Category: STORY

AZAM YAWEKA REKODI MPYA

TIMU ya Azam imekua ya kwanza katika historia ya Ligi Kuu NBC kupata matokeo ya ushindi katika mechi nane mfululizo baada ya kuifunga  Polisi Tanzania bao 1-0 ugenini.

Likiwa bao la kwanza kufunga msimu huu kwa Ayoub Lyanga dakika ya 15 limetosha kuifanya timu ya Azam kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi katika nafasi ya pili kwa kushinda mechi 11 kutoa sare mbili na kupoteza mbili.

Ushindi huo umeendelea kuididimiza timu ya Polisi mkiani katika msimamo wa Ligi ikisalia na pointi tisa katika nafasi ya 16 baada ya kukamilisha michezo 15 ya mzunguko wa kwanza.

Mchezo huo ulikuwa wa kwanza kwa Kocha wa zamani wa timu ya Yanga Mwinyi Zahera kuongoza timu ya Polisi huku mchezo wake wa pili akitarajiwa kukutana na timu yake ya zamani Disemba 17 katika uwanja wa Mkapa mkoani Dar es Salaam.

Mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu NBC unatarajiwa kumalizika Disemba 7 kwa michezo miwili, mapema saa 8:00 mchana timu ya Singida Big Stars itakuwa mwenyeji wa Coastal Union ya Tanga kwenye uwanja wa Liti, Singida huku uwanja wa Majaliwa, Lindi Namungo itaikaribisha Yanga majira ya saa 1:00 usiku.

 

POLISI TANZANIA KUTOKA MKIANI LEO ?

TIMU ya Polisi Tanzania ikiwa imeshinda michezo michache (2) kuliko timu yoyote katika Ligi Kuu NBC msimu huu leo inawakaribisha Azam FC katika uwanja wa Ushirika, mkoani Kilimanjaro saa 10:00 alasiri.

Polisi imeshinda mchezo mmoja katika uwanja wa nyumbani dhidi ya Namungo ya mkoani Lindi kwa bao 1-0 na mchezo mmoja ugenini dhidi ya Ihefu ya Mbarali, Mbeya kwa mabao 2-1.

Mchezo wa mwisho kucheza katika uwanja wa nyumbani Polisi ilipoteza kwa mabao 3-1 dhidi ya Simba na endapo timu hiyo itashinda katika mchezo wa leo itajinasua kutoka nafasi ya mwisho katika msimamo na kupanda kwa nafasi mbili.

Wapinzani wa Polisi katika mchezo wa leo timu ya Azam imepata ushindi katika michezo saba mfululizo chini ya kaimu kocha mkuu Kali Ongala na kukusanya pointi 32 wakishika nafasi ya tatu.

Azam ikipata ushindi katika mchezo huo itakusanya jumla ya pointi 35 sawa na kinara wa msimamo wa Ligi Yanga wakizidiwa kwa mabao tisa huku vinara hao wakiwa na mchezo mmoja mkononi.

SIMBA YAPANDA KILELENI, PHIRI, MAYELE WAENDELEZA VITA

TIMU ya Simba imemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu NBC kwa kicheko baada ya kuichapa Coastal Union mabao 3-0 katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Kwa ushindi huo wa ugenini Simba imefikisha pointi 34 na kuwa vinara wakiwazidi mahasimu wao Yanga kwa pointi mbili na michezo miwili.

Mabao ya Moses Phiri dakika ya 53 na 61 na moja la Clatous Chama dakika ya 89 yameibakisha timu ya Coastal Union nafasi ya 13 ikiwa na point 12 baada ya michezo 14.

Mabao mawili ya Moses Phiri yamemfanya kufikisha mabao 10 sawa na Fiston Mayele wa Yanga na kuungana kuwa vinara wa mabao.

Pasi ya Clatous Chama iliyozaa bao la kwanza la Moses Phiri inamfanya kufikisha pasi saba na kuwa kinara wa pasi zilizozaa mabao.

Mchezo wa mapema Ruvu Shooting imeendelea kusota kwa kushindwa kupata matokeo katika michezo saba mfululizo baada ya kufungwa na timu ya Dodoma Jiji mabao 2-1.

Mabao ya Hassan Mwaterema na Salum Kipaga aliyejifunga yameisogeza Dodoma mpaka nafasi ya 12 kwa kufikisha pointi 15 huku bao pekee la Ruvu lililofungwa na Ally Bilali likiibakiza Ruvu nafasi ya 15 na alama 11 baada ya michezo 15.

KALI ONGALA AENDELEZA REKODI, SIMBA YANGURUMA MOSHI

Timu ya Azam chini ya kocha Kali Ongala imepata ushindi wa saba mfululizo katika michezo ya Ligi Kuu NBC baada ya kuifunga Coastal Union ya Tanga mabao 3-2.

Ushindi huo unaifanya Azam kukalia nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi kwa kufikisha pointi 32 sawa na vinara Yanga huku wakizidiwa kwa tofauti ya mabao tisa.

Azam inaendelea kuonyesha ubabe katika michezo ya nyumbani ikipata ushindi kwenye michezo saba na kuwa kinara kwa timu zilizoshinda mechi nyingi katika uwanja wake.

Uwanja wa Ushirika mkoani Kilimanjaro Moses Phiri amefunga mabao mawili akiisaidia timu yake ya Simba kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Polisi Tanzania.

Mabao hayo ya Moses Phiri yanamfanya kufikisha mabao nane na kushika nafasi ya pili nyuma ya Fiston Mayele wa timu ya Yanga mwenye mabao 10.

Bao lingine la Simba katika mchezo huo limefungwa na John Bocco aliyefikisha mabao manne katika msimamo wa wafungaji huku bao pekee la timu ya Polisi likifungwa na Zuberi Mbogo kwenye dakika za nyongeza kipindi cha pili.