MAFUNZO YA ‘VAR’ YAFUNGWA DAR ES SALAAM.

Kozi maalum ya Teknolojia ya Msaidizi wa Video (VAR) iliyofanyika kwa takribani siku 5 kwenye ukumbi wa uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es salaam imefungwa rasmi Jana Aprili 18, 2025 ikijumisha waamuzi 20 kutoka Tanzania Bara na Visiwani ikiwa ni mwendelezo wa Kozi hiyo yenye jumla ya moduli 6 mpaka kutamatika.

Kozi hiyo ambayo ni sehemu ya mkakati wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuhakikisha nchi inakuwa na waamuzi waliobobea kwenye matumizi ya teknolojia hiyo ya kisasa inayotumika kusaidia kutoa maamuzi sahihi uwanjani imefungwa rasmi Kwa awamu ya pili na Mkurugenzi wa Sheria, Habari na Masoko wa TFF Boniface Wambura ambaye pia ndiye msimamizi Mkuu wa Kozi hiyo inayowezeshwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Akizungumza baada ya kufunga rasmi awamu ya pili ya Kozi hiyo Mkurugenzi wa Sheria, Habari na Masoko wa TFF, Boniface Wambura aliwapongeza waamuzi waliomaliza mafunzo hayo na kuwataka kwenda kutumia vyema ujuzi walioupata kwa maendeleo ya soka la Tanzania.

Aidha Wambura alieleza kuwa Kozi hiyo ni muendelezo na kwamba TFF itaendelea kuwekeza kwenye teknolojia hiyo Kwa kutoa elimu Kwa waamuzi wengi zaidi na hata kuzalisha wakufunzi wazawa ili kuhakikisha usimamizi wa mechi nchini unaendana sawa na mabadiliko kulingana na wakati Kwa kufuata viwango vya kimataifa.

Ikumbukwe kozi hiyo ni hatua muhimu kuelekea maandalizi ya matumizi rasmi ya VAR katika mechi za ligi kuu ya NBC na mashindano mbalimbali yatakayofanyika ndani ya Tanzania.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *