Tag: #NBCPL#STORY

COASTAL, JKT KUANZA NYUMBANI LEO LIGI KUU YA NBC.

 

LIGI Kuu ya NBC inarejea leo Septemba 29 kwa michezo miwili kuchezwa kwenye mikoa ya Tanga na Shinyanga.

JKT Tanzania watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar katika uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga saa 10 alasiri huku ukiwa mchezo wa kwanza wa JKT Tanzania kucheza nyumbani tangu kupanda Ligi Kuu ya NBC msimu huu wa 2023/2024.

Coastal Union itacheza kwa mara ya kwanza kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga saa 1:00 usiku dhidi ya Tabora United huku Coastal ikiwa haijapata ushindi wowote msimu huu.

LIGI KUU KUENDELEA LEO.

MZUNGUKO wa tatu wa Ligi Kuu ya NBC unatarajiwa kutamatika leo kwa michezo miwili kupigwa kwenye viwanja viwili tofauti vya mkoa wa Dar es Salaam.

Saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Uhuru, Dar timu ya Simba iliyoshinda michezo yote miwili mpaka sasa itakuwa mwenyeji wa Coastal Union ya Tanga ambayo bado haijapata ushindi katika mchezo wowote wa ligi msimu huu.

Timu ya Azam itakua mwenyeji wa Singida BS saa 1:00 usiku kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar ikiwa ni mchezo wa mwisho kuchezwa kwenye mzunguko wa tatu.

Azam inacheza na Singida huku ikiwa na rekodi ya kushinda michezo yote kwenye uwanja wa nyumbani huku Singida ikiwa haijapata ushindi wala kufunga bao kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu.

KMC YAANZA VYEMA NYUMBANI

TIMU ya KMC ya Dar imefanikiwa kupata ushindi wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC kwa mabao 2-1 dhidi ya JKT Tanzania ikicheza katika uwanja wake wa Uhuru, Dar.

Awesu Awesu na Waziri Junior ndio waliofunga mabao mawili na kuifanya JKT Tanzania kuwa timu iliyoruhusu mabao mengi mpaka sasa kwenye Ligi kuu ya NBC (7) sawa na KMC huku bao la JKT likifungwa na Edward Songo.

Ushindi huo umeipeleka KMC mpaka nafasi ya nane ikifikisha alama nne huku JKT ikisalia nafasi ya 10 nyuma ya Ihefu ya Mbeya.

POLISI YAONESHA MAKALI, PAMBA HAIKAMATIKI

TIMU ya Polisi Tanzania imepata ushindi wa kwanza kwenye Ligi ya NBC Championship dhidi ya Ruvu Shooting kwa bao 1-0.

Ushindi huo ulihakikishwa mapema dakika ya 15 kwa bao la Denis Mushi na kufanya Ruvu Shooting kupoteza mchezo wa pili mfululizo baada ya kufungwa dhidi ya FGA Talents mabao 2-1 katika mchezo wa ufunguzi.

Pamba ya Mwanza imeendeleza makali yake kwenye Ligi ya Championship baada ya leo kupata ushindi wa pili mfululizo kwa kuifunga Pan African ya jijini Dar es Salaam bao 1-0.

Bao pekee la Pamba katika mchezo huo likifungwa na Jamal Mtegeta kwa mkwaju wa penalti dakika ya 80.

Bao hilo ni la pili mfululizo kwa Jamal Mtegeta aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Dodoma Jiji, ambapo bao lingine alilifunga katika mchezo uliopita dhidi ya Cosmopolitan na Pamba ilishinda kwa mabao 4-0.

Ushindi huo unaifanya Pamba, kujichimbia kileleni mwa ligi hiyo ikivuna pointi sita huku ikiwa haijaruhusu bao, wakati Pan African inarejea Dar es Salaam na pointi tatu ilizozivuna kwenye ushindi wa mabao 3-2 mbele ya Copco FC.

TABORA UTD YATAMBA

Mkoani Tabora Tanzania Prisons imepoteza mchezo wa pili mfululizo dhidi ya Tabora United kwa mabao 3-1.

Tabora UTD iliyopoteza mchezo wa ufunguzi dhidi ya Azam kwa mabao 4-0 imepata ushindi huo wa kwanza kwa mabao ya John Ben aliefunga mawili na Erick Okutu huku bao la Prisons likifungwa na Samson Mbangula.

Prisons imeruhusu mabao sita kwenye michezo miwili iliyopita huku wakiwa na alama moja pekee waliyopata suluhu dhidi ya Singida Fountain Gate inayowaweka nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.