Michezo mitatu ya Ligi Kuu ya NBC msimu huu mzunguko wa tisa imeshuhudia TRA ikilazimishwa suluhu nyumbani na Yanga, JKT Tanzania ikiibuka na ushindi wa bao bao moja dhidi ya Kagera Sugar huku Namungo ikiichapa Coastal Union mabao 2-1.
Baada ya suluhu hiyo iliyopatikana uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Yanga imeshindwa kupata ushindi kwenye mchezo wa pili mfululizo ikiwa ni baada ya kupoteza katika ‘Dabi’ ya Kariakoo dhidi ya mahasimu wao Simba.
Katika mchezo huo timu zote mbili zilishindwa kutumia nafasi zao kupata mabao hivyo kulazimisha kugawana alama baada ya dakika 90 za mchezo.
Katika mchezo wa pili uliochezwa uwanja wa Mej Jen Isamuhyo, timu ya JKT Tanzania waliikaribisha Kagera Sugar na kubaki na alama zote tatu baada ya ushindi wa bao moja.
Valentino Mashaka ndiye aliyeipa JKT Tanzania ushindi baada ya kufunga bao la pekee la mchezo dakika ya 61.
Ushindi huo unaifanya JKT kukwea hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikifikisha alama 16.
Namungo ilihitimisha michezo ya jana kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.
Namungo ilianza kwa kasi na kupata bao la mapema sekunde ya 17 kupitia Gamba Matiko lakini Coastal Union ilisawazisha dakika ya tisa kupitia Shiza Kichuya.
Hata hivyo Namungo iliendelea kupambana kutafuta bao la ushindi na juhudi zake zilizaa matunda dakika ya 66 baada ya Herbert Lukindo kufunga bao la pili kwa ‘utosi’ na kunyanyua mashabiki wake wa Namungo hivyo kuondoka na alama tatu muhimu.
Hizo ni alama tatu muhimu kwa kocha Juma Mgunda na vijana wake, zikiwafanya kufikisha alama 12 na kupanda hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.