Ligi Kuu ya NBC inaendelea kwa michezo mitatu muhimu ambayo inaweza kubadilisha nafasi za timu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.
Mchezo wa kwanza utaanza saa 10:00 alasiri katika Uwanja wa Mej. Jen. Isamuhyo ambapo JKT Tanzania watakuwa wenyeji wa Fountain Gate.
JKT Tanzania wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa nafasi ya 6 kwenye msimamo huku Fountain Gate ikiwa nafasi ya 11, alama tatu zina umuhimu mkubwa kwa pande zote mbili huku JKT wakisaka kusogea juu zaidi na Fountain Gate kujinasua kwenye eneo la chini.
Saa 12:30 jioni, macho yatahamia Uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga ambapo Coastal Union wataikaribisha Simba katika mchezo mwingine wa ushindani mkubwa.
Simba wanaingia wakiwa nafasi ya 2 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC wakisaka kuendelea kupunguza tofauti ya alama kileleni, huku Coastal Union wakiwa nafasi ya 12 wakihitaji matokeo mazuri kujiweka salama zaidi.
Mchezo wa mwisho leo utachezwa saa 3:00 usiku katika Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi ambapo Namungo watacheza dhidi ya Mbeya City ambayo haijapata matokeo ya kufurahisha hivi karibuni.
Mbeya city wakiwa katika nafasi ya 14 kwenye ya msimamo na Namungo wakiwa nafasi ya 13 wakisaka alama muhimu mbele ya mashabiki wao wa nyumbani ili kuboresha nafasi zao kuelekea mwisho wa msimu.
Michezo ya leo ina uzito mkubwa kwa timu zinazowania nafasi za juu pamoja na zile zinazopambana kujinasua kwenye maeneo ya chini ya msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.