MZUNGUKO wa 28 wa Ligi ya NBC Championship utapigwa leo Aprili 13 kwa michezo nane kuchezwa kwenye mikoa Saba tofauti majira ya saa 10:00 alasiri.
Mkoani Mwanza michezo miwili itapigwa Copco itakuwa mwenyeji wa Polisi Tanzania kwenye uwanja wa CCM Kirumba huku Pamba ikiwa mwenyeji wa FGA Talents kwenye uwanja wa Nyamagana.
Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Mbuni kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya huku Stand United ikicheza dhidi ya Transit Camp kwenye uwanja CCM Kambarage mkoani Shinyanga na Cosmopolitan itaialika Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Mabatini, Pwani.
Michezo mitatu ya timu zilizo ndani ya nne bora kwenye msimamo wa Ligi ya NBC Championship inabeba hisia za watu wengi kutokana na kila timu kuwa na nafasi ya kupanda Ligi Kuu ya NBC.
Michezo hiyo ni Mbeya Kwanza dhidi ya Pan African kwenye uwanja wa Nangwanda mkoani Mtwara, Biashara United dhidi ya Green warriors kwenye uwanja wa Karume mkoani Mara na TMA dhidi ya KenGold kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha.
Michezo yote itachezwa saa 10:00 alasiri na baadhi ya michezo kurushwa mubashara kupitia chaneli za TV3, ST Bongo, TV3 YouTube na ST Bongo Youtube.