LIGI Kuu ya NBC iliendelea jana Februari 14, 2025 kwa michezo minne kupigwa kwenye mikoa ya Tabora, Dar es Saalam, Mbeya na Kagera.
Mchezo wa mapema saa 8:00 Mchana ulizikutanisha Tabora United dhidi ya Kengold na kumalizika kwa sare ya bao moja, Bao kwa upande wa Kengold likifungwa na Selemani Bwenzi kwa mkwaju wa penati na kufikisha mabao matatu kwenye michezo mitatu ya Ligi Kuu ya NBC aliyocheza mpaka sasa huku bao la Tabora United la kusawazisha likifungwa na Heritier Makambo na kufikisha jumla ya mabao sita kwenye Ligi Kuu ya NBC mpaka sasa.
Mkoani Mbeya, Tanzania Prisons ikaialika Namungo kwenye uwanja wa Sokoine saa 10:00 alasiri na kumalizika kwa Namungo kuibuka na ushindi wa bao moja, ushindi huo unaipandisha Namungo hadi nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikifikisha Alama 21.
Young Africans ikiwa ugenini KMC Complex, Dar es Salaam ikaibuka na ushindi mnono wa mabao 1-6 dhidi ya KMC na kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikifikisha alama 49 kwenye michezo 19 ya Ligi Kuu ya NBC, Young Africans imefunga jumla ya mabao 48 mengi zaidi kuliko timu yoyote kwenye Ligi Kuu ya NBC mpaka sasa.
Kagera Sugar ikiwa katika uwanja wake wa nyumbani Kaitaba mkoani Kagera, imepata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate, imewachukua takribani siku 102 kwa Kagera Sugar kupata ushindi kwenye uwanja wake wa nyumbani kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu, Mara ya mwisho Kagera kupata ushindi ilikuwa ni Novemba 4, 2024 dhidi ya Dodoma Jiji ambapo iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Ligi hiyo inaendele leo Februari 15, 2025 kwa michezo miwili, mchezo wa kwanza ukizikutanisha Pamba Jiji dhidi ya Coastal Union saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mwanza huku Mchezo wa pili na wa mwisho ukizikutanisha Azam FC dhidi ya Mashujaa kwenye uwanja wa Azam Complex saa 1:00 usiku.