Ligi Kuu ya NBC ligi ya nne kwa ubora barani Afrika inarejea wikiendi hii febuari 1 baada ya mapumziko ya takribani mwezi mmoja .
Ligi hiyo itaanza kwa michezo miwili ya viporo vya mzunguko wa 16 ambavyo ni mechi za Yanga dhidi ya Kagera Sugar Februari 1 katika uwanja wa KMC mkoani Dar es Salaam.
Februari 2 Tabora United itakuwa mwenyeji wa Simba katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora katika mchezo uliokuwa umepangiwa tarehe mpya.
Mzunguko wa 17 utaanza rasmi februari tano hadi saba kwa michezo nane itakayochezwa katika viwanja mbalimbali nchini .
Akizungumza kuhusu kurejea kwa Ligi Afisa Habari wa Bodi ya Ligi (TPLB), Karim Boimanda amesema kuwa maandalizi yote yako tayari na kwa upande wa usimamizi Bodi iko tayari, timu, viwanja vimekaguliwa ubora wake viko na upande wa ratiba ilishatoka mapema” Amesema Boimanda na kuongeza kuwa
“Mapumziko ya Ligi yalitokana na uwepo wa michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyochezwa mwanzoni mwa mwezi januari kisiwani Pemba na pia uwepo wa fainali za kombe la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani yaani CHAN ambazo zilipaswa kufanyika februari kabla ya kusogezwa mbele hadi agosti 2 ambapo Tanzania,Kenya na Uganda ni nchi zinazoandaa michuano hiyo”.