YAKISALIA masaa machache kabla ya watani wa jadi wa soka la Tanzania timu ya Simba na Yanga kukutana kwenye uwanja wa Mkapa, Dar kesho majira ya saa 11:00 jioni nahodha msaidizi wa Simba Mohammed Hussein amesema wapo tayari kushinda mchezo huo ili kuendelea kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa Habari kuelekea mchezo huo Mohammed amesema “endapo tukipata alama tatu katika mchezo wa kesho tutakua katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi ili tupambane kwa Pamoja tushinde mchezo huo”
Nahodha huyo amesema pia presha ni kubwa kuelekea mchezo huo kwani hawajafanikiwa kushinda mchezo dhidi ya Yanga kwa kipindi kirefu hivyo wapo tayari kupambania nembo ya timu yao kuhakikisha wanarudisha heshima dhidi ya watani zao wa jadi.
“Unaposhindwa kupata matokeo mazuri dhidi ya mpinzani wako mkuu inaibua mijadala mingi sana na hiyo ni mojawapo ya sababu kuu inayotupelekea kesho tupambane kushinda mechi hiyo” alisema Mohammed.