Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Juni 8, 2026 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;
Ligi Kuu ya NBC
Mechi Namba 189: TRA United 2-1 Mtibwa Sugar
Mchezaji wa Mtibwa Sugar, Magata Fredrick amefungiwa michezo mitano (5) na kutozwaV faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kurudi uwanjani na kuwa sehemu ya mchezo licha ya kufanyiwa mabadiliko na timu yake.
Magata alifanya tukio hilo Sekunde chache baada ya kufanyiwa mabadiliko na alipoona timu yake ikishambuliwa alirudi uwanjani hivyo kufanya wachezaji wa timu ya Mtibwa kuwa 12. Baada ya shambulio hilo, Magata alitoka nje huku akijificha nyuma ya wachezaji wa timu yake ili asionekane na waamuzi. Kosa hili ni kinyume na kanuni ya17:30 kuhusu Taratibu za Mchezo.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:5(5.6) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Klabu ya TRA United imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Etienne Ndayiragije kutokuhudhuria kwenye mkutano wa waandishi wa habari siku moja kabla ya mchezo bila kutoa taarifa na badala yake alifika kocha msaidizi kinyume na kanuni ya 17:58 kuhusu Taratibu za Mchezo.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba 191: Coastal Union 1–2 Simba SC
Mchezaji wa Coastal Union, Meshack Abraham amefungiwa michezo mitatu (3) kwa kosala kumchezea mchezo usio wa kiungwana (rafu) mchezaji wa Simba Anicet Oura nakuhatarisha usalama wake.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:5 Udhibiti kwa Mchezaji.
Mechi Namba 193: TRA United 1–2 Fountain Gate
Klabu ya TRA United imetozwa faini ya Sh. 11,000,000 (milioni kumi na moja) kwa kosala Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Etienne Ndayiragije kutokuhudhuria kwenye mkutano nawaandishi wa habari siku moja kabla ya mchezo bila kutoa taarifa na badala yake kuwakilishwa na Kocha Msaidizi kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:58 kuhusu Taratibu za Mchezo.
Hili ni kosa la kujirudia kwa Kocha huyo ambapo licha ya klabu hiyo kukumbushwa kuhusu utekelezaji wa kanuni hiyo bado kocha huyo hakuhudhuria mikutano hiyo kwenye michezo mitano (5) mtawalia. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba 197: Simba SC 1-0 Dodoma Jiji FC
Klabu ya Simba imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la mtoto muokota mipira kuchukua chupa za maji zilizokuwa pembeni ya goli ya Dodoma Jiji nakumwaga maji yaliyokuwa ndani ya chupa hizo na baadae kuondoka na taulo la mlinda mlango wa Dodoma jiji.
Baada ya mtoto muokota mipira kuondoka na taulo hilo, mlinda mlango huyo na mchezaji Andy Bikoko walimfuata wakimtaka kurejesha taulo hilo, lakini baadhi ya washabiki wa Klabu ya simba waliokua karibu na eneo hilo walianza kurusha chupa zenye vimiminika kwa wachezaji hao wa Dodoma Jiji.
Kitendo hicho cha mtoto muokota mipira kumwaga maji, kuondoka na taulo na washabiki wa Simba kurusha chupa, vinatafsiriwa kutokuwa vya kiungwana.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:2 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Mshabiki wa klabu ya Simba, Omary Omary (maarufu kwa jina la Bomba) amefungiwa kuingia viwanjani kwa kipindi cha miezi 12 kwa kosa la kufanya fujo kwenye vyumba vyakubadilishia nguo vya timu ya Dodoma Jiji akimtuhumu kiongozi wa Dodoma Jiji aliyekuwa ndani ya chumba hicho na imani za kishirikina.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:2 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Mechi Namba 199: Young Africans 3-1 Namungo FC
Mashabiki wa Young Africans, Baraka Shekimweri (maarufu kwa jina la Baraka Yanga) na Abdulrahman Saidi (maarufu kwa jina la Fumau Mshairi) kwa Pamoja wamefungiwa kuingia viwanjani kwa kipindi cha miezi mitatu (3) kwa kosa la kukiuka utaratibu maalumu wa kuketi uwanjani.
Mashabiki hao kwa pamoja wakiwa na tiketi zenye hadhi ya kuketi kwenye jukwaa la VIP B, walilazimisha kwenda kwenye jukwaa lenye hadhi ya VIP A licha ya kuelekezwa na watu wa tiketi kuwa hawana sifa ya kuketi jukwaa hilo, Mashabiki hao waliruka uzio unaotenganisha maeneo hayo na kwenda jukwaa la VIP A kinyume na utaratibu maalumu wa uwanjani hapo.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:2 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Ligi ya Championship ya NBC
Mechi Namba 206: Mbuni 0-1 TMA
Klabu ya Mbuni ya Mkoani Arusha imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kutokuheshimu ratiba ya mtiririko wa matukio hivyo kuingia uwanjani kwa kuchelewa kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:33 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 kuhusu Taratibu za Mchezo
Mchezaji wa Mbuni, Yunus Lema ametozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kukwepa kupeana mikono na timu mgeni kabla ya mchezo ilihali alikuwa sehemu ya kikosi cha kwanza. Yunus alielekea kwenye benchi la timu yake wakati ambao timu mgeni na timu mwenyeji walikuwa wakipeana mikono kabla ya mchezo kuanza.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 41:5(5.4) kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji
Mechi Namba 207: African Sports 1-3 Polisi Tanzania
Klabu ya African Sports ya Mkoani Tanga imepewa adhabu ya onyo kali kwa kosa la kuwakilishwa na wawakilishi wanne (4) badala ya wawakilishi wa tano (5) kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:2(2.1).Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 kuhusu taratibu za mchezo.