiwa imeshinda mechi saba na kupata  sare moja.

Kwa upande wa Yanga inayoshikilia nafasi ya pili katika msimamo huo imecheza michezo saba imeshinda mechi zote kwa kufunga mabao 12 na kuvuna alama zote 21 huku ikiwa haijaruhusu nyavu zao ‘kutikiswa’ na wapinzani wao.

Ikumbukwe kuwa utakuwa ni mchezo huo utaamua nani kuwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kati ya Singida ikiongozwa na kocha wake Dennis Kitambi ama Yanga chini ya Miguel Gamondi.

NAMUNGO YAIZAMISHA PAMBA, FOUNTAIN GATE, MASHUJAA HAKUNA MBABE.

Ligi Kuu ya NBC imeendelea na kushuhudia michezo miwili ikichezwa katika viwanja vya Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara na Majaliwa mkoani Lindi.

Mchezo wa kwanza uliochezwa majira ya jioni timu ya Fountain Gate iliikaribisha timu ya Mashujaa na kushuhudia sare ya mabao 2-2.

Mabao ya Fountain Gate yalifungwa na Nicholas Gyan na Salum Kihimbwa huku magoli ya Mashujaa yakifungwa na Seif Karihe na Hassan Ali.

Mchezo wa pili uliochezwa Uwanja wa Majaliwa Lindi timu ya Namungo waliwakaribisha Pamba Jiji ya Mwanza katika mchezo ambao wenyeji Namungo walifanikiwa kubaki na alama tatu muhimu za mchezo huo baada ya mchezaji wao Ibrahim Abdallah kufunga goli pekee dakika ya 14 ya mchezo huo.

Ligi ya NBC leo itaendelea kwa michezo miwili ambapo KenGold watawakaribisha Dodoma Jiji katika Uwanja wa Sokoine Mbeya na Coastal Union watawakaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Sheikhe Amri Abeid jijini Arusha huku michezo yote ikitarajiwa kuanza saa 10:00 alasiri.