LIGI KUU YA NBC YAENDELEA KUSHIKA KASI

 

LIGI kuu ya NBC imeendelea kushika kasi kwa michezo mitatu iliyochezwa kwenye viwanja vya Lake Tanganyika mkoani Kigoma, Tanzanite Kwaraaa mkoani Manyara na Majaliwa mkoani Lindi.

Mchezo wa kwanza uliopigwa saa 8 kamili mchana ulizikutanisha timu za Fountain gate na Mbeya city na kushuhudia Fountain Gate ikipoteza kwa bao moja lililofungwa na Habib Kyombo kwa mkwaju wa penati dakika ya 56.

Mbeya City iliyopanda daraja kutoka ligi ya Championship ya NBC imefanikiwa kuwa miongoni mwa timu tatu zilizokusanya alama tatu katika mzunguko wa kwanza huku mchezaji wa timu hiyo Habib Kyombo akiibuka mchezaji bora wa mchezo huo.

Mchezo wa pili ulipigwa kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma na kushuhudia maafande hao wakitoshana nguvu kwa sare ya bao moja.

Timu zote zilipambana kupata ushindi na alikuwa Mundhir Vuai wa Mashujaa dakika 78 aliyewapa uongozi kabla ya Paul Peter wa JKT kuisawazishia timu yake dakika nane baadae na kufanya mchezo huo kumalizika kwa sare.

Paul peter aliibuka shujaa wa mchezo huo baada ya kuonyesha mchezo mzuri na kuisawazishia timu yake bao lililoipa alama ugenini.

Mchezo wa tatu ulichezwa saa moja kamili usiku na kushuhudia Namungo ikitoshana nguvu na Pamba jiji ya Mwanza kwa sare ya bao moja.

Dakika 19 zilitosha kwa Pamba jiji kupata bao lililofungwa na Staphan Siwa na hadi mapumziko wageni walikuwa mbele kwa bao hilo.

Namungo walipambana kupata bao la kusawazisha na dakika ya saba ya nyongeza kipindi cha pili Abdulaziz Shahame aliwanyanyua kwenye viti mashabiki wa ‘Wauaji wa Kusini’ kwa bao la kusawazisha na kufanya ubao wa matokeo kusoma sare ya 1-1.

Cyprian Kipenye wa Namungo aliibuka nyota wa mchezo huo baada ya kuonyesha kiwango bora .

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *