TIMU ya Cosmopolitan kutoka Dar es Salaam imeshuka daraja kutoka Ligi ya Championship ya NBC na kuungana na Biashara United ya Mara hivyo rasmi timu hizo zitashiriki ligi ya First League msimu wa 2025/26.
Cosmopolitan imeshuka daraja baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Songea United kwenye mchezo wa mwisho wa ligi hiyo.
Timu hiyo imeshuka daraja huku ikiwa imefunga mabao machache (19) sawa na timu ya Kiluvya kutoka Dar es Salaam itakayocheza hatua ya mtoano kutafuta nafasi ya kusalia ligi ya Championship ya NBC.
Cosmopolitan imeaga ligi ya Championship ya NBC ikiwa imeshinda michezo michache (5) sawa na timu ya Transit Camp inayotafuta nafasi ya kusalia kwenye ligi hiyo endapo itashinda mchezo wake wa hatua ya mtoano dhidi ya Kiluvya.
 
					 
		 
		 
		 
		