MSHAMBULIAJI wa Singida Black Stars Elvis Rupia amekuwa kinara wa kuchana nyavu za timu mbalimbali za Ligi Kuu ya NBC kwa kufunga mabao baada ya kufanikiwa kuifungia mabao nane timu yake hadi sasa.
Rupia ameweza kufunga katika michezo ya Singida dhidi ya KenGold, Dodoma, Azam, Tabora na JKT Tanzania ndani ya michezo 16 ambayo timu yake imecheza na kufanikiwa kuipatia alama 33 ikiwa nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu.
Kiungo wa Simba Jean Ahoua anashikilia nafasi ya pili akiwa ameshafunga mabao saba na kuweza kusaidia timu yake kupata alama 40 huku ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu.
Selemani Mwalimu wa Fountain Gate anashikilia nafasi ya tatu akiwa amefunga mabao sita na kuiwezesha timu yake kupata alama 20 huku wakiwa nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu.
Clement Mzize wa Yanga anafuata licha ya kuanza msimu vibaya baada ya kuwa majeruhi mpaka sasa amefanikiwa kufunga mabao sita huku timu yake ikiwa imekusanya alama 39.
Leonel Ateba wa Simba amefunga mabao matano akiwa katika mbio za ufungaji bora kwa kuiwezesha timu yake kupata alama 40 huku wakiwa ndio vinara wa kukusanya alama nyingi kuliko timu yoyote.