AMESHINDIKANA ndivyo unavyoweza kusema kwa golikipa wa timu ya Simba, Moussa Camara ambae ni kinara wa ‘hati safi’ katika michezo 19 Ligi Kuu ya NBC baada ya kuwaacha mbali wapinzani wake wa karibu.
Camara amesajiliwa na Simba katika dirisha kubwa la usajili anaongoza kutokuruhusu mabao ambapo mpaka sasa amekusanya hati safi 15 katika michezo ya Simba dhidi ya Tabora United nyumbani na ugenini,Fountain Gate,Prisons nyumbani na ugenini,Dodoma Jiji,Namungo nyumbani na ugenini,Azam,Mashujaa,JKT Tanzania,Pamba Jiji,Singida Black Stars,Ken Gold na KMC.
Pamoja na hati safi hizo Camara pia ndio golikipa ambaye ameruhusu mabao machache zaidi katika Ligi Kuu ya NBC ikiwa ni mabao 6 tu tangu msimu wa 2024/2025 uanze.
Golikipa huyo ameruhusu mabao katika mechi dhidi ya Coastal Union mawili,Young Africans,Kagera Sugar mawili na Fountain Gate mawili huku mabao mawili ni ya timu yake kujifunga dhidi ya Young African na dhidi ya Fountain Gate.
Patrick Munthali wa timu ya Mashujaa ndie anaefuatia kwa kukusanya hati safi akiwa nazo 10 katika michezo 20 aliyocheza mpaka sasa huku timu yake ikiwa imeruhusu mabao 18.
Mlinda mlango wa Young Africans Djigui Diarra ndio wa tatu kwenye hati safi akiwa amekusanya hati tisa na kuruhusu mbao tisa katika michezo 20 ambayo timu yake imeshacheza.
Mohamed Mustafa wa timu ya Azam amekusanya hati tisa pia wakiwa wameruhusu mabao tisa sawa na Young Africans.
Yona Amos wa Pamba Jiji amekusanya hati safi nane na ameruhusu mabao 18,Metacha Mnata wa Singida Black Stars akiwa ameruhusu mabao 17 na kukusanya hati safi 7 na Yakoub Suleiman wa JKT Tanzania akiwa na hati 7 na kufungwa mabao 15 katika michezo 20 waliyocheza mpaka sasa.
Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo kwa michezo miwili ya mzunguko wa 21 ambapo timu ya Tanzania Prisons itaikaribisha katika uwanja wa Sokoine timu ya Tabora United saa nane mchana na JKT Tanzania watakuwa wenyeji wa timu ya Kagera Sugar katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.