LIGI KUU YA NBC YAZIDI KUSHIKA KASI.

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kwa michezo mitatu iliyotoa ushindani mkubwa huku Simba pekee ikifanikiwa kuondoka na alama tatu muhimu na michezo mingine kutamatika kwa sare. 

 

Katika Uwanja wa Mej. Jen Isamuhyo, Dar es Salaam, mchezo wa mapema ulikuwa kati ya JKT Tanzania na Fountain Gate uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 kwenye mchezo uliokuwa wa kukata na shoka.

 

Fountain Gate walionyesha makali mapema baada ya Juma Abushiri kufungua ukurasa wa mabao dakika ya 3 kabla ya Ismail Kader kuongeza la pili dakika ya 45 na kuwapa wageni uongozi wa mabao mawili kipindi cha kwanza. 

 

Kipindi cha pili JKT Tanzania walirudi kwa nguvu ambapo Salehe Karabaka alipunguza pengo dakika ya 54 kabla ya Paul Peter kuisawazishia timu hiyo dakika ya 86 kwa moja ya bao ‘kali’ la msimu huu na kufanya mchezo kumalizika kwa sare ya mabao 2-2. 

 

Mkoani Tanga katika Uwanja wa Mkwakwani, Simba iliondoka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union.

 

Coastal Union walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia Maabad Maulid dakika ya 8, lakini Simba waligeuza matokeo kupitia Libase Gueye dakika ya 37 kabla ya Anicet Oura kufunga bao la ushindi dakika ya 44 na kuipa Simba alama tatu muhimu ugenini.

 

Mkoani Lindi katika mchezo wa saa tatu usiku, Namungo na Mbeya City waligawana alama baada ya sare ya bao 1-1.

 

Namungo walitangulia kupitia Hassan Kabunda dakika ya 6 huku Mbeya City wakisawazisha kupitia Eliud Ambokile dakika ya 28.

 

Matokeo hayo yanaendelea kuongeza ushindani katika hatua za mwisho za msimu wa Ligi Kuu ya NBC na kufanya kila mchezo kuwa mgumu na wenye ushindani mkali.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *