Author: Yahaya Abushehe

Mahesabu makali Championship

MAHESABU MAKALI NBC CHAMPIONSHIP IKIINGIA MZUNGUKO WA 18.

Mzunguko wa 18 wa NBC Championship unaanza leo ukiwa umebeba presha na mahesabu makali kwa kila timu. Kadri msimu unavyoelekea hatua ya mwisho, kila alama imekuwa ya thamani kubwa katika mbio za kupanda Ligi Kuu ya NBC na vita ya kujiokoa kushuka daraja.

Timu nne zilizo juu ya msimamo Geita Gold, Kagera Sugar, Mbeya Kwanza na Transit Camp zinaingia katika mzunguko huu zikitambua kuwa ushindi pekee ndio utakaozidi kuweka hai ndoto zao za kupanda daraja. Tofauti ya alama kati yao si kubwa, hali inayofanya kila mchezo kuwa wa hadhi ya fainali.

Katika ratiba ya mzunguko huu, Kagera Sugar itaialika Bigman kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera, huku Transit Camp wakisafiri hadi Songea kuvaana na Songea United katika Uwanja wa Majimaji.
Macho mengi yataelekezwa mkoani Geita ambako Geita Gold watakuwa wenyeji wa Mbeya Kwanza kwenye Uwanja wa Nyankumbu, mchezo unaotajwa kuwa na uzito mkubwa katika kuamua mwelekeo wa kileleni.

Lakini kwa upande wa chini ya msimamo nao si shwari. Timu za B19, Hausung, Barberian na African Sports zinaingia katika michezo ya mzunguko huu zikiwa chini ya presha kubwa ya kutafuta ushindi ili kujinasua kutoka kwenye mstari wa kushuka daraja na michezo ya mtoano.

Kupoteza alama katika hatua hii kunaweza kuongeza mzigo wa presha na kuifanya mizunguko ijayo kuwa migumu zaidi kwao.

Majibu ya mahesabu makali ya mzunguko wa 18 yatapatikana ndani ya dakika 90 za kila mchezo. Je, ni nani ataongeza kasi ya alama na kujitenga kileleni? Na nani atasalia kuhesabu maumivu ya kupoteza nafasi muhimu?

NBC Championship imeingia katika hatua ambayo makosa madogo yanaweza kugharimu msimu mzima.

Transit VS Kagera

NI VITA YA NAFASI NBC CHAMPIONSHIP LEO

LIGI ya Championship ya NBC inaendelea leo kwa michezo miwili mikubwa yenye uzito wa kipekee katika kupambania nafasi za juu na kuepuka hatari ya kushuka daraja.

Katika mchezo unaovuta hisia za mashabiki wengi, Transit Camp itaialika Kagera Sugar kwenye uwanja wa Filbert Bayi mkoani Pwani, huku mchezo mwingine ukizikutanisha Hausung na African Sports katika uwanja wa Amani, mkoani Njombe.

Transit Camp inayoshika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi ikiwa na alama 33, inaingia uwanjani ikiwa na lengo moja tu la ushindi na kukusanya alama tatu zitakazoiwezesha kufikisha jumla ya alama 36 na kupanda hadi nafasi ya pili, ikinufaika na faida ya matokeo ya ana kwa ana (head to head) dhidi ya Kagera Sugar.

Kwa upande wao, Kagera Sugar waliopo nafasi ya pili wakiwa na alama 36, wanahitaji ushindi ili kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC, wakisubiri pia kwa jicho la pili matokeo ya mchezo wa Geita Gold dhidi ya Barberian unaotarajiwa kuchezwa kesho.

Ushindani wa alama na nafasi baina ya timu hizo mbili unaipa mechi hiyo hadhi ya ushindani wa kweli, ikitarajiwa kuwa miongoni mwa michezo inayofuatiliwa kwa karibu zaidi leo, hasa kutokana na ubora wa vikosi na mwenendo wao katika michezo ya hivi karibuni.

VITA YA KUBAKI LIGI YA CHAMPIONSHIP YA NBC

Wakati huo huo, vita nyingine ya kusaka uhai itapigwa Njombe, ambapo Hausung na African Sports zitavaana katika pambano la kujiokoa dhidi ya mstari wa kushuka daraja huku timu zote mbili zikikusanya alama nane na zikitofautiana tu katika idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Ushindi kwa Hausung (nafasi ya 14) au African Sports (nafasi ya 15) utaifanya timu husika kupaa hadi nafasi ya 13 hatua muhimu katika mbio za kusalia Ligi ya Championship ya NBC.

Mchezo wa Transit Camp dhidi ya Kagera Sugar utarushwa mubashara (Live) kupitia chaneli ya FIFA+, kuwapa fursa mashabiki wengi kushuhudia moja ya michezo mikubwa ya msimu huu.

Saa 72

TAARIFA YA KAMATI YA SAA 72

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Desemba 15, 2025 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;

Ligi Kuu ya NBC

Mechi Namba 032:  Singida BS FC 1-3 TRA United FC

Mchezaji Khalid Aucho wa klabu ya Singida BS ya mkoani Singida amefungiwa michezo mitano (5) na kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kufanya kitendo kisicho cha kiuanamichezo kwa kumpiga na kumsukuma mchezaji Adam Adam wa klabu ya TRA United wakati wa mchezo tajwa hapo juu.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:21 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu, Alex Pancras kutoka Dar es Salaam amepewa Onyo Kali kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu na kushindwa kuchukua hatua stahiki kwa kitendo cha ukiukwaji wa sheria za mpira kilichofanywa na mchezaji Khalid Aucho.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.6) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.

Mechi Namba 031: Simba SC 0-2 Azam FC

Mchezaji Jonathan Sowah wa klabu ya Simba ya mkoani Dar es Salaam amefungiwa michezo mitano (5) na kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kufanya kitendo kisicho cha kiuanamichezo kwa kumpiga kiwiko mchezaji Himid Mao wa klabu ya Azam wakati wa mchezo tajwa hapo juu.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:21 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Mchezaji Allasane Kante wa klabu ya Simba ya mkoani Dar es Salaam amefungiwa michezo mitano (5) na kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kufanya kitendo kisicho cha kiuanamichezo kwa kumpiga teke kwa makusudi mchezaji Feisal Salum wa klabu ya Azam wakati wa mchezo tajwa hapo juu.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:21 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu, Abdallah Mwinyimkuu kutoka Singida ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano (5) kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu na kushindwa kuchukua hatua kwa vitendo vya ukiukwaji wa sheria za mpira vilivyofanywa na wachezaji Jonathan Sowah na Allasane Kante katika mchezo huo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.6) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.

Mechi Namba 046:  Coastal Union FC 0-1 Young Africans SC

Klabu ya Young Africans ya mkoani Dar es Salaam imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la shabiki wake kuruka uzio na kuingia kwenye eneo la kuchezea (pitch), ambapo shabiki huyo alionekana kufika hadi kwenye goli la timu ya Coastal Union na kuinama kama Ishara ya kutafuta, kuchukua ama kuweka kitu.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

MUHIMU

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inazikumbusha klabu zake kuendelea kusisitiza umuhimu wa mchezo wa kiungwana na tabia njema mchezoni kwa wachezaji, viongozi na mashabiki wake. Ukumbusho huu unakuja kufuatia mfululizo wa matukio ya wachezaji kufanya vitendo visivyo vya kiuanamichezo kwa wachezaji wenzao ikiwemo kupiga.

Pamoja na kuhatarisha usalama wa wachezaji, matukio hayo pia yamekuwa yakileta taswira mbaya kwa Ligi yetu jambo ambalo linaweza kushusha hadhi yake na kwamba licha ya adhabu kali ambazo zimekuwa zikitolewa kwa wachezaji husika, bado matukio hayo yameonekana kuendelea viwanjani.

Ligi ya Championship ya NBC

Mechi Namba 061:  African Sports Club 0-2 Transit Camp FC

Klabu ya Transit Camp ya mkoani Dar es Salaam imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kuwakilishwa na maofisa wanne (4) badala ya watano (5) kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM) kuelekea mchezo tajwa hapo juu kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:2(2.1) ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

First League

Mechi Namba 7A: Alliance FC vs Biashara United

Klabu ya Alliance ya mkoani Mwanza imepewa ushindi wa mabao matatu (3) na pointi tatu (3) katika mchezo tajwa hapo juu, huku Biashara United ikipoteza mchezo huo kwa mujibu wa Kanuni ya 17:31 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

Biashara United ilisababisha mchezo huo kuvunjwa katika dakika ya 67 baada ya wachezaji wawili (2) wa timu hiyo iliyoanza mchezo ikiwa na wachezaji wanane (8) tu, kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo hivyo kufanya timu hiyo kusalia na wacheza sita (6) pekee ambao hawawezi kufanya mchezo uendelee kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni ya 17:30 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 10A: Pan African FC vs Moro Kids FC

Klabu ya Pan African ya mkoani Dar es Salaam imepoteza mchezo tajwa hapo juu na timu ya Moro Kids imepewa ushindi wa mabao matatu (3) na alama tatu (3) kwa kosa la Pan African kushindwa kuandaa mchezo huo kikamilifu, jambo lililosababisha mchezo huo kushindwa kufanyika kwa mujibu wa Kanuni.

Pan African ilishindwa kupeleka uwanjani gari maalum la kubebea wagonjwa (Ambulance) kama ilivyoelekezwa kwenye Kanuni ya 17:7 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo, hata baada ya kupita dakika 30 za kusubiri kwa mujibu wa kanuni.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:7 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo na Kanuni ya 32:1 ya First League kuhusu Kuvuruga Mchezo.

Nassor Idrissa

NASSOR IDRISSA MWENYEKITI MPYA BODI YA LIGI.

NASSOR Idrissa ‘Father’ amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) baada  ya kupata kura saba (7) dhidi ya kura sita (6) za mpinzani wake CPA Hosea Lugano kwenye uchaguzi uliofanyika jana Novemba 29, 2025 katika Hotel ya Golden Tulip, Masaki Jijini Dar Es Salaam.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Nassor alisisitiza chini ya utawala wake atahakikisha haki inapatikana kwa kila timu bila kujali ukubwa wa timu, hususani maamuzi yanayotolewa ndani ya Dakika 90 za mchezo.

Katika Hatua nyengine Hassan Muhsini Mwenyekiti wa Coastal Union amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania ambapo katika nafasi hiyo hakuwa na mpinzani hivyo kupitishwa kwa kura ya ndio wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).

Pia Japhet Makau Rais wa Fountain Gatena Gilbert Nkolonko Mwenyekiti wa Mbeya City wamechaguliwa kuwa wajumbe wawakilishi wa klabu za Ligi Kuu ya NBC huku Ahmed Gao wa Bigman na John Ndumbaro wa Mbeya City wakichaguliwa kuwa wajumbe wawakilishi wa klabu za Ligi ya Championship ya NBC wakati huohuo Azim Khan wa Dar City akichaguliwa kuwa mjumbe muwakilishi wa klabu za First League.

kagera sugar kupindua meza

KAGERA SUGAR KUPINDUA MSIMAMO LEO ?

Kagera Sugar inashuka Dimbani hii leo Novemba 22 kuwakabili Polisi Tanzania kwenye muendelezo wa Ligi ya Championship ya NBC 2025/2026 mchezo utakao chezwa kwenye uwanja wa Kaitaba kuanzia saa 10:00 alasiri.

Kagera Sugar inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC ikiwa na alama 13 sawa na Geita Gold inayoshika nafasi ya kwanza wakitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Kwa upande wa Polisi Tanzania ina jumla ya Alama 10 baaada ya michezo mitano ya Ligi ya Championship ya NBC ikishinda michezo mitatu, kufungwa mmoja na kutoka sare mchezo mmoja.

UShindi kwenye mchezo wa leo unaweza kuwapeleka ‘Wana Nkurukumbi’ Kagera Sugar kwenye kilele cha Ligi ya Championship ya NBC ikiwa mpinzani wake wa Karibu Geita Gold akipata matokeo mengine tofauti na ushindi.

Mkoani Tanga African Sports itaikaribisha Geita Gold kinara wa Ligi ya Championship ya NBC kwenye uwanja wa Mkwakwani mchezo utakaoanza saa 10:00 alasiri, Mchezo huu utarushwa Mubashara ‘Live’ kupitia FIFA+.