PRISONS WABABE WA MBEYA DABI LIGI KUU YA NBC

Mchezaji wa Mbeya City (kushoto) akichuana na mchezaji wa Tanzania Prisons

TIMU ya Tanzania Prisons imeendeleza ubabe wake katika mchezo wa dabi ya Jiji la Mbeya baada ya kuifunga timu ya Mbeya City mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliochezwa Uwanja wa KMC mkoani Dar es Salaam jana Oktoba 21.

Mchezo huo ulianza majira ya saa 10:00 alasiri ambapo timu zote zilikuwa zikipambana kupata alama tatu huku mashabiki wa timu zote mbili wakionekana kushangilia kwa bendi na ngoma zilizonogesha mchezo huo.

Mbeya City kinara wa Ligi Kuu ya NBC alianza mchezo kwa kushambulia sana lango la ‘hasimu’ wake huku Tanzania Prisons ikifanya mashambulizi ya kushtukiza na hadi timu zinaenda mapumzikoni hakuna aliyekuwa ametikisa ‘nyavu’ za mwenzake hivyo kuwapa kazi ya ziada makocha wakati wa mapumziko namna bora ya kujipanga kwa ajili ya kipindi cha pili.

Dakika ya 73 kipindi cha pili Tanzania Prisons ilipata bao la kwanza kupitia kwa Jeremiah Juma na dakika moja baadae Haruni Chanongo aliiongezea bao la pili na kufifisha matumaini ya Mbeya City kubakiza alama zote tatu nyumbani.

Tanzania Prisons wakishangilia

Dakika ya 87 Mbeya City ilipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Daniel Lukandamila hivyo mchezo kutamatika kwa Mbeya City kupoteza 1-2 na kuifanya ‘Purple Nation’ kupoteza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu.

Mchezaji wa Tanzania Prisons, Jeremiah Juma alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo kutokana na kiwango kizuri alichokionyesha ikiwa ni pamoja na kuwafungia ‘Wajelajela’ bao na kuonyesha kiwango kizuri akiisaidia timu yake kushinda.

Jeremiah Juma

Matokeo hayo yanaifanya Tanzania Prisons kupanda hadi nafasi ya tano ikiwa na alama sita huku Mbeya City ikiendelea kushikilia ‘usukani’ wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na alama saba.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *