TIMU za Alliance Fc ya Mwanza na Lipuli ya Iringa zimeanza mashindano ya First League hatua ya Nane Bora vibaya baada ya kupoteza michezo yao ya ufunguzi.
Alliance ilipoteza dhidi ya Stand United ya Shinyanga kwa mabao 2-0 huku Lipuli ikifungwa na Cosmopolitan ya Dar es Salaam kwa mabao 3-1.
Timu za Alliance na Lipuli zilikuwa miongoni mwa timu zilizoshiriki hatua ya nane bora msimu uliopita Mkoani Mwanza huku zikifungwa na timu ngeni katika hatua hiyo msimu huu.
Cosmopolitan wanakwea nafasi ya kwanza kwenye kundi A wakiwa na Idadi kubwa ya mabao ya kufunga (3) dhidi ya Stand yenye mabao (2).
Ligi hiyo itaendelea tena Aprili 25 kwa michezo miwili ya Kundi B timu ya African Lyon ya Dar ikiikaribisha Rhino Rangers saa 10:00 alasiri na TMA ya Arusha ikiwa mwenyeji wa Dar City ya Dar saa 1:00 usiku huku michezo yote ikipigwa uwanja wa Azam Dar na kuonyeshwa Mbashara kupitia kituo cha televisheni cha Azam.