LIGI Kuu ya NBC iliendelea jana kwa michezo miwili ya mzunguko wa 22 kuchezwa viwanja viwili jijini Dar es Salaam.
Mchezo wa kwanza ulichezwa saa kumi jioni ambapo timu ya JKT Tanzania iliwakaribisha timu ya KenGold kutoka Mbeya katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni mkoani Dar es Salaam.
Mchezo ulianza kwa kasi ambapo kila mchezaji alipambana kuhakikisha timu yake inapata alama muhimu ,dakika ya 45 mchezaji wa JKT, Edward Songo aliipatia timu yake goli kwa mkwaju wa penati hivyo kuifanya timu yake kwenda mapumziko ikiwa kifua mbele.
Kipindi cha pili kianza ambapo Ken Gold walionekana wakilisaka kwa kasi lango la JKT Tanzania na dakika ya 85 mchezaji wa wao Selemani Bwenzi aliwaamsha mashabiki wa ‘makarasha’ kwa kuipatia timu yake bao la kusawazisha na kufanya mchezo kuisha wakiwa wamegawana alama moja moja.
Mchezaji wa Ken Gold Seleman Bwenzi alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo.
JKT Tanzania wamefikisha alama 27 wakiwa wamefunga mabao 16 na kuruhusu mabao 16 na wakiwa nafasi ya sita baada ya kucheza mizunguko 22 ya Ligi Kuu ya NBC 2024/2025.
KenGold wanaendelea kusalia nafasi ya 16 kwenye msimamo wakiwa na alama 15 wakifunga mabao 18 kuruhusu 38 baada ya mizunguko 22 ya Ligi Kuu ya NBC.
Mchezo wa pili ni timu ya Azam iliwapokaribisha timu ya Namungo katika uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi mchezo uliochezwa saa moja jioni.
Ilimchukua dakika 12 mchezaji wa Namungo, Hamis Halifa kuwaweka mbele timu yake kabla ya mchezaji wa Azam, Gibril Sillah kuweka mzani sawa katika dakika ya 43 ya mchezo huo hivyo timu zote kwenda mapumziko ubao ukisomeka 1-1 matokeo yaliyobaki mpaka mwisho wa mchezo.
Mlinda mlango wa Namungo, Jonathan Nahimana alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.
Azam wapo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC wakiwa na alama 45 wakifunga mabao 32 kufungwa 12 huku Namungo wakiwa nafasi ya 12 wakiwa na alama 23 wakifunga mabao 16 na kuruhusu mabao 27.
Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo kwa michezo miwili ambapo timu ya Pamba Jiji itawakaribisha Young Africans katika uwanja wa CCM Kirumba huku Tabora United wakiwakaribisha Dodoma Jiji katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.