Author: Cynthia Michael

MASHUJAA,KMC HAKUNA MBABE LIGI KUU YA NBC

TIMU ya Mashujaa imeshindwa kubaki na alama zote tatu nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya bao moja na timu ya KMC kwenye uwanja wa Lake Tanganyika Mkoani Kigoma.

Mchezo ulianza kwa kila timu kupambania timu yake na dakika ya 11 Mundhur Vuai wa Mashujaa aliifungia timu yake bao la kuongoza na kuwanyanyua mashabiki wa Mashujaa waliojitokeza uwanjani.

Ikisalia dakika moja mchezo kumalizika huku Mashujaa ikiamini imeshakusanya alama zote tatu mchezaji Akramu Muhina aliisawazishia KMC na kufanya timu hizo kugawana alama.

Mashujaa imesalia nafasi ya 7 na alama 34 huku KMC ikiwa na alama 34 kwenye nafasi ya 10 na kujihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26.Akram Muhina wa KMC ndiye aliibuka mchezaji bora wa mchezo baada ya kuiokoa timu yake kwa bao la ugenini na kuipa tiketi ya Ligi Kuu ya NBC msimu ujao.

JKT YASHINDWA KUFURUKUTA UGENINI LIGI KUU YA NBC

MZUNGUKO wa 29 ulibaki na kicheko kwa timu ya Pamba jiji ilipokuwa mwenyeji wa JKT Tanzania mkoani Mwanza kwenye uwanja wa CCM Kirumba baada ya kuchomoza na ushindi ‘finyu’ wa bao 1-0 nyumbani.

Dakika ya 40 zilitosha kwa timu ya Pamba jiji kupata uongozi kwa bao lililofungwa na Zabona Mayombya.

Pamba jiji imejiweka nafasi ya 11 ikiwa na alama 33 huku JKT Tanzania ikisalia nafasi ya 6 na alama zake 35.

Katika mchezo huo mchezaji wa Pamba jiji Zabona Mayombya aliyefunga bao pekee alichaguliwa kuwa mchezaji bora na nyota wa mchezo huo.

KMC YAFUFUA MATUMAINI YA KUSALIA LIGI KUU YA NBC.

 

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kwa mchezo mmoja kati ya Tabora United iliyokuwa mwenyeji wa KMC kwenye dimba la Alli Hassan Mwinyi mkoani Tabora saa 10:00 na kumalizika Tabora United kupoteza kwa bao moja.

Deogratius Anthony wa KMC ndiye aliyeibuka shujaa wa KMC kwani bao lake la dakika ya 59 ndio lilipeleka maumivu kwa Tabora na kuifanya KMC kufikisha alama 33 na kupanda kutoka nafasi ya 13 hadi ya 9 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC huku ikisalia michezo miwili kumalizika kwa msimu.

Tabora United imeendeleza rekodi mbaya baada ya kupoteza mchezo wa sita mfululizo kwenye Ligi Kuu ya NBC ikisalia nafasi ya tano na alama 37 mbili zaidi ya JKT inayoshika nafasi ya sita.

Mchezaji wa KMC Deogratius Anthony alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kufunga bao pekee lililoleta utofauti kwenye mchezo huo.

KAGERA SUGAR RASMI NBC CHAMPIONSHIP

 

 

TIMU ya Kagera Sugar imeaga rasmi Ligi Kuu ya NBC baada ya timu ya Pamba Jiji kuifunga KenGold 0-2 ugenini na kufikisha alama 30 ambazo haziwezi kufikiwa na Kagera ikiwa itashinda michezo yake miwili iliyosalia.

Pamba Jiji ilipata bao lake la kuongoza kipindi cha kwanza lililofungwa na mchezaji Yonta Camara dakika ya 30 anayecheza kwa mkopo kwenye timu hiyo kutokea Singida Black Stars.

Kipindi cha pili Yonta Camara kwa mara nyingine aliipatia bao la pili timu yake Dakika ya 60 na kufanya matokeo kuwa 0-2 hivyo kuzamisha matumaini ya Kagera kuendelea kusalia Ligi Kuu ya NBC .

Pamba jiji imefikisha alama 30 ikiwa nafasi ya 11 huku KenGold ikiwa tayari imeshuka daraja baada ya kukusanya alama 16 ikicheza msimu mmoja pekee wa Ligi Kuu ya NBC tangu kupanda ligi ya NBC championship.

FOUNTAIN ‘HALI TETE’ LIGI KUU YA NBC.

 

Ligi Kuu ya NBC imeendelea mzunguko wa 28 JKT Tanzania ikiikaribisha Fountain Gate ya mkoani Manyara kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na ‘kuichapa’ mabao 3-1 na kuishusha hadi nafasi ya 13 ya msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Ilimchukua dakika saba pekee Mohamed Bakari kuwaamsha mashabiki wa JKT kwa kuipatia timu yake bao la kwanza baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Edward Songo.

Shiza Kichuya aliipatia JKT bao la pili dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza (45) na ‘Maafande’ kwenda mapumziko wakiongoza 2-0.

Edward Songo alipigilia ‘Msumari’ wa tatu dakika ya 60 na kuifanya Fountain kuwa timu iliyofungwa mabao mengi hadi sasa (54).

Dakika ya 86 Fountain Gate ‘Walijipata’ na kufunga bao la kwanza kupitia kwa William Edger hivyo mchezo kumalizika 3-1.

Fountain iliyoanza vyema
Msimu huu wa Ligi Kuu ya NBC imejikuta na muendelezo mbovu wa matokeo mazuri ikiwa miongoni mwa timu zilizopoteza michezo mingi (15) nyuma ya Kagera Sugar (16) na Ken Gold (17) zilizoshuka daraja.

Shiza Kichuya wa JKT aliibuka mchezaji bora baada ya kufunga bao na kutoa pasi ya bao hivyo kuifanya JKT kufikisha alama 35 na kukwea hadi nafasi ya sita ya msimamo.