Category: STORY

TABORA , BIASHARA UNITED NANI KUKATA TIKETI YA LIGI KUU YA NBC 2024/2025?

 

MKOANI Tabora leo Juni 16 unapigwa mchezo wa marudiano kutafuta ushiriki wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025 unaozikutanisha timu za Tabora United na Biashara United.

Mchezo huu utapigwa kuanzia saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Ali Hassani Mwinyi, Tabora na kurushwa Mbashara na Azam Tv kupitia chaneli ya Azam Sports 1 HD.

Mchezo wa Kwanza uliopigwa katika uwanja wa Karume mkoani Mara ulimalizika kwa Biashara kuibuka na Ushindi wa Bao moja lililofungwa na Herbert Lukindo dakika ya 90+9 kupitia mkwaju wa penati.

Mshindi wa Jumla kwenye michezo hii miwili atashiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025.

MUDATHIR YAHYA NA REKODI YA BAO LA MAPEMA ZAIDI LIGI KUU YA NBC 2023/2024.

 

JUMLA ya mabao 517 yamefungwa kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2023/2024 huku rekodi ya bao la mapema zaidi ikishikiliwa na Mudathir Yahya.

Mudathir Yahya alifunga bao hilo sekunde ya 44 dhidi ya KMC mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro ukitumika Kama uwanja wa nyumbani wa KMC.

Mabao mengine ya mapema yalifungwa na Sospeter Bajana wa Azam FC sekunde ya 54 kwenye mchezo dhidi ya JKT Tanzania.

Yassin Mgaza wa Dodoma jiji, Awesu Awesu wa KMC na Ibrahim Ajibu wa Coastal Union wote wamefunga bao kwenye dakika ya kwanza.

Yassin mgaza akifunga dhidi ya Tabora UTD, Awesu Awesu akifunga dhidi Mashujaa na Ibrahim Ajibu akifunga dhidi Dodoma Jiji.

‘FEI TOTO’ NA REKODI YA HAT-TRICK YA MAPEMA ZAIDI LIGI KUU YA NBC 2023/2024.

 

MCHEZAJI Feisal Salum ‘Fei Toto’ ameingia kwenye rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga Hat-trick ya haraka zaidi Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2023/2024 akitumia dakika 9 .

Feisal Salum alifunga Hat-trick hiyo kwenye mchezo wa kwanza Ligi Kuu ya NBC dhidi Kitayosce iliyobadili jina na kuwa Tabora United katika dakika ya tatu, sita na 12 hivyo kutumia dakika tisa kufunga idadi hiyo ya mabao.

Msimu wa 2023/2024 Feisal Salum amehusika kwenye mabao 26 ya kikosi cha Azam akifunga mabao 19 akitoa pasi za mabao 7 na kuwa mchezaji wa Azam aliyehusika kwenye mabao mengi zaidi.

NTIBAZONKIZA MTAALAMU WA PENATI LIGI KUU YA NBC.

Jumla ya mabao 35 ya penati yamefungwa kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2023/2024 huku Said Ntibazonkiza akiibuka kinara kwa kufunga mabao Mengi (7).

Ntibazonkiza alifunga mabao hayo kwenye michezo dhidi ya Prisons, Kagera Sugar, KMC, Mashujaa, Singida FG, Geita Gold na JKT Tanzania.

Stephane Ki Aziz wa Young Africans anafuatia akifunga mabao matatu, Derick mukombozi wa Namungo FC akifunga mabao mawili sambamba na Lucas Kikoti wa Coastal Union huku waliosia wakifunga bao moja.

JKT YASALIA LIGI KUU YA NBC, TABORA KUIVAA BIASHARA UNITED.

 

JKT Tanzania imefanikiwa kubakia Ligi Kuu ya NBC baada ya hii Leo kutoka suluhu na Tabora United kwenye mchezo wa pili wa mtoano hivyo JKT Tanzania kusonga mbele kwa jumla ya mabao 4-0.

Mchezo wa kwanza wa mtoano uliochezwa kwenye uwanja wa Ali hassan Mwinyi mkoani Tabora ulishuhudia wenyeji Tabora United wakikubali kichapo cha mabao 4-0 dhidi ya wageni wao JKT Tanzania.

Sasa Tabora United itakwenda kujaribu bahati yao ya kusalia Ligi Kuu ya NBC kwa kuwavaa Biashara United iliyokuwa ikishiriki Ligi ya NBC Championship, mchezo wa kwanza utachezwa Juni 12 mkoani Mara huku mchezo wa pili utachezwa Juni 16.

Mshindi wa jumla kwenye michezo hiyo miwili atashiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025 na atakayepoteza atashiriki Ligi ya NBC ya Championship.