TIMU ya KMC ya Dar es Salaam imejihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi Kuu NBC msimu 2023/24 baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-0.
Ushindi wa mabao 2-1 walioupata Mbeya City katika mchezo wa awali jijini Mbeya, haukutosha kuwahakikishia mapema Wagonga Nyundo hao nafasi ya kucheza Ligi Kuu ya NBC 2023/24 baada ya kupoteza kwa jumla ya mabao 3-2.
Mabao ya Daruweshi Saliboko na Awesu Awesu yalitosha kuwafanya vijana hao wa Kinondoni kumaliza msimu wakiwa na uhakika wa kushiriki Ligi hiyo msimu ujao.
Kipigo hicho kinaifanya timu ya Mbeya City kusafiri mpaka Kigoma kucheza dhidi ya Mashujaa kwenye uwanja wa Lake Tanganyika tarehe 19 Juni kabla ya kurudiana tarehe 24 Juni kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Mshindi wa matokeo ya jumla kwenye michezo hiyo ndiye atapata nafasi ya kushiriki Ligi Kuu NBC msimu wa 2023/24 na atakayefungwa atashiriki Ligi ya Championship kwa msimu ujao.