LIGI KUU YA NBC KUENDELEA LEO.

LIGI Kuu ya NBC inaendelea kushika kasi ambapo michezo ya mizunguko ya 14,15 na 16 imepigwa katika mikoa mbalimbali.

Singida Black Stars waliwakaribisha KenGold katika uwanja wa CCM Liti mkoani Singida katika mchezo uliochezwa disemba 24, saa 8:00 mchana.

Mchezo huo uliozikutanisha timu hizo kwa mara ya pili kwenye Ligi Kuu ya NBC ulianza kwa kasi ambapo KenGold walifanikiwa kuanza kutikisa nyavu dakika ya 25 kupitia mchezaji wao Herbet Lukindo hivyo kwenda mapumziko wakiwa wanaongoza kwa bao 1.

Kipindi cha pili Singida walirudi kwa kasi na kufanikiwa kufunga mabao mawili kupitia wachezaji wake Josephat Arthur ambaye pia alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo na Elvis Rupia hivyo kufanikiwa kuweka kabatini alama 3 muhimu za mchezo huo.

Mchezo wa pili ulichezwa majira ya saa kumi na robo alasiri mkoani Dar es Salaam Simba wakiwakaribisha JKT Tanzania katika uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge.

Katika mchezo huo timu zote zilishambuliana kwa kasi dakika zote huku timu ya JKT Tanzania wakiwa wanalinda lango lao kwa ustadi mkubwa kuzuia mashambulizi yaliyokuwa yakifanywa na Simba.

Simba walifanikiwa kupata bao dakika za nyongeza za mchezo huo kupitia mkwaju wa penati uliopigwa na mchezaji wao Jean Ahoua baada ya beki wao Shomari Kapombe kufanyiwa madhambi akiwa ndani ya boksi hivyo mchezo huo kuisha kwa 1-0.

Golikipa wa JKT Yakoub Suleiman alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kuonyesha kiwango kikubwa ndani ya dakika 90.

Disemba 25 Ligi Kuu ya NBC iliendelea mkoani Manyara na Dodoma katika mchezo wa kwanza uliopigwa saa nane mchana Fountain Gate ikiwakaribisha Namungo katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa.

Namungo walianza kwa kasi kwa kulisaka lango la mwenyeji wao ambapo dakika ya 10 ya mchezo huo mchezaji Pius Buswita alifanikiwa kuwaweka mbele Namungo na dakika ya 30 mchezaji wa Fountain Gate Salum Kihimbwa aliwafanikiwa kusawazisha hivyo kwenda mapumziko wakiwa 1-1.

Kipindi cha pili Namungo walifanikiwa kufunga bao la pili kupitia mchezaji wao Geofrey Julius hivyo kufanikiwa kuondoka na alama tatu za mchezo huo na pia alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Mchezo mwingine ulichezwa jijini Dodoma ambapo Dodoma Jiji waliwakaribisha timu ya Yanga majira ya saa 10 alasiri katika uwanja wa CCM Jamhuri .

Yanga walianza kwa kasi na kufanikiwa kuutawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa ambapo dakika ya 19 mshambuliaji Clement Mzize alianza kutikisa nyavu za wenyeji wao, dakika ya 29 Aziz Ki aliongezea bao na dakika chache baadae Mzize aliongezea bao la 3 hivyo Yanga kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao matatu.

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kuendelea kutawala mchezo huo ambapo dakika ya 63 Prince Dube alifunga bao la 4 kwa Yanga na mshambuliaji wa Yanga Clement Mzize alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kufunga mabao mawili na kiwango kikubwa alichoonyesha katika mchezo huo.

Ligi Kuu itaendelea leo siku ya kufungua zawadi za Krismasi mkoani Mbeya ambapo timu ya Prisons watawakaribisha Pamba kutoka Mwanza saa 10:00 alasiri.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *