Pazia la Ligi kuu ya NBC msimu wa 2022/2023 linafunguliwa rasmi hii leo Agosti 15, 2022 kwa timu nne za Ihefu SC, Ruvu Shooting FC, Namungo FC na Mtibwa Sugar FC kushuka katika viwanja viwili kuzisaka alama tatu.
Mchezo wa kwanza wa ufunguzi utazikutanisha Ihefu dhidi ya Ruvu Shooting majira ya saa 10:00 alasiri katika dimba la Highland Estate, Mbarali Mkoani Mbeya wakati mchezo wa pili utazikutanisha Namungo dhidi ya Mtibwa Sugar katika dimba la Benjamin Mkapa kuanzia saa 1:00 usiku.
Timu ya Namungo inatumia uwanja wa Benjamin Mkapa kama uwanja wake wa nyumbani baada ya uwanja wao wa Majaliwa, Lindi kuwa katika maboresho.
Msimu huu wa 2022/2023 unashirikisha jumla ya timu 16 ambapo kila timu itacheza jumla ya michezo 30 kwa mtindo wa nyumbani na ugenini na kufanya jumla ya michezo 240 sawa na michezo 120 nyumbani na 120 ugenini kwa timu zote.
