Kiungo mshambuliaji wa klabu ya Simba, Elie Mpanzu amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Oktoba wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2026/27, huku Steven Barker pia wa Simba akichaguliwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.

Mpanzu alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo akiwashinda Iddi Selemani wa Azam FC na Nathaniel Chilambo wa Simba, alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo mitatu ambayo ilicheza mwezi huo na kushinda yote, huku nyota huyo akifunga mabao matatu.

Kwa upande wa Barker aliyeingia fainali na Florent Ibenge wa Azam na Juma Mgunda wa Namungo, aliiongoza Simba kushinda michezo yote mitatu iliyocheza mwezi huo na kupanda kutoka nafasi ya pili hadi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.
Kamati pia imeteua mabao matatu bora, ambayo yatapigiwa kura na mashabiki ili kupata bao bora la mwezi Oktoba. Mabao hayo ni Hassan Mubiru (Azam v Mbeya City), Elie Mpanzu (Simba v Young Africans) na Selemani Bwenzi (Simba V Mashujaa).
Kamati ya Tuzo pia imemteua Meneja wa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Jackson Mwendwa kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Oktoba kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.
Pia Kamati ya Tuzo imemchagua Ramadhan Kalanje wa KMC kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Oktoba wa Ligi ya Championship ya NBC, akiwashinda Abdulkarim Segeja wa Kigamboni na Hamdani Ally wa Transit Camp alioingia nao fainali.
Kwa upande wa Kocha Bora wa ligi hiyo, kamati ilimchagua Awadh Juma wa Mtibwa Sugar aliyewashinda Habibu Kondo wa Bandari na Mohamed Muya wa KMC alioingia nao fainali katika mchakato huo.