TIMU ya Azam imeshusha kipigo kizito cha mabao 5-0 kwa timu ya Tabora United na kulipa kisasi cha kufungwa 2-1 na timu hiyo kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza.
Dakika 11 zilimtosha Abdul Suleiman ‘Sopu’ kufungua ukurasa wa mabao kwa timu yake huku winga wa timu hiyo Gibril Sillah akiiongezea timu yake mabao mawili dakika ya 16 na 29 na dakika ya mwisho ya kipindi cha kwa Iddy Nado aliongeza jingine hivyo Azam Kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 4-0.
Kipindi cha pili Tabora walionyesha nia ya kutafuta bao kwa mashambulizi kadhaa kabla ya ndoto yao ‘kudidimizwa’ dakika ya 89 na mshambuliaji wa Azam Nassor Saadun ambaye aliongeza bao kwa timu yake na kufanya mchezo huo kutamatika kwa mabao 5-0.
Mabao mawili ya Gibril Sillah aliyeibuka mchezaji bora wa mchezo huo yanamfanya kufikisha jumla ya mabao 11 sawa na Pacome Zouzoua wa Young Africans kwenye msimamo wa vinara wa mabao.