MCHEZAJI Duke Abuya wa Klabu ya Young Africans, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Disemba wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2025/26, huku Pedro Goncalves pia wa Young Africans akichaguliwa kuwa Kocha Bora wa Ligi hiyo kwa mwezi huo.
Duke alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo akiisaidia timu yake kushinda michezo miwili iliyocheza mwezi huo, pamoja na kuhusika katika mabao mawili kwa dakika 180 za michezo hiyo.
Mchezaji huyo aliwashinda Nassor Saadun wa Azam na Prince Dube wa Young Africans alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kwa upande wa Pedro aliyeingia fainali katika mchakato huo na Florent Ibenge wa Azam na Etienne Ndairagije wa TRA United, aliiongoza timu yake kushinda michezo miwili na kupaa kutoka nafasi ya nne hadi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo. Young Africans ilizifunga Fountain Gate (2-0), na Coastal Union (0-1).
Wakati huohuo Meneja wa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Said Mpuche, amechaguliwa kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Disemba kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.

Katika hatua nyingine mchezaji wa Transit Camp, Adam Uledi, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Disemba wa Ligi ya Championship ya NBC 2025/26, huku Shadrack Nsajigwa pia wa Transit Camp akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.
Uledi aliyeingia fainali katika mchakato huo na Obrey Chirwa wa Kagera Sugar na Boniface Mwanjonde wa Mbeya Kwanza, alionesha kiwango chenye mwendelezo ikiwa ni pamoja na kucheza dakika 450 za michezo mitano aliyocheza.
Kwa upande wa Nsajigwa aliyeingia fainali na Juma Kaseja wa Kagera Sugar na Zuberi Katwila wa Geita Gold aliiwezesha timu yake kushinda michezo yote mitano iliyocheza mwezi huo.