Category: STORY

MTIBWA HAIKAMATIKI,JKT YAREJEA KILELENI LIGI KUU YA NBC.

 

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kwa michezo miwili iliyochezwa mkoani Dodoma kwenye uwanja wa Jamhuri na jiji Dar es saalam katika uwanja wa Mej. Jen Isamuhyo.

Mchezo wa Kwanza uliopigwa saa kumi alasiri kati ya Mtibwa Sugar na Tanzania Prisons na kushuhudia Mtibwa sugar ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons.

Tanzania Prisons walitangulia kupata bao la mapema dakika ya nane kupitia kwa George Mpole akitumia mkwaju wa penati na Mtibwa sugar ilijibu mapigo kwa kusawazisha dakika ya 38 kupitia Magata Fredrick naye kwa mkwaju wa penati na dakika ya 87 Ismail Mhesa aliipatia Mtibwa bao la ushindi na kuwahakikishia alama tatu muhimu nyumbani.

Katika mchezo mwingine uliochezwa saa moja jioni maafande wa JKT Tanzania waliibuka na ushindi mnono wa Mabao 3-0 dhidi ya Pamba jiji ya Mwanza.

JKT walifungua ukurasa wa mabao dakika ya 34 kupitia kwa Valentino Mashaka bao lililowapa morali na kuwadhibiti Pamba jiji waliojaribu kujibu mashambulizi lakini walishindwa kusawazisha hadi kipindi cha kwanza kinatamatika.

Kipindi cha pili Salehe Karabaka aliendelea kuzamisha jahazi la Pamba jiji baada ya kufunga bao la pili dakika ya 55 na dakika ya 70 Valentino Mashaka aliyewapatia bao la tatu na kuihakikishia ushindi JKT.

Matokeo ya michezo hii yanaendelea kuongeza moto wa ushindani kwenye Ligi Kuu ya NBC huku JKT Tanzania wakiwa kileleni kwa alama 24 na Mtibwa Sugar ikishika nafasi ya tatu baada ya kukusanya alama 20.

COASTAL, TRA HAKUNA MBABE MKWAKWANI.

 

TIMU ya Coastal union imeshindwa kupata ushindi nyumbani kwenye mchezo wa pili mfululizo baada ya kulazimishwa sare ya bao moja na TRA kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC katika uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Coastal union ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 35 kupitia kwa Shiza Kichuya aliyesajiliwa kwenye dirisha dogo la usajili na kuipeleka Coastal mapumziko ikiwa kifua mbele.

Kipindi cha pili kilianza kwa TRA United kuonyesha nia ya kusawazisha mapema na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 48 kupitia kwa Denis Nkane alipofunga bao la kusawazisha.

Licha ya timu zote kutengeneza nafasi kadhaa katika dakika za mwisho hakuna aliyeweza kuongeza bao jingine na hivyo mchezo kumalizika kwa timu hizo kugawana alama.

Matokeo haya yameifanya kila timu kuongeza alama kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC, TRA ikiwa nafasi ya 8 na alama 13 na Coastal Union nafasi ya 11 na alama 11 kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Transit VS Kagera

NI VITA YA NAFASI NBC CHAMPIONSHIP LEO

LIGI ya Championship ya NBC inaendelea leo kwa michezo miwili mikubwa yenye uzito wa kipekee katika kupambania nafasi za juu na kuepuka hatari ya kushuka daraja.

Katika mchezo unaovuta hisia za mashabiki wengi, Transit Camp itaialika Kagera Sugar kwenye uwanja wa Filbert Bayi mkoani Pwani, huku mchezo mwingine ukizikutanisha Hausung na African Sports katika uwanja wa Amani, mkoani Njombe.

Transit Camp inayoshika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi ikiwa na alama 33, inaingia uwanjani ikiwa na lengo moja tu la ushindi na kukusanya alama tatu zitakazoiwezesha kufikisha jumla ya alama 36 na kupanda hadi nafasi ya pili, ikinufaika na faida ya matokeo ya ana kwa ana (head to head) dhidi ya Kagera Sugar.

Kwa upande wao, Kagera Sugar waliopo nafasi ya pili wakiwa na alama 36, wanahitaji ushindi ili kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC, wakisubiri pia kwa jicho la pili matokeo ya mchezo wa Geita Gold dhidi ya Barberian unaotarajiwa kuchezwa kesho.

Ushindani wa alama na nafasi baina ya timu hizo mbili unaipa mechi hiyo hadhi ya ushindani wa kweli, ikitarajiwa kuwa miongoni mwa michezo inayofuatiliwa kwa karibu zaidi leo, hasa kutokana na ubora wa vikosi na mwenendo wao katika michezo ya hivi karibuni.

VITA YA KUBAKI LIGI YA CHAMPIONSHIP YA NBC

Wakati huo huo, vita nyingine ya kusaka uhai itapigwa Njombe, ambapo Hausung na African Sports zitavaana katika pambano la kujiokoa dhidi ya mstari wa kushuka daraja huku timu zote mbili zikikusanya alama nane na zikitofautiana tu katika idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Ushindi kwa Hausung (nafasi ya 14) au African Sports (nafasi ya 15) utaifanya timu husika kupaa hadi nafasi ya 13 hatua muhimu katika mbio za kusalia Ligi ya Championship ya NBC.

Mchezo wa Transit Camp dhidi ya Kagera Sugar utarushwa mubashara (Live) kupitia chaneli ya FIFA+, kuwapa fursa mashabiki wengi kushuhudia moja ya michezo mikubwa ya msimu huu.

AZAM HAIJAPOTEZA MCHEZO KWENYE LIGI KUU YA NBC.

LIGI kuu ya NBC imeendelea kwa timu ya Azam kuwakaribisha TRA United katika dimba la Azam Complex kwenye pambano lililokuwa na ushindani mkubwa na Azam ikiibuka mbabe kwa kushinda mabao 2-0.

Azam wakicheza nyumbani walianza mchezo kwa kasi wakitawala umiliki wa mpira na kutengeneza nafasi zilizozaa matunda baada ya Jean Ngite kufunga bao la kuongoza dakika ya 28.

Kipindi cha pili dakika ya 70 Iddi Nado aliongeza bao la pili na kuwaamsha mashabiki wa Azam waliofurahia timu yao kuongeza bao na kumaliza na ushindi hivyo kusogea hadi nafasi ya tano ikifikisha alama 16.

Kwa matokeo hayo timu ya TRA United inashika nafasi ya 9 ikiwa na alama 12 katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC huku mchezo unaofuata itakuwa mgeni wa timu ya Coastal Union iliyopata sare katika mchezo uliopita nyumbani dhidi ya KMC inayoshika mkia kwenye msimamo.

VIWANJA VIWILI KUWAKA MOTO LIGI KUU YA NBC LEO.

LIGI Kuu ya NBC leo itaendelea mkoani Dar es Salaam katika viwanja viwili ambapo timu ya Simba itakuwa mwenyeji wa Mashujaa katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo majira ya saa 10:00 alasiri huku timu ya Azam ikiwaalika TRA katika uwanja wa Azam Complex Chamazi saa 1:00 usiku.

Simba ipo nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imecheza michezo sita, ikishinda michezo minne, sare moja na kufungwa mchezo mmoja huku ikikusanya alama 13.

Mchezaji wa Azam, Zidane Sereri

Mashujaa ipo nafasi ya nane katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikicheza michezo 10, ikishinda michezo mitatu, sare nne na kufungwa michezo mitatu huku ikikusanya alama 13.

Kwa upande wa timu ya Azam imecheza michezo saba hadi sasa bila kupoteza ikishinda michezo mitatu na sare nne na kufanikiwa kukusanya alama 13 katika michezo hiyo.

Timu ya TRA United ipo nafasi ya tisa katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa imecheza michezo nane, ikishinda michezo mitatu, sare tatu na kufungwa michezo miwili huku ikikusanya alama 12.