Category: STORY

YOUNG AFRICANS YAREJEA KILELENI LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Young Africans imeendelea kuonyesha kwanini inaiwakilisha nchi kwenye mashindano ya Afrika baada ya kushinda 3-1 dhidi ya Dodoma Jiji na kukwea hadi nafasi ya kwanza ya msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Young Africans iliyokuwa ya kwanza kuruhusu bao dakika nne kabla ya kipindi cha kwanza kutamatika kupitia kwa Edgar William haikukata tamaa na zikisalia dakika tatu mchezo kwenda mapumziko ilisawazisha kupitia kwa Laurindo Dilson akitumia mkwaju wa penati baada ya Andy Bikoko kumchezea rafu mchezaji wa Young Africans.

Kipindi cha pili Laurindo aliongeza bao na Prince Dube kupigilia msumari wa tatu na kupeleka furaha kwa ‘Wananchi’ na huzuni kwa ‘wakulima wa zabibu’.

Laurindo Dilson ‘Depu’ amekuwa na kiwango bora kwenye Ligi Kuu ya NBC tangu ajiunge na Young Africans akifunga mabao matatu na kutoa pasi ya bao moja huku akishinda tuzo ya mchezaji bora wa mchezo dhidi ya Dodoma Jiji na kufanikiwa kuifanya Young Africans kurejea kileleni ikifikisha jumla ya alama 22.

Young Africans inaungana na Azam Fc na kuwa timu pekee ambazo hazijapoteza mchezo hadi sasa kwenye Ligi Kuu ya NBC na zikiwa zimeruhusu mabao machache pia (2) huku ‘Wananchi’ wakiongoza kwa kufunga mabao hadi sasa (21).

Mkoani Tanga kwenye uwanja wa Mkwakwani Coastal Union ililazimishwa sare ya bao moja na timu ya KMC ikiwa sare ya pili kwa KMC iliyopoteza michezo nane hadi sasa na ikishika nafasi ya mwisho ya msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

KMC iliyoshinda mchezo mmoja pekee hadi sasa imefanikiwa kufikisha mabao matatu kwenye ligi hiyo ikiwa timu iliyofunga mabao machache hadi sasa huku ikiongoza kwa kufungwa mabao mengi (18).

Sare hiyo inaifanya Coastal Union iliyopoteza mchezo wao uliopita ugenini dhidi ya Namungo kukwea hadi nafasi ya 11 ikifikisha jumla ya alama 10 ikiwa imepata ushindi kwenye michezo miwili pekee.

 

MTIBWA YAENDELEZA MOTO LIGI KUU YA NBC

TIMU ya Mtibwa Sugar imefanikiwa kuondoka na alama tatu muhimu baada ya kuifunga Pamba Jiji bao moja katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliochewa katika dimba la Jamhuri mkoani Dodoma.

Mchezo huo uliokuwa mkali tangu mwanzo ulishuhudia timu zote zikicheza kwa tahadhari kubwa huku kila moja ikilenga kutumia vizuri nafasi zilizojitokeza ingawa wababe hao walienda mapumziko bila bao kupatikana.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kutengeneza nafasi na dakika ya 90+3 Twalib Hassan aliibuka shujaa wa Mtibwa Sugar baada ya kufunga bao la ushindi akitumia vyema nafasi ya mwisho na kuamsha shangwe kubwa kwa benchi la ufundi na mashabiki wa timu hiyo.

Bao hilo lilitosha kukusanya alama tatu kwa ‘wakata miwa’ huku Pamba Jiji ikilazimika kuondoka mikono mitupu licha ya kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo.

James Mwashinga wa Pamba aliibuka mchezaji bora wa mchezo huo licha ya timu yake kupoteza dakika za mwisho.

Mchezo wa mapema ulishuhudia ‘maafande’ wa Tanzania Prisons na JKT Tanzania wakigawana alama baada kutoka suluhu kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.

DODOMA JIJI, PRISONS KUUMANA LEO LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Dodoma Jiji itaikaribisha Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaochezwa leo majira ya saa 1:00 usiku kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Mchezo huo ni muhimu kwa timu zote mbili kwani zinapambana kujinasua ‘mkiani’ Dodoma Jiji ikiwa nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kucheza michezo tisa ikishinda mchezo mmoja ,kupata sare minne na kufungwa michezo mitano .

Mchezaji wa Dodoma Jiji Mwana Kibuta

Aidha Dodoma Jiji imeruhusu mabao 10 huku ikifunga mabao matano na kuweza kukusanya alama saba katika michezo hiyo.

Kwa upande wa Tanzania Prisons inashika nafasi 14 katika msimamo ikiwa imecheza michezo saba, ikishinda michezo miwili, sare mbili na kufungwa michezo minne.

Kwa upande wa alama timu hiyo imefanikiwa kukusanya alama saba, ikifunga mabao matatu na kufungwa mabao matano katika michezo hiyo.

MTIBWA SUGAR YASOGEA NAFASI YA NNE LIGI KUU YA NBC

 

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kwa mchezo mmoja uliochezwa katika uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma na kushuhudia Mtibwa sugar ikifanikiwa kuondoka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City.

Mtibwa Sugar ilianza mchezo kwa kasi na dhamira ya kutafuta ushindi mapema na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 27 baada ya George Chota kufunga bao la kwanza kwa shuti lililomshinda kipa wa Mbeya City Beno Kakolanya na kuwapa wenyeji uongozi wa 1-0.

Mbeya City haikukata tamaa na dakika ya 45+2 Eliud Ambokile aliisawazishia Mbeya City bao baada ya kutumia vyema krosi ya beki wa kulia Maranyingi na kufanya matokeo kuwa 1-1 hadi mapumziko.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa kutoka Mtibwa Sugar wakitafuta bao la ushindi na dakika ya 63 Said Mkopi aliibuka shujaa baada ya kufunga bao la pili kwa ustadi mkubwa lililowarejesha Mtibwa Sugar mbele na matokeo kuwa 2-1.

Mbeya City ilijaribu kurejea mchezoni kwa kuongeza kasi ya mashambulizi lakini safu ya ulinzi ya Mtibwa Sugar ilisimama imara hadi filimbi ya mwisho na kuhakikisha wanachukua alama tatu muhimu huku timu hiyo ikipanda hadi nafasi ya 4 kwenye msimamo wa Ligi Kuu wakifikisha na alama 14.

 

YOUNG AFRICANS ‘YAICHAPA’ MASHUJAA LIGI KUU YA NBC.

Young Africans imeendelea kuonyesha ubora wao katika Ligi Kuu ya NBC ilipokutana na Mashujaa katika wa uwanja KMC Complex baada ya kuichapa Mashujaa mabao 6-0.

Kikosi cha Young Africans kilitawala mchezo kuanzia dakika ya kwanza hadi mwisho huku wachezaji sita wakiandika majina yao kwenye orodha ya wafungaji.

Bao la kwanza lilifungwa mapema dakika ya 8 na Mohamed Damaro na dakika ya 28 Duke Abuya aliongeza bao la pili baada ya kumalizia pasi safi kutoka kwa Maxi Nzengeli.

Dakika saba baadae Pacome Zouzoua aliweka bao la tatu kwenye dakika ya 35 na Young Africans kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao matatu.

Kipindi cha pili Young Africans waliendelea kushambulia bila kuchoka na alikuwa Prince dube alifunga bao la nne dakika ya 79 kabla ya Mudathir Yahya kuongeza bao la tano dakika moja baadae na msumari wa sita wa ‘Wananchi’ ulipigiliwa na mshambuliaji wao mpya Laurindo Dilson ‘Depu’.

Ushindi huu unaipeleka Young Africans ‘kileleni’ mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Katika mchezo huu Mudathir Yahya alikuwa mchezaji bora wa mchezo huu