Category: STORY

WAANDISHI WA HABARI WANOLEWA DAR ES SALAAM.

 

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Leo Agosti 6 imeendesha semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuelekea msimu wa 2024/2025.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo Rais wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) ambaye pia ndiye mgeni rasmi alisisitiza waandishi kuwa na usawa katika kuwasilisha taarifa zao kwa jamii na waache tabia ya kuzungumzia timu pendwa tu kwani timu zote zinashiriki ligi moja.

“Mwaka ujao tumewapa nafasi timu ya ‘kupromote’ (kuzitangaza) mechi zao za nyumbani, na timu itakayofanya vizuri tutaipa tuzo” alisema Wallace Karia.

Semina hiyo ilimalizika kwa mchezo wa kirafiki kati ya watumishi wa Bodi ya Ligi na wanahabari ambapo ulimalizika kwa sare ya bao 2.

WANANCHI WAMEFURAHI.

 

TAMASHA la siku ya Mwananchi limehitimishwa Jana Agosti 4, 2024 kwa mchezo wa kimataifa wa Kirafiki kati ya Yanga na Red Arrows kutoka Zambia.

Bao la kusawazisha la Mudathir Yahya na la pili kwa mkwaju wa penati likifungwa na Ki Aziz yalitosha kuipa ushindi Yanga wa mabao 2-1 huku bao pekee la Red Arrows likifungwa na Ricky Banda.

Mgeni rasmi kwenye tamasha hilo alikuwa Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk Philip Mpango.

Yanga ilitumia nafasi hiyo kumkabidhi Dk Mpango kadi yake ya Uwanachama na jezi ya timu ya Yanga.

Wasanii mbalimbali walipata nafasi ya kutumbuiza wakiwemo Pado MC, Nzegele Boy, Billnass, Marioo na Harmonize, kwa upande wa singeli Meja Kunta alikuwepo.

Hii ni mara ya sita tamasha hili kufanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019 likiboreshwa msimu hadi msimu.

SIMBA DAY “YAFANA” BENJAMIN MKAPA.

I

‘IMEFANA’ ndivyo unavyoweza kusema, kilele cha SIMBA DAY kimefikiwa leo katika uwanja wa Benjamin Mkapa kwa mchezo wa kimataifa wa kirafiki kati ya Simba na APR ya Rwanda.

Mchezo huo umemalizika kwa Simba kushinda kwa mabao 2-0 mabao ya Simba yakifungwa na Deborah Fernandes na Edwin Balua.

Simba imetumia siku hii kutambulisha kikosi chake kitakachotumika msimu wa kimashindano wa 2024/2025.

Burudani ya muziki iliisindikiza siku hiyo kutoka kwa wasanii mbalimbali kutumbuiza akiwemo Ali Saleh Kiba lakini Pia Chino Kidd, Joh Makini na Oka Martin.

Ikumbukwe hii ni SIMBA DAY ya 16 tangu kuanzishwa kwake Mwaka 2009 na muasisi wake aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba Hassan Dalali.

LIGI KUU YA NBC RASMI AGOSTI 16.

 

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania imetangaza tarehe ya kuanza kwa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025 kuwa ni Agosti 16, 2024.

Kalenda ya matukio iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inaonyesha kuwa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025 itamalizika Mei 24,2025.

Taarifa hiyo imeeleza tarehe ya kuanza na kumalizika kwa Ligi za NBC Championship na Ligi ya First League msimu wa 2024/2025.

NBC Championship inatarajiwa kuanza Septemba 14, 2024 na kutamatika Mei 10, 2025 huku First League ikitarajiwa kuanza Novemba 23, 2024 na kutamatika Aprili 19, 2025.

TABORA UNITED YASALIA LIGI KUU YA NBC 2024/2025.

 

TABORA UNITED imefanikiwa kusalia Ligi Kuu ya NBC kwa msimu ujao wa 2024/2025 baada ya Leo kuifunga Biashara United mabao 2-0 hivyo Kuvuka hatua ya mtoano kwa ushindi wa jumla 2-1.

Ikumbukwe kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa mkoani Mara kwenye uwanja wa Karume Biashara United iliibuka na ushindi wa Bao 1.

Kabla ya kukutana na Biashara Tabora United iliianza hatua hii ya mtoano kwa kucheza na JKT Tanzania na kupoteza kwa jumla ya mabao 4-0 huku upande wa Biashara United wakishinda kwa jumla ya mabao 4-0 dhidi ya Mbeya Kwanza.

Sasa rasmi Tabora United itashiriki Ligi Kuu ya NBC huku Biashara United ikisalia Ligi ya NBC Championship msimu wa 2024/2025.