Category: STORY

YANGA YAENDELEZA REKODI

Timu ya Yanga imeendeleza rekodi yake ya ushindi katika mechi za ndani ya Nchi kwa kufikisha mechi 49 bila kupoteza baada ya kuifunga timu ya Mbeya City mabao 2-0.

Mabao yote ya Yanga yamefungwa na Fiston Mayele aliyetimiza idadi ya mabao 10 baada ya kucheza michezo 12 huku akiwa na mabao 19 katika michezo yote aliyocheza msimu huu pamoja na ile ya kimataifa.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha pointi 32 kileleni wakiwa na mechi moja mkononi watakayocheza na timu ya Ihefu Novemba 29 kwenye uwanja wa Highland Estates.

Timu ya Ruvu Shooting ilikua mwenyeji wa Singida Big Stars majira ya saa 10:00 alasiri na kupoteza kwa bao 1-0 lililofungwa na Frank Zakaria likiwafanya Singida kubaki nafasi ya nne katika msimamo wakiwa na pointi 24.

Ruvu inaendelea kusalia na pointi 11 huku ikiwa na pointi tatu zaidi ya timu inayokamata nafasi ya mwisho katika msimamo wa Ligi Ihefu SC.

Timu ya Namungo imepata ushindi wa tano msimu huu na kuifanya timu hio kufikisha pointi 18 na kuendelea kubaki nafasi ya nane katika msimamo wa Ligi Kuu NBC.

Ushindi huo ulihakikishwa dakika ya 82 kwa bao la Abdulmalick Hamza likiwa bao la 11 kwa timu ya Namungo huku mabao sita kati ya hayo yakifungwa na Reliants Lusajo.

SIMBA YAENDELEA KUSOTA UGENINI

TIMU ya Simba imeendeleza rekodi mbaya katika Ligi Kuu NBC inapocheza michezo ya ugenini baada ya kushindwa kuondoka na pointi tatu katika uwanja wa Sokoine Mbeya dhidi ya timu ya Mbeya City na kulazimishwa sare ya bao moja.

Simba wamecheza mechi sita ugenini na kufanikiwa kushinda mechi mbili pekee, kutoka sare tatu na kupoteza moja huku wapinzani wao wa jadi timu ya Yanga ikishinda mechi sita kati ya sita ilizocheza ugenini.

Mabao ya mchezo wa leo yamefungwa na Mzamiru Yassin dakika ya 15 kwa pasi ya John Bocco aliehusika katika mabao manne mpaka sasa katika mechi mbili mfululizo zilizopita huku bao la Mbeya City likifungwa na Tariq Seif dakika ya 79 kwa pasi ya Awadh Juma.

Baada ya kufanikiwa kupata alama moja timu ta Mbeya City imepanda mpaka nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi wakizidiwa alama mbili na timu ya Mtibwa Sugar pamoja na Singida Big Stars wenye pointi 21 huku simba ikisalia nafasi ya tatu na pointi 28.

Mkoani Singida timu ya Singida Big Stars baada ya kufungwa mabao 4-1 na timu ya Yanga mchezo wa raundi ya 12 leo imefanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC ya Dar es Salaam katika uwanja wa CCM Liti.

Singida ilijihakikishia ushindi kipindi cha kwanza dakika ya 40 kupitia kwa mchezaji wa zamani wa timu ya Simba aliewahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu kwa misimu miwili Meddie Kagere.

Ushindi wa leo unaifanya Singida kuendelea kushika nafasi ya nne wakifikisha pointi 21 na mchezo mmoja mkononi huku KMC ikisalia na pointi 14 katika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC.

Michezo miwili ya leo iliyopigwa mikoa ya Singida na Mbeya imekamilisha idadi ya michezo 100 tangu kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu NBC.

MAYELE AMPIKU SABILO UFUNGAJI BORA

BAADA ya kufunga mabao matatu ‘Hat-Trick’ katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Singida Big Stars mchezaji wa timu ya Yanga Fiston Mayele ameendelea kuwa mwiba kwa magolikipa baada ya kufunga magoli mawili leo dhidi ya Dodoma Jiji.

Mabao hayo yameisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa 2-0 na kuishusha timu ya Azam katika nafasi ya kwanza kwa tofauti ya mabao nane kwenye msimamo wa Ligi kwa kufikisha pointi 29 wakiwa na mechi tatu mkononi.

Hii ni mara ya kwanza kwa Fiston Mayele aliyemaliza nafasi ya pili msimu uliopita nyuma ya George Mpole katika wafungaji kuongoza katika msimamo wa vinara wa mabao msimu huu.

Mchezo huo umeshuhudia Tuisila Kisinda na Dennis Nkane wakitoa pasi za mabao zao za kwanza tangu kuanza kwa msimu huu na mechi ya pili kwa golikipa Abutwalib Mshery bila kuruhusu bao.

Ligi kuu NBC itaendelea tena kesho Novemba 23 kwa michezo miwili kati ya Singida Big Stars na KMC uwanja wa Liti Singida majira ya saa 8:00 mchana huku Mbeya City watakua wenyeji wa Simba uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya saa 10:00 alasiri.

MTIBWA YAISHUSHA MBEYA CITY, PRISONS HOI

TIMU ya Mtibwa Sugar imefanikiwa kuishusha timu ya Mbeya City katika nafasi nne za juu katika msimamo wa Ligi baada ya kuifunga Polisi Tanzania bao 2-1.

Polisi Tanzania ilikua ya kwanza kuandika bao kupitia kwa Ambrose Awio dakika ya 35 huku mabao ya Mtibwa yakifungwa na Ismail Mhesa dakika 45 kabla ya Onesmo Mayaya kufunga la pili dakika ya 48.

Huu ni mchezo wa pili mfululizo kwa Mtibwa kupata ushindi nyumbani ikiwa ni baada ya kuifunga timu ya Coastal Union idadi hiyo ya mabao katika raundi ya 12.

Ushindi huo unaisogeza Mtibwa nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu NBC kwa kufikisha pointi 21 ikiizidi Mbeya City kwa pointi tatu na mchezo mmoja.

Mkoani Mbeya Tanzania Prisons imeendelea kusuasua baada ya kupoteza mechi dhidi ya Kagera Sugar kwa bao 1-0 lililofungwa na Meshack Mwamita dakika ya 85 kwa shuti la mbali lililomshinda golikipa Edward Mwakyusa.

Timu ya Tanzania Prisons imepoteza mchezo wa tatu mfululizo iliyocheza nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar huku wakishuka mpaka nafasi ya 11 katika msimamo wa Ligi Kuu NBC.

Bada ya ushindi huo Kagera Sugar imepanda hadi nafasi ya tisa kwa kufikisha pointi 15 bila mchezo wowote mkononi.

AZAM YAENDELEA KUWA TISHIO

TIMU ya Azam imeendelea kuwa na mwenendo mzuri wa matokeo katika Ligi Kuu NBC baada ya kuifunga timu ya Namungo bao moja ugenini na kufanikiwa kukusanya alama zote tatu zinazowapeleka nafasi ya kwanza katika msimamo.

Bao hilo limefungwa na beki Edward Manyama dakika ya 29 na kuendeleza rekodi bora ya kutokupoteza mchezo wowote kwa kaimu kocha mkuu wa timu hiyo Kali Ongala.

Matokeo hayo yanaifanya Namungo kusalia na pointi 15 katika nafasi ya tisa huku wakiwa na ukame wa kushinda katika michezo minne mfululizo.

Mkoani Mbeya mchezo wa mapema timu ya Mbeya City imetoka suluhu dhidi ya Geita Gold matokeo yanayofanya timu hizo kulingana Pointi 18 kila moja huku Mbeya City ikiwa na uwiano mzuri wa mabao.

Mchezo mwingine uliopigwa uwanja wa Highland Estates timu ya Ihefu imepata ushindi wa pili msimu huu baada ya kuifunga timu ya Coastal Union mabao 2-1.

Mabao ya Ihefu yamefungwa na Never Tigere dakika ya 42 na Niko Wadada dakika ya 46 huku bao pekee la Coastal likifungwa na Mbarack Amza dakika ya 38 linalomfanya kufikisha mabao matano katika orodha ya wafungaji msimu huu.

Pamoja na ushindi huo Ihefu wanaendelea kusalia nafasi ya mwisho katika msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na alama nane baada ya michezo 12.