KARIA AZITAKA KLABU LIGI KUU KUTOKA NA AZIMIO MOJA

Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wallace Karia amezitaka klabu za Ligi Kuu ya NBC kutoka na azimio moja mara baada ya mafunzo ya Weledi katika Uendeshaji wa klabu nchini kwa Watendaji Wakuu na Wenyeviti wa Klabu.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo Karia amesema kuwa Klabu zinapaswa kuwa na azimio moja kwa ajili ya ustawi wa soka letu hususani kwa upande wa matangazo wanayopata klabu.

“Ligi yetu imekua sana tunapaswa tuwe na azimio moja mfano kuhusu matangazo yanayoonekana wakati wa mechi zetu yanapaswa kuzinufaisha klabu zetu na sio wale wanaoandaa mabango hayo”alisema Karia na kuongeza,

“FIFA wameleta mafunzo haya kwa wakati muafaka nawashukuru sana natazamia kukaa na Bodi ya Ligi Kuu ili kuona namna ya kuongeza uwepo wa mafunzo kama haya kwa manufaa ya taifa letu na vizazi vijavyo vya soka hususani katika masuala ya utawala bora katika klabu za soka” alisema Karia.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mnguto amewashukuru FIFA kwa mafunzo waliyopata kwani klabu nyingi zitanufaika na ujuzi waliopata.

“Nawashukuru sana FIFA sisi kama Klabu za Tanzania tumenufaika kwa hizi siku mbili na tunatamani tupate muda mwingi zaidi kuwa nanyi” alisema Mnguto.

Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoandaliwa na FIFA wakishirikiana na TFF na Bodi ya Ligi yamefanyika Dar es Salaam katika hoteli ya Johari Rotana.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *